Na
Greyson Mwase na Asteria Muhozya, Morogoro
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa zoezi la utoaji
wa leseni kwa ajili ya utafiti, uchimbaji na biashara ya madini linatarajiwa
kuanza muda wowote kuanzia sasa mara baada ya uanzishwaji wa Tume ya Madini.
Profesa
Msanjila ameyasema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari kwenye mkutano wa baraza la kwanza la wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini
Morogoro tarehe 07 Mei, 2018 wenye lengo
la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya
madini.
Akielezea
hatua iliyofikiwa ya zoezi hilo, Profesa Msanjila amesema kinachofanyika kwa
sasa ni uchambuzi wa maombi ya leseni zote zilizokwishawasilishwa na kampuni
mbalimbali zenye lengo la kujihusisha na shughuli za madini nchini.
Katika hatua nyingine, akielezea mkutano huo,
Profesa Msanjila amesema mkutano huo wa kwanza unaambatana na uzinduzi wa
Baraza la Wafanyakazi ambalo lipo kisheria.
Ameendelea
kueleza kuwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na
umuhimu wa baraza la wafanyakazi, muundo wa Wizara ya Madini na maadili katika
utumishi wa umma.
Ametaja
masuala mengine kuwa ni pamoja na mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa
fedha 2017/2018, mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 na marekebisho ya Sheria
ya Madini ya mwaka 2017.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula amesema kuwa
tayari tume imekaa na kuweka mkakati
kuhusu masuala ya leseni ili kuhakikisha kuwa leseni zinatolewa kwa
wakati baada ya zoezi la utoaji wa
leseni kusitishwa tangu Julai mwaka 2017.
Akielezea
hatua iliyofikiwa ya zoezi la uchambuzi wa leseni, Profesa Kikula amesema zaidi
ya leseni 8,000 zimeshachambuliwa na kusisitiza kuwa zoezi
litakapokamilika waombaji waliokidhi
vigezo watataarifiwa ili kuanza kufanya
taratibu za malipo.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi
la Wizara ya Madini, Agathon William amesema kuwa baraza la wafanyakazi ni
chombo muhimu kinachowaunganisha
wafanyakazi wa Wizara katika uongozi kwa pamoja mahali pa kazi ili kuleta tija
katika utekelezaji wa shughuli za Wizara.
Amesema
baraza huishauri Wizara juu ya kuongeza ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa
kuchukuliwa kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo na Wizara ni za kuridhisha
kulingana na malengo ya Taifa ya kuleta maendeleo na kupunguza umaskini kwa
kuanzisha viwanda vingi vitakavyoongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi wa Taifa.
Ameendelea
kusema kuwa baraza hilo hujadili na kushauri mipango na bajeti ya wizara na
kupima mafanikio na kuridhia utekelezaji wake pamoja na upandishwaji wa vyeo
wafanyakazi kutokana na miundo ya utumishi.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akitoa ufafanuzi katika mkutano huo
|
No comments:
Post a Comment