Thursday, March 29, 2018

Tanzania yaendelea kutekeleza malengo ya ICGLR

Na Mohamed Saif,

Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kutekeleza malengo na makubaliano mbalimbali ya Mpango wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ili kuleta tija kwenye shughuli za madini kwa Nchi Wanachama.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema hayo Machi 27, 2018 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa Kikanda wa Wataalam wa Madini ya Dhahabu katika Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR Regional Gold Expert Meeting) uliofanyikia Jijini Arusha.

Gambo alisema Tanzania imekuwa Mwanachama rasmi wa ICGLR Mwaka 2008 na kwamba tangu wakati huo imeendelea kutekeleza malengo ya mpango wa ICGLR ili kufanikisha udhibiti wa uvunaji haramu wa madini na kuhakikisha manufaa ya pamoja ya rasilimali husika yanapatikana kwenye Nchi Wanachama.

Malengo ya ICGLR ni kuwianisha sheria za nchi wanachama ili kuweka uwiano katika sheria za kudhibiti uvunaji haramu wa madini, kuwa na hati moja ya usafirishaji madini ya Tin, Tantalum, Tungsten (3TG) na dhahabu ili kuhakikisha kuwa madini hayo yanachimbwa na kutumika kihalali na kurasimisha shughuli za wachimbaji wadogo.

Malengo mengine ya ICGLR ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za uchimbaji madini, kuimarisha uwazi na uwajibikaji na kuwa na mfumo wa kanzidata utakaowezesha kufuatilia taarifa za uvunaji, usafirishaji na uuzaji wa madini.

Katika kutambua malengo hayo, Gambo alisema Nchi Wanachama wanao wajibu wa pamoja kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanafikiwa kwa manufaa ya wanachama wote.

Gambo alizungumzia changamoto mbalimbali zinazozikabili Nchi Wanachama ambazo ni pamoja na uvunaji haramu wa madini, utoroshwaji wa madini, uharibifu wa mazingira, ukosefu wa teknolojia na baadhi ya Nchi kuwa na changamoto za Kiusalama.

Hata hivyo alisema changamoto hizo zisiwe sababu ya kurudi nyuma badala yake juhudi za pamoja, mshikamano wa dhati unahitajika ili kukabiliana nazo na kuhakikisha zinatatuliwa.
"Ni jukumu letu sote kwa pamoja kuhakikisha tunafikia malengo bila kurudi nyuma hasa ikizingatiwa changamoto tunazokabiliana nazo ni nyingi na hatupaswi kukata tamaa wala kurudi nyuma," alisema.

Akizungumzia hali ya uchimbaji dhahabu nchini, Gambo alisema hivi sasa Tanzania inashika nafasi ya Nne Barani Afrika na kwamba juhudi mbalimbali zinaendelezwa za kurasimisha uchimbaji mdogo. Hata hivyo alisema changamoto kuu iliyopo ni utoroshaji wa madini hayo ambayo Serikali inaendelea kukabiliana nayo.

Gambo alielezea mabadiliko mbalimbali yanayoendelea kufanyika kwenye Sekta ya Madini nchini ikiwemo mabadiliko ya Sheria ya Madini kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akifungua rasmi Mkutano wa Wataalam wa Madini ya Dhahabu wa Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).

Wataalam wa Madini ya Dhahabu kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR wakiendelea na majadiliano Jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment