Na Greyson Mwase,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewapongeza
wakandarasi kwa kukamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi za Serikali katika eneo
la Ihumwa jijini Dodoma.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 27
Machi, 2019 mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo na kuonesha
kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.
“Nimefurahishwa sana na wakandarasi
waliochukua zabuni za kujenga majengo ya ofisi hizi, hivyo ninawaomba Wakala wa
Ujenzi Tanzania (TBA) watoe vyeti kwenye majengo ambayo yamekamilika kwa
asilimia mia ili waanze kutumia majengo hayo kama ilivyokusudiwa,” alisema
Majaliwa.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa
hakuridhishwa na ubora wa milango iliyopachikwa kwenye jengo la Ofisi
ya Makamu wa Rais pamoja na Jengo la Wizara ya Fedha na kuagiza milango hiyo
kubadilishwa.
Pia, Majaliwa ameliagiza Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka umeme mkubwa katika eneo hilo kwa wakati ili
majengo yakamilike kwa asilimia mia na kufikia azma ya Serikali ya kuhamia
katika mji wa Serikali baada ya ofisi hizo kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Mgufuli.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha,
Philip Mpango, amesema mradi wa ujenzi wa nyumba hizo umezalisha ajira kubwa
kwa vijana kutokana na kuajiri takribani watu 1141 walioshiriki katika ujenzi
huo.
Akizungumzia hatua iliyofikiwa katika
ujenzi wa Jengo la Wizara ya Madini, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amesema jengo la Wizara
limekamilika kwa asilimia 99, na kubainisha kuwa, mkandarasi yupo katika hatua
za mwisho ili aweze kukabidhi jengo hilo.
Sehemu ya Jengo la Wizara ya Madini lililopo
katika eneo la mji wa Serikali Ihumwa jijini Dodoma ambalo mpaka sasa
limekamilika kwa asilimia 99.
|
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati mbele) wakipata maelezo ya
hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Madini kwenye mji wa
Serikali, Ihumwa jijini Dodoma kutoka kwa msimamizi wa mradi wa ujenzi huo (kulia).
|
No comments:
Post a Comment