Na
Veronica Simba, Dodoma
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki amekabidhi vitendea kazi mbalimbali vyenye thamani ya jumla ya
Dola za Marekani 350,000 kwa Ofisi za Madini za Kanda mbalimbali nchini.
Akikabidhi vifaa
hivyo kwa Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda hizo, jana Mei 4 2018 Makao
Makuu ya Wizara jijini Dodoma; Waziri Kairuki aliwataka wahusika kuvitunza
kutokana na gharama kubwa iliyotumika kuvinunua.
“Serikali imekopa kwa
ajili ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelezwa ili iweze kuchangia zaidi
katika uchumi wa nchi. Tunaamini vitawasaidia sana katika utendaji wa majukumu
yenu. Mvitunze.”
Akifafanua kuhusu
vifaa vilivyotolewa, Waziri alisema kuwa ni pamoja na kifaa maalum kinachotumia
teknolojia ya kisasa kung’amua uwepo wa aina ya gesi hatarishi kwa afya, chini
ya Migodi ya Madini.
Alisema kuwa kifaa
hicho kinamsaidia muhusika kutambua sehemu yenye hewa hiyo hatarishi na hivyo
kuchukua hatua stahiki za kujiepusha na ajali inayotokana na kuvuta hewa ya
aina hiyo.
Aidha, alitaja vifaa
vingine kuwa ni kifaa maalum cha kukuza taswira za madini kinachojulikana
kitaalam kama ‘Hand Lens’. “Kifaa hiki hutumika katika shughuli za
uthaminishaji madini ya vito ambapo husaidia kuyakuza madini husika katika
ukubwa unaotakiwa ili kukokotoa thamani yake halisi tofauti na unapotumia macho
ya kawaida,” alifafanua.
Vingine ni pamoja na
GPS zinazotumika kupima mipaka ya maeneo, ‘Printer’, viatu na sare maalum
vinavyotumika migodini, Kompyuta, na vifaa vingine vya kijiolojia.
Kwa upande wake,
Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Prof.
Shukrani Manya alisema kuwa vifaa hivyo vimetolewa kupitia Mradi wa Usimamizi
Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP).
Alisema kuwa, zoezi
la kugawa vifaa hivyo limefanyika katika awamu kadhaa, ambapo kwa awamu ya
kwanza, Kanda za Madini zilizogawiwa ni Kanda ya Kusini (Mtwara na Nachingwea),
Kanda ya Ziwa Nyasa (Songea, Njombe na Tunduru), Kanda ya Kusini Magharibi
(Chunya) na Makao Makuu ya Wizara (Ofisi ya Ukaguzi wa Migodi, wachimbaji
wadogo na utoaji leseni).
Nyingine ni Ofisi za
Madini za Singida, Dodoma, Morogoro, Tanga, Handeni, Musoma, Bariadi, Mpanda,
Kigoma, Mwanza, Geita, Bukoba, Arusha, Moshi, Mirerani na Tabora.
“Vifaa vilivyobaki ni
kwa ajili ya Ofisi za Shinyanga, Kahama, Kituo cha Uongezaji Thamani Madini
(TGC), Ofisi ya Biashara ya Madini na Ofisi ya Kamishna wa Madini, ambao ndiyo
wanaopatiwa leo hii,” alifafanua Prof. Manya.
Akizungumza baada ya
zoezi hilo la kukabidhi vifaa; Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof Idris Kikula
alisema kuwa, ni jambo la kutia faraja kwa kupata vitendea kazi kwa Ofisi hizo
za Madini, ambazo kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanyika
mwaka 2017, sasa ziko chini ya Tume.
Alisema kuwa,
upatikanaji wa vifaa hivyo vya kisasa utasaidia Tume kutimiza jukumu lake kubwa
la kusimamia mapato stahiki ya Taifa yanayotokana na shughuli za madini.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) akikabidhi vitendea kazi mbalimbali kwa baadhi ya Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Makao Makuu ya Wizara Dodoma, Mei 4 mwaka huu. |

No comments:
Post a Comment