Na
Veronica Simba, Mara
Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini imetembelea na kukagua Mgodi wa Buhemba na ule wa
CATA Mining Ltd iliyopo mkoani Mara ikiwa katika ziara ya kazi Machi 15 mwaka
huu.
Mkurugenzi Mtendaji
wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku, aliieleza Kamati kuwa Shirika
limekamilisha upembuzi yakinifu katika mabaki ya dhahabu yaliyoachwa kipindi
cha nyuma ambapo umebaini kuwapo takribani tani 796,400 za mabaki ya mchanga wa
dhahabu yenye wastani wa kilo 852 za dhahabu.
“Aidha, upembuzi huo
ulibaini kuwa mabaki hayo ya mchanga yatachenjuliwa kwa kutumia teknolojia ya Carbon in Leach (CIL). Mtambo
unatarajiwa kuchakata mabaki ya mchanga wa dhahabu kiasi cha tani 246,240 kwa
mwaka,” alisema.
Aliongeza kuwa,
tathmini ya kiuchumi ya mradi imeonesha gharama za uwekezaji zinakadiriwa
kufikia Dola milioni 3.96 na kwamba gharama za uendeshaji kwa mwaka
zinakadiriwa kufikia Dola milioni 4.46 na kutarajiwa kuingiza faida inayofikia
Dola milioni 3.45 kwa mwaka.
Kuhusu tathmini ya
mashapo katika miamba migumu, Kamati ilielezwa kuwa taarifa za kitaalam
zinaonesha kwamba wakati Kampuni ya Meremeta inafunga uzalishaji katika mgodi,
kiasi cha wakia 600,000 zilisalia kwenye miamba migumu.
Akifafanua zaidi,
alisema kuwa STAMICO imeamua kufanya upya tathmini ya mashapo hayo ili
kujiridhisha. “Hadi sasa kiasi cha mashapo yenye wakia 441,772 kimethibitika
kuwemo kwenye miamba migumu kutoka katika migodi ya wazi. Ukadiriaji wa mashapo
unaendelea,” alisema.
Vilevile, ilielezwa
kuwa Shirika lilifanikiwa kuchoronga shimo moja katika eneo la Nyasanero ili
kutathmini mkanda mpya wa dhahabu. Tathmini kamili ya kiasi cha dhahabu
kilichopo kwenye mwamba itakamilika mara baada ya kupokea majibu ya maabara.
Akieleza zaidi,
alisema kuwa Januari mwaka huu, Shirika lilitangaza zabuni ya kumpata mbia wa
kushirikiana naye katika kuendesha mradi kwa njia ya ushindani. Alisema, tayari
Kampuni tatu zimenunua zabuni husika na kwamba uchambuzi wa zabuni hizo
unaendelea.
Katika Mgodi wa CATA
Mining Company Limited, Kamati ilielezwa kuwa Mgodi huo unamilikiwa kwa ubia
kati ya Mtanzania, Mahuza Mumangi na Raia wa Canada Stefan Nagy kwa uwiano wa
asilimia 50 kwa 50.
Akitoa taarifa kwa
Kamati ya Bunge kuhusu Mgodi huo, Kamishna Msaidizi wa Madini, Ofisi ya Madini
Musoma, Samwel Mayuki alisema kuwa Kampuni inamiliki leseni sita za uchimbaji
mdogo katika eneo la Kataryo ambapo kuna miundombinu mbalimbali ikiwemo mitambo
ya kusaga na kuchenjua madini.
“Kuanzia Julai 2016
hadi Juni 2017, Mgodi umezalisha kilo 241.3 za dhahabu zenye thamani ya Dola
8,880,240.57 sawa na wastani wa shilingi bilioni 19.5 za Tanzania. Mrabaha
uliolipwa ni Dola 355,209.66 sawa na shilingi milioni 781 za Tanzania,” alisema
Mayuki.
Aidha, Kamishna Mayuki
aliongeza kuwa, kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Novemba 2017 Mgodi
umezalisha kilo 62.4 za dhahabu zenye thamani ya Dola 2,239,659.86 sawa na
shilingi bilioni 4.9 za Tanzania. Kiasi cha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini
kilicholipwa ni Dola 134,388.56 na Dola 22,396.57 sawa na wastani wa shilingi
milioni 295.7 za mrabaha na milioni 49.3 za ada ya ukaguzi.
Vilevile, alisema
Mgodi umeajiri jumla ya wafanyakazi 351 ambao kati yao 318 sawa na asilimia 91
ni watanzania.
Hata hivyo, ilielezwa
kuwa changamoto kubwa inayoukabili Mgodi kwa sasa ni kusimamishwa kwa shughuli
za Mgodi kuanzia Juni 2017 kutokana na mgogoro baina ya wawekezaji husika na
Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambao ni wamiliki wa eneo hilo la uchimbaji.
“Hali hiyo
imesababisha hasara mbalimbali ikiwemo kusimama kwa ajira za watanzania 318,
kushindwa kurejesha mikopo ya Benki na hasara ya kupoteza mapato ya mamilioni
ya shilingi kutokana na kusimama kwa uzalishaji.”
Kamati iliiagiza
Wizara kuhakikisha inasaidia katika kushughulikia mgogoro huo ili shughuli za
uzalishaji katika Mgodi zirejee mapema.
Viongozi mbalimbali
wa Wizara walishiriki ziara hiyo wakiongozwa na Naibu Waziri wa Madini
Stanslaus Nyongo, ambaye aliahidi kwa niaba ya Wizara kutekeleza maagizo
yaliyotolewa na Kamati.
No comments:
Post a Comment