Na
Veronica Simba, Dodoma
Naibu Waziri mpya wa
Madini, Dotto Biteko ameeleza kuwa anatamani kuiona sekta ya madini ikichangia
zaidi ya ilivyo sasa katika Pato la Taifa.
Ameyasema hayo mapema
leo, Januari 15 mjini Dodoma, alipowasili rasmi katika Ofisi yake ya Makao
Makuu na kupokelewa na viongozi mbalimbali pamoja na watumishi wa Wizara ya
Madini na wa Wizara ya Nishati.
Amesema kuwa, sekta
ya madini inaweza kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa kutoka asilimia
Nne ya sasa na kuweza kufikia asilimia 10 au zaidi ikiwa kutakuwa na
ushirikiano baina ya wafanyakazi wote na viongozi wa Wizara huku kila mmoja
akijituma kutimiza wajibu wake ipasavyo.
“Tujiulize hivi ni
kwanini hadi leo sekta hii inachangia asilimia Nne tu katika Pato la Taifa
badala ya kupanda hadi asilimia 10 au zaidi. Tubainishe ni madini yapi
yanayotupatia fedha nyingi zaidi na ni mbinu gani tutumie ili tuweze kupanda
zaidi,” amesisitiza.
Hata hivyo, Naibu
Waziri Biteko alibainisha kuwa ujio wake wizarani haulengi kubadili au kugeuza
mambo bali ni kuongeza nguvu zaidi kwa watangulizi wake katika kutekeleza yale
ambayo yameagizwa na Mheshimiwa Rais John Magufuli kwa niaba ya wananchi na
Taifa kwa ujumla.
“Tuombeane kwa Mungu
atupe kibali, hekima na uwezo wa kuyaona matatizo lakini zaidi sana atupe uwezo
wa kutekeleza majukumu yetu ili sekta hii ya madini iwe sekta ambayo ina
mchango mkubwa kwa Taifa letu.”
Aidha, amesema kuwa falsafa
yake ya utendaji kazi ni kwa kila mmoja kuheshimu nafasi ya mwenzake bila
kujali nafasi aliyonayo. “Binafsi ninaamini hakuna mkubwa kwenye kufanya kazi.
Ukubwa wako unaonekana kwenye matokeo ya kazi unayofanya. Kwa hiyo tushirikiane
wote. Mimi ninaamini katika nguvu ya ushirikiano,” amesisitiza.
Viongozi mbalimbali
waliompokea Naibu Waziri Biteko akiwemo Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani,
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu wa Madini Profesa Simon
Msanjila, wamemwahidi ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza kwa niaba
ya wafanyakazi wote wa Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati, Kaimu Kamishna wa
Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga amempongeza Naibu Waziri
kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo na kueleza kwamba wafanyakazi wanayo imani kubwa
kuwa atasimamia vema utekelezaji wa majukumu katika sekta husika.
“Hii ni kwa sababu
tunaamini unaifahamu vema sekta ya madini kutokana na kuwa umekuwepo kwenye
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa muda mrefu na umeweza
kuisimamia vizuri.”
Wafanyakazi wa Wizara
ya Madini na Wizara ya Nishati wana uhusiano wa karibu kikazi kutokana na
kufanya kazi kwa pamoja kwa muda mrefu katika iliyokuwa Wizara ya Nishati na
Madini kabla ya kutenganishwa na kuwa Wizara mbili tofauti. Hii ndiyo sababu
wangali wanashirikiana katika mambo mbalimbali kama hafla hii ya kumpokea Naibu
Waziri.
Naibu Waziri Biteko
aliteuliwa katika nafasi hiyo Januari 6 mwaka huu na kuapishwa tarehe 8 Januari
na Rais John Magufuli.
No comments:
Post a Comment