Na
Veronica Simba, Dodoma
Naibu Waziri wa
Madini Doto Biteko ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya madini nchini,
kuzingatia sheria mpya ya madini ambayo inaelekeza namna bora ya usimamizi wa
sekta hiyo.
Alitoa wito huo jana,
Machi 22 mwaka huu kwa nyakati tofauti, alipokuwa katika ziara ya Mkoa wa
Dodoma, kukagua shughuli mbalimbali za madini.
“Moja ya mambo muhimu ambayo sheria mpya ya
madini inaelekeza ni kutunza rekodi za uzalishaji wa madini ili Serikali iweze
kujua ni kitu gani kinazalishwa na hatimaye tuweze kujua kodi gani zinalipwa na
wenye leseni husika,” alifafanua.
Aidha, Naibu Waziri
aliwataka wenye leseni kushirikiana na wachimbaji wadogo wa madini ili waweze
kunufaika kupitia kazi wanazofanya. “Kwa maneno mengine, asitokee mtu wa
kumnyanyasa mchimbaji mdogo eti kwa sababu tu ana leseni,” alisisitiza.
Vilevile, aliwaagiza
kuweka wigo kuzunguka mashimo yaliyo wazi ili kuonyesha hali ya tahadhari kuwa
eneo hilo ni hatari na linaweza kusababisha ajali, ikiwa ni hatua mojawapo ya
kuzingatia usalama migodini.
Akizungumzia
changamoto kuu iliyowasilishwa kwake na wachimbaji wa mawe ya nakshi aina ya
Granite na Dorelite Dyke katika maeneo ya Itiso wilayani Chamwino na Ntyuka Wilaya
ya Dodoma Mjini, kuhusu vibali vya kusafirisha mawe hayo nje ya nchi, Biteko
alisema kuwa awali Serikali ilisimamisha utoaji vibali hivyo kuzuia
usafirishaji wa mawe ghafi nje ya nchi.
“Changamoto
iliyokuwepo awali, ni kuwa wako watu walikuwa wanasafirisha madini nje ya nchi
yakiwa ghafi, yanaongezwa thamani huko kasha tunarejeshewa sisi tununue bidhaa
hizo.”
Akifafanua zaidi,
alisema kuwa, jambo linalotia moyo ni kwamba uongezaji thamani madini hivi sasa
umeanza kufanyika nchini kwa kiwango kinachotakiwa kusafirishwa nje ya nchi.
Alisema, jambo hilo hilo litaleta manufaa kwani thamani, ajira na teknolojia
vyote vitabaki ndani na manufaa yatabaki ndani ya nchi pia.
Alipongeza wachimbaji
wa mawe ya nakshi wa Itiso na Ntyuka ya kudhamiria kujenga mitambo ya uongezaji
thamani mawe hayo katika maeneo husika.
Alisema kiu ya
Serikali ni kuona madini yanayochimbwa Tanzania, yanaongezwa thamani nchini na
hatimaye kusafirisha bidhaa zinazotokana na madini hayo na kuziuza katika nchi
nyingine mbalimbali na siyo vinginevyo.
Aidha, Naibu Waziri
aliwasisitiza wamiliki wote wa leseni za madini kufanya kazi zao huku
wakizingatia kujenga mahusiano mema na jamii zinazowazunguka.
Alisema kuwa kmujibu
wa kanuni mpya iliyopo hivi sasa, mwenye leseni anapaswa kuwasilisha mpango
wake wa utoaji huduma kwa jamii (CSR) kwenye Halmashauri husika ili
iuthibitishe mpango huo kabla ya utekelezaji wake.
“Ule utaratibu wa mtu
anajifungia ofisini, anasema nitawajengea shule pasipo Serikali ya Kijiji au
Wilaya kujua, tumeufuta kwa sababu mwanzo ulikuwa unatengeneza matatizo mengi,”
alifafanua Biteko.
Alisema, Serikali
itafanya kazi ya kuangalia na kuthibitisha thamani halisi ya fedha
zitakazotumika katika mpango huo, ili kujiridhisha.
Naibu Waziri
alimwagiza Afisa Madini Mkazi wa Dodoma Silimu Mtigile kuandaa na kuendesha
semina siku ya Jumatatu, Machi 26 mwaka
huu, kwa ajili ya wachimbaji wa eneo la Nholi kuhusu sheria mpya ya madini,
kufuatia maombi waliyowasilisha kwake alipokuwa akizungumza nao.
Hata hivyo, alisema
kuwa semina za aina hiyo zitaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini
kote ili kuwajengea uelewa wa sheria hiyo mpya wadau wa madini waweze kufahamu
haki na wajibu wao.
Akizungumzia suala la
baadhi ya watu kueneza propaganda kuhusu sheria hiyo kuwa ni kandamizi; Biteko
aliwataka watanzania kupuuza kauli hizo kwani sheria husika imelenga
kuwanufaisha watanzania na siyo kinyume chake.
“Kama kuna bepari
anadhani kwamba tunaweza kurudi nyuma katika hili, amekwama. Heri tuwe na
wawekezaji wachache wanaofuata sheria kuliko kuwa nao wengi wenye kutaka tu
kuchuma mali na kuondoka.”
Katika ziara hiyo,
Naibu Waziri Biteko aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Dodoma Silimu Mtigile,
wataalam kutoka wizarani na ofisi ya madini Dodoma pamoja na viongozi wa Wilaya
na Halmashauri akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Elizabeth Kitundu.
No comments:
Post a Comment