Monday, January 22, 2018

Na Rhoda James, Lindi

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka Wachimbaji wa Madini ya Jasi kuungana ili kuweza kuandaa Kanuni ndogo ndogo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto katika utekelezaji wa shughuli zao ikiwemo ya Bei ya Madini ya Jasi.

Aliyasema hayo tarehe 17 Januari, 2018, wakati alipowatembelea   Wachimbaji Wadogo katika ziara ambayo inalenga kutatua migogoro iliyopo katika sekta husika katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Naibu Waziri alisema kuwa bei ya madini ya Jasi imekuwa ikitofautiana kutokana na kukosekana kwa umoja baina ya wachimbaji wa madini hayo.
“ Jiungeni pamoja mpange bei ya kuuza Jasi kwa pamoja na mkiwa kitu kimoja changamoto hizi hazitakuwepo,” amesisitiza Biteko.

Pia, Naibu Waziri alisema kuwa, ameelezwa kuwa ipo changamoto ya miundombinu ya barabara na hivyo kuitaka Halmashauri ya Kilwa kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo   kwa kuwa  itatumka kwa  shughuli mbalimbali.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kusini, Mayigi   Makolobela alisema kuwa Jasi inayochimbwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara ina ubora wa asilimia 89-95 na iko juu ukilinganisha na Jasi inayopatikana nchi  jirani.

Vilevile, Makolobela ameeleza kuwa kiwango cha Jasi kilichochimbwa katika kipindi cha Mwezi Julai hadi Desemba, 2017 kilikuwa Tani 44,500 na gharama yake ilikuwa Shilingi bilioni 4.6.

Aliongeza kuwa, katika kiasi hicho cha Jasi kilichopatikana Serikali imekusanya Mrabaha wa shilingi milioni 138 kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2017.

Naye Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Jasi Mkoa wa Lindi, Peter Ludvick alimweleza Naibu Waziri kuwa ikiwa Serikali itawasaidia  suala la miundombinu hususan barabara wachimbaji watazalisha mara tatu ya kiwango wanachokizalisha hivi sasa.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, akitoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Jasi, Peter Ludvick (wa tatu kushoto). Naibu Waziri amemweleza  mwenyekiti huyo kuhusu umuhimu wa kuandaa Kanuni ndogo ndogo ambazo zitawasaidia wachimbaji wa madini hayo kukabiliana na changamoto ya Bei ya Madini ya Jasi.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akiwa katika kijiji cha Hotel Tatu katika eneo ambalo Madini ya Jasi yanahifadhiwa kwa muda tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kwenye viwanda mbalimbali nchini. Wengine katika picha ni Kamishna Msaidizi wa Kanda ya Kusini, Mayigi Makolobela (wa pili kushoto), wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Christopher Ngubiagai na Wengine katika picha Watumishi wa Madini pamoja na wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo.

No comments:

Post a Comment