Monday, March 26, 2018

Madini ya ujenzi, viwanda yanachangia zaidi kwenye uchumi kupita mengine – Biteko


Ø Yachangia bilioni 7.1 mrabaha 2016/17

Ø Asema usimamizi mzuri unaweza kukuza mchango huo kufikia bilioni 15 kwa mwaka

Na Veronica Simba, Dodoma

Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, amesema kuwa madini ya ujenzi na viwanda yanaipatia Serikali fedha nyingi kupita aina nyingine zote za madini yanayopatikana nchini.

Akizungumza na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini Dodoma, Machi 22 mwaka huu akiwa kwenye ziara ya kazi, Biteko alisema kuwa takwimu za makusanyo ya Serikali zinabainisha hayo.

“Mfano mwaka 2016/17, takribani tani milioni 15.6 za madini ya ujenzi zilizochimbwa, zilizalisha shilingi bilioni 230.6; ambapo katika hiyo, ulipatikana mrabaha wa shilingi bilioni 7.1,” alisema.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Biteko alieleza kuwa, idadi ya wachimbaji wa dhahabu na madini mengine nchi nzima ikijumlishwa, haiwezi kufika hata robo ya wale wanaofanya shughuli za madini ya ujenzi nchini.

Alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inaongeza vituo vya madini ya ujenzi na viwanda kutoka 85 vilivyopo sasa nchi nzima hadi kufikia 174. “Nina uhakika tukiviongeza vituo kufikia idadi hiyo, tutakusanya mrabaha wa zaidi ya shilingi bilioni 15 katika madini hayo pekee.”

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alitoa wito kwa wakandarasi wote wanaotekeleza miradi mbalimbali hususan ya ujenzi wa barabara kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria ya madini inayomtaka kila mtu aliyepewa leseni kulipa tozo na kodi mbalimbali ambazo zimeelekezwa na sheria hiyo.

Alisema, Serikali haiwezi kukubali kuona mtu yeyote anafanya kazi ya ujenzi, amelipwa fedha na Serikali lakini yeye kwa upande wake hataki kulipa kiasi ambacho anapaswa kuilipa Serikali.

“Kama tuna watanzania ambao ni maskini na tunachukua mrabaha kwao, halafu kampuni kubwa yenye mtaji mkubwa, inayoendesha shughuli za ujenzi, iache kulipa kodi stahiki; hiyo haikubaliki,” alisisitiza.

Biteko alisema kuwa, Wizara ya Madini itaandaa utaratibu wa kukutana na kujadiliana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ambao ndiyo hupewa leseni kwa mujibu wa sheria, kuhusu namna bora ya kusimamia suala husika ili madeni yaliyopo yalipwe.

Maagizo hayo ya Naibu Waziri Biteko yalikuja kufuatia ripoti iliyosomwa kwake na Afisa Madini Mkazi Dodoma Silimu Mtigile, kuwa ofisi yake inakabiliwa na changamoto ya ukusanyaji mirabaha inayotokana na wakandarasi wa barabara.

“Katika miradi mikubwa ya barabara iliyopo Dodoma, ulipwaji wa mirabaha ya madini ujenzi kutoka kwa wakandarasi umekuwa wa kusuasua ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi 642,632,195.00 kimekusanywa, sawa na asilimia 33.11 kati ya jumla ya shilingi 1,941,177,853.23 zinazopaswa kulipwa,” alisema Mtigile.

Aliitaja miradi hiyo ya barabara kuwa ni barabara ya Dodoma kwenda Iringa, iliyotekelezwa na Kampuni ya CCCC, barabara ya Dodoma mjini hadi Mayamaya iliyotekelezwa na Kampuni ya Sinohydro; ambazo zote mbili zimekamilika pamoja na barabara kutoka Mayamaya hadi Mela inayotekelezwa na Kampuni ya CHICO inayotarajiwa kukamilika baada ya muda mfupi.

Naibu Waziri alisema kuwa, Wizara itaisimamia sheria ya madini katika kuhakikisha kila madau anatimiza wajibu wake ipasavyo. Aidha, aliiagiza Ofisi hiyo ya Madini Dodoma, kuhakikisha wanaendelea kufuatilia malipo husika na kutokuruhusu mitambo ya wakandarasi wanaodaiwa, iliyoko eneo la kazi, kuchukuliwa hadi pale watakapokamilisha malipo yao.

Aliwataka watumishi wote wa sekta ya madini kufikiria namna gani sekta hiyo itafanikiwa kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa. Pia, aliwakumbusha kuwa, mojawapo ya kazi kubwa ya Wizara ni pamoja na kuwalea wachimbaji wadogo waliopo ili wakue.

“Tusifanye kazi za kukamata tu. Tufanye kazi kubwa ya kuwalea watu hawa ili wafuate sheria. Ukiwafundisha wakafuata sheria, utatumia nguvu ndogo sana kuwakamata, kwa sababu watakuwa ni watu wenye uelewa tayari,” alisisitiza.

Katika taarifa yake kwa Naibu Waziri; Mtigile alibainisha mojawapo ya mafanikio makubwa ya Ofisi yake kuwa ni pamoja na ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli mwaka hadi mwaka, ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/17, lengo la kukusanya maduhuli lilikuwa jumla ya shilingi 1,200,000,000. Alisema Ofisi ilifanikiwa kutimiza lengo kwa kukusanya shilingi 1,444,100,922.00 sawa na asilimia 120.34.

Aidha, alibainisha kuwa lengo la mwaka 2017/18 ni kukusanya jumla ya shilingi 1,230,000,000.00; ambapo hadi kufikia Februari 28 mwaka huu, Ofisi yake imekusanya jumla ya shilingi 812,384,840.98 sawa na asilimia 66.05. Alisema kuwa, katika pesa hizo, makusanyo ya mirabaha ya madini pekee ni jumla ya shilingi 621,329,912.38 sawa na asilimia 76.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Biteko pamoja na kuipongeza ofisi ya madini Dodoma kwa jitihada na mafanikio iliyopata; alizungumzia makusanyo ya maduhuli kwa nchi nzima kuwa yanaleta matumaini baada ya mabadiliko ya sheria ya madini.

“Sheria hii tulipoibadilisha, imeongeza msukumo mkubwa kwenye usimamizi wa sekta na hivyo, kwa sasa ukusanyaji wa maduhuli umekuwa mzuri sana ukilinganisha na miaka iliyopita.”

Akitoa mfano, alisema kuwa, mathalani mwezi Februari mwaka huu, makusanyo yalikuwa zaidi ya asilimia 85. Alisema anaamini Wizara yake itavuka lengo ililowekewa la shilingi bilioni 250 kutokana na uwepo wa sheria hiyo nzuri inayosaidia kusimamia vizuri mapato ya serikali.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, akisalimiana na wafanyakazi wa Ofisi ya Madini Dodoma, alipowasili katika Ofisi hiyo akiwa katika ziara ya kazi, Machi 22 mwaka huu.


Baadhi ya wafanyakazi katika Ofisi ya Madini Dodoma, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani), alipotembelea ofisi hiyo na kuzungumza na wafanyakazi Machi 22 mwaka huu. Kutoka kushoto ni Halima Kikoti, Affa Edward Affa na Betilda Kirway.


Shughuli za uchimbaji madini ya nakshi zikiendelea katika Mgodi uliopo Ntyuka Dodoma, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) mgodini hapo Machi 22 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, akikagua tarazo zilizotengenezwa na mawe ya nakshi katika mgodi uliopo Ntyuka Dodoma, wakati wa ziara yake Machi 22 mwaka huu.


Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko na Ujumbe aliofuatana nao, wakikagua maeneo ya uchimbaji wa madini ya dhahabu yaliyopo kijiji cha Nholi wilayani Bahi, Machi 22 mwaka huu.


Sehemu ya shehena ya mawe ya nakshi aina ya Graphite. Taswira hii ilichukuliwa Machi 22 mwaka huu wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani) katika Mgodi uliopo Itiso wilayani Chamwino.

No comments:

Post a Comment