Na Asteria Muhozya,
Kampuni ya Saruji
ya Dangote imetakiwa kuwalipa kwa wakati Wachimbaji wa Madini ya Jasi ili
kuwawezesha kulipa kodi zao kwa Serikali kulingana na taratibu zilizopo.
Hayo yamesemwa
tarehe 19/01/2018 na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alipotembelea
kiwandani hapo wakati wa ziara yake ya kutembelea Mikoa ya Lindi na Mtwara.
Naibu Waziri
amesema kuwa, lazima Wachimbaji Wadogo wapate malipo yao kwa wakati baada ya kuuza
madini ili kuwawezesha kulipa kodi za Serikali pamoja na kurejesha mikopo yao
kwa wakati katika Benki walizokopa.
Pia, Naibu Waziri
Biteko ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuandaa rasimu ya Mkataba ndani ya
kipindi cha wiki mbili na kueleza kuwa, kuwepo kwa mkataba huo ambao
kutawawezesha Wachimbaji wadogo wa madini ya Jasi kutatua changamoto zilizopo
baina yao na Kiwanda husika.
“Andaeni rasimu
ya mkataba ili kila moja auze madini yake kwa bei inayoeleweka bila kuoneana na
kila moja apate faida anayostahili,” amesema Biteko.
Ameongeza kuwa
zipo changamoto za Wachimbaji wadogo kutokuwa na umoja na hivyo kuwataka kuwa
na umoja ili waweze kufanikiwa katika shughuli zao ikiwemo kuwepo na bei moja
ya madini yao.
Kwa upande wake,
Mkurugezi Mtendaji wa Mitambo ya uzalishaji wa katika Kiwanda cha
Saruji cha Dangote, Hemendra Raithatha amesema kuwa kulikuwepo na tatizo la
malipo isipokuwa hivi sasa tatizo limeshughulikiwa, na kuahidi
kuwa wachimbaji wa madini watalipwa kwa wakati.
Pia, Raithatha
ameongeza kuwa, kiwanda hicho kipo tayari kufanya kazi na Wachimbaji wa Jasi
kwa kuwa mali ghafi nyingi za kutengeneza Saruji zinatoka kwa wachimbaji hao
jambo ambalo linaimarisha mahusiano kati ya pande husika.
Aidha,
ameishukuru Serikali kwa Mahusiano mazuri kati yake na Kiwanda hicho na pia
amemshukuru Naibu Waziri kwa kutembelea kiwanda hicho.
Mbali na Naibu Waziri, ziara hiyo imehudhuriwa
pia na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mayigi Makolobela,
Watumishi wa Wizara ya Madini, Uongozi
wa Halmashauri ya Mtwara, Uongozi wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Jasi na Kamati
ya Ulinzi na Usalama.
Naibu Waziri
amefanya ziara yake ya siku tatu katika Mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo
ililenga kukutana na wadau wa sekta hiyo na kukagua shughuli zinazofanyika
ikiwemo kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo.
Eneo la uzalishaji
Kitalu Na. 1 katika Kiwanda cha Saruji cha Dangote.
|
No comments:
Post a Comment