Na
Veronica Simba, Dodoma
Naibu Waziri mpya wa
Madini Dotto Biteko ametembelea Chuo cha Madini (MRI) na kutoa changamoto
kadhaa kwa Menejimenti na wafanyakazi wote, ili kiwe na tija stahiki kwa Taifa.
Akizungumza baada ya
kutembelea sehemu mbalimbali za Chuo hicho kilichopo Dodoma, Januari 15 mwaka
huu, Naibu Waziri alieleza kutokuridhishwa kwake na utekelezaji hafifu wa
masuala kadhaa muhimu na hivyo kutoa changamoto kwa uongozi wa Chuo kuyafanyia
kazi mapema.
Moja ya mambo muhimu
aliyoelekeza yatekelezwe ni pamoja na matumizi mazuri ya rasilimali za Serikali
kwa manufaa ya Taifa. Aliwataka kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais John
Magufuli anayetaka rasilimali kidogo inayopatikana nchini itumike vizuri na
kuleta matokeo.
“Mathalani, viko
vifaa vya mamilioni ya shilingi katika baadhi ya maabara zenu na havijawahi
kufanya kazi kwa muda wa miezi Sita sasa. Vinachakaa na kuharibika tu. Akija
aliyetufadhili kununua vile vifaa, atatushangaa. Tutaonekana wote hatuna uwezo
wa kufikiri kumbe ni watu wachache tu wanaosababisha,”alisema.
Kufuatia suala hilo,
Naibu Waziri aliagiza maabara zote zenye vifaa ambavyo havifanyi kazi
zirekebishwe na zianze kufanya kazi kufikia mwisho wa mwezi huu wa kwanza.
Changamoto nyingine
aliyoitoa Naibu Waziri ni kwa Chuo kufanya tafiti ili kuisaidia Serikali kujua
mahitaji halisi ya rasilimali watu kwenye sekta ya madini.
“Ninyi ni tofauti
kabisa na taasisi nyingine zinazofanya biashara. Mkifanya vizuri, maafisa wetu
wa madini kule mikoani na kwingineko kwenye kanda watafanya kazi rahisi sana.
Kwa sababu ninyi mtakuwa mmeshafanya utafiti kwa niaba ya Wizara kugundua
mahitaji ya rasilimali watu kwenye sekta ya madini.”
Akifafanua zaidi, alisema
kwamba Wizara inategemea kupata chemchemi ya fikra kutoka kwenye taasisi hiyo
ya Chuo. Alisema, Chuo kinatarajiwa kuzalisha wataalam wazuri ambao watakwenda
kufanya kazi sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenda kufundisha wachimbaji
wadogowadogo namna nzuri ya kuchenjua madini kwa kuzingatia usalama wa
mazingira na kupata tija ili kupandisha hadhi ya mavuno ya rasilimali
wanayopata.
Aidha, aliongeza kuwa
haipendezi kuona Chuo kikifundisha vijana wengi wa kitanzania lakini kwenye
migodi kunakuwa na wafanyakazi wa kigeni wakifanya kazi ambazo watanzania
wanaweza kufanya.
“Changamoto kwenu
kama Chuo, je, vijana wetu mnawanoa kiasi cha kutosha kushindana katika soko la
ajira? Ninyi ni taasisi ya kitaaluma, mnatakiwa kuyaona mambo ya kesho leo. Na
mambo ya jana yawasaidie kuboresha kesho ya nchi hii.”
Vilevile, aliwataka
kuachana na utamaduni wa kulalamika kwa masuala mbalimbali badala yake
wahakikishe wanatimiza wajibu wao ipasavyo na matokeo ya kazi yao yaonekane.
Alisema, matokeo mazuri ya kazi ndiyo yatakayoihamasisha Serikali kuona umuhimu
wa kuboresha yale wanayoyalalamikia ikiwemo suala la maslahi.
Hii ni ziara ya
kwanza ya Naibu Waziri Biteko katika Chuo cha Madini tangu alipoteuliwa kushika
nafasi hiyo na kuapishwa na Rais John Magufuli Januari 8 mwaka huu, Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Chuo cha Madini (MRI) kilichopo Dodoma, alipowatembelea hivi karibuni. |
Sehemu ya wafanyakazi
wa Chuo cha Madini (MRI) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko
(hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati alipowatembelea hivi
karibuni kujitambulisha kwao na kujionea utendaji kazi wa Chuo hicho.
|
Naibu Waziri wa
Madini Dotto Biteko akikagua sehemu mbalimbali za Chuo cha Madini (MRI),
alipofanya ziara ya siku moja kujitambulisha na kujionea utendaji kazi wa Chuo
hicho, Januari 15 mwaka huu.
|
No comments:
Post a Comment