Na
Veronica Simba, Nzega
Uongozi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) umeridhia kukilea Chuo cha Madini Dodoma (MRI) baada
ya kuombwa na Wizara ya Madini ambayo ndiyo inamiliki Chuo hicho.
Dhamira hiyo iliwekwa
wazi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ilipotembelea na
kukagua Kampasi ya Chuo cha Madini iliyopo Nzega mkoani Tabora, Machi 17 mwaka
huu.
Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa
alisema kuwa UDSM ina uzoefu wa kutosha katika kulea vyuo mbalimbali hivyo iko
tayari kufanya kazi hiyo.
“Sisi tunataka
kuthibitisha kwamba tuko tayari kukilea hiki Chuo, kama tutapewa jukumu hilo.
Hii ni kwa sababu tunao uzoefu wa kutosha uliotokana na kulea vyuo vingine
mbalimbali vikiwemo SUA, Muhimbili, Mzumbe na vingine kadhaa,” alisema.
Aidha, aliongeza
kuwa, katika Mpango-Kazi walioundaa na kuuwasilisha wizarani, umebainisha kuwa
udahili wa wanafunzi utaanza mapema mwakani.
“Mwaka huu tumepanga
uwe wa maandalizi lakini mwakani tunapanga kuanza udahili wa wanafunzi wa UDSM
wanaosomea Kampasi ya Nzega na Dodoma.”
Awali, akiwasilisha
taarifa ya Chuo cha Madini kwa Kamati hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini
Profesa Simon Msanjila alisema kuwa Mpango wa Serikali ni kuifanya MRI kuwa
kitovu cha mafunzo ya kozi mbalimbali za madini hapa nchini.
“Wizara iliunda
kamati kwa ajili ya kupitia kitaalam
miundombinu yote iliyoko kampasi ya Nzega na Dodoma pamoja na kuangalia
uwezekano wa kuimarisha taaluma katika Chuo hiki; kuimarisha uendeshaji wa
Chuo; uanzishaji wa kozi mpya na hasa kukiwezesha Chuo kuwa cha mfano na kitovu
cha mafunzo ya kozi zote za madini nchini,” alifafanua.
Alisema kuwa, Wizara
imeshapokea taarifa ya Kamati husika na inaifanyia kazi ili kuangalia uwezekano
wa UDSM kukilea Chuo hicho.
Aidha, Profesa
Msanjila alieleza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa Kampasi ya Nzega ni kuongeza
wataalam wa kada ya kati katika sekta ya madini. Hivyo, pamoja na shughuli
nyingine za taaluma, Kampasi hiyo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa
vitendo katika fani za jiolojia na utafutaji wa madini, uhandisi wa uchimbaji
madini, uhandisi wa uchenjuaji madini, usimamizi wa mazingira migodini na
upimaji wa ardhi na migodi.
Vilevile, alieleza
lengo jingine kuwa ni kukipanua Chuo hicho kiweze kuendesha shughuli zake kwa
ufanisi zaidi, mathalani Kampasi ya Nzega ambayo ina migodi itakayowezesha
wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Chuo cha Madini
kilianzishwa rasmi mwaka 1982 kwa lengo la kutoa mafunzo ya kada ya kati katika
sekta ya madini. Chimbuko la wazo hilo lilitokana na mahitaji ya watendaji wa
kada hiyo.
Jumla ya wanafunzi
542 wamedahiliwa na Chuo kufanya mafunzo ya muda mrefu kwa nadharia na vitendo
katika fani mbalimbali za madini.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakikagua majengo mbalimbali ya Chuo cha Madini Kampasi ya Nzega, walipokuwa katika ziara ya kazi Machi 17 mwaka huu. |
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakikagua majengo mbalimbali ya Chuo cha Madini Kampasi ya Nzega, walipokuwa katika ziara ya kazi Machi 17 mwaka huu. |
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakikagua Mgodi wa Madini (Pit) uliopo katika Chuo cha Madini Kampasi ya Nzega, walipokuwa katika ziara ya kazi Machi 17 mwaka huu. |
No comments:
Post a Comment