Ø Katibu Mkuu Madini atoa siku 14
kwa uongozi kuwasilisha mpango mkakati
Na
Veronica Simba, Biharamulo
Serikali imetoa siku
14 kwa kampuni ya Stamigold, inayomiliki Mgodi wa Dhahabu uliopo Biharamulo
mkoani Kagera, kuandaa mpango mkakati wa kibiashara, utakaobainisha namna
itakavyojiendesha pasipo kuitegemea Serikali.
Agizo hilo lilitolewa
jana, Januari 6, 2018 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila
alipotembelea Mgodi huo na kuzungumza na Menejimenti pamoja na wafanyakazi
wake.
Profesa Msanjila
alisema kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Madini, ni kuona Kampuni tanzu
hiyo ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), inajiendesha kibiashara na
kiushindani ili ipate faida stahiki na kulinufaisha Taifa kama ilivyo dhamira
ya kuanzishwa kwake, na siyo vinginevyo.
“Menejimenti ya
Kampuni, Bodi pamoja na Menejimenti ya STAMICO, nawapa hadi tarehe 21 mwezi
huu, kila upande uwe umewasilisha mapendekezo ya kimkakati yanayobainisha namna
gani Stamigold itaweza kusimama yenyewe na kujiendesha kiushindani kama zilivyo
kampuni nyingine za kibiashara. Kwa upande wetu, Kamishna wa Madini na mimi
Katibu Mkuu pia tutakuja na mapendekezo yetu.”
Akifafanua zaidi, Katibu
Mkuu alisema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kampuni ya Stamigold
hivyo haitakubali kuona mgodi huo unaendeshwa kwa hasara. “Kila mtu awajibike
kwenye eneo lake,” alisisitiza.
Alisema, pamoja na
kuwa Stamigold ni kampuni ya Serikali lakini imesajiliwa na Taasisi inayotoa
leseni za biashara ya Brela, hivyo inapaswa kujiendesha kama kampuni nyingine
za kibiashara. “Kampuni ya serikali ambayo haifanyi biashara haiendi
kujiandikisha Brela. Ninyi mnafanya biashara hivyo lazima mfanye kazi
kibiashara.”
Aidha, Profesa
Msanjila aliutaka uongozi wa kampuni kuhakikisha unaweka wazi taarifa zote za
mapato na matumizi kwa wafanyakazi wote ili waelewe wanazalisha kiasi gani,
wanapata faida kiasi gani, matumizi ni kiasi gani na kama kuna hasara
ibainishwe wazi.
Alifafanua kuwa
utaratibu wa kuweka wazi mapato na matumizi kwa wafanyakazi wote utaondoa
manung’uniko kwani utaratibu wa kibiashara unamtaka mwajiri amlipe mfanyakazi
kulingana na mapato. “Huwezi kumlipa mtu mshahara hata pale ambapo hazalishi.
Hii siyo sawa kibiashara maana lazima utapata hasara. Huu ndiyo ukweli ndugu
zangu. Tubadilike. Hakuna hela ya kuchezea.”
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Mhandisi John Nayopa alimhakikishia Katibu Mkuu
kuwa maagizo yote aliyoyatoa yatatekelezwa ndani ya muda alioelekeza. Aidha,
aliwataka wafanyakazi wa Stamigold kutoa ushirikiano kwa kutoa maoni na ushauri
wao wakati wa kuandaa mpango mkakati huo utakaoiwezesha Kampuni kujiendesha
kibiashara.
Katika ziara hiyo,
Katibu Mkuu aliambatana na viongozi wengine wa Wizara akiwemo Mkurugenzi Msaidizi
wa Rasilimaliwatu, Miriam Mbaga, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa
Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahaya Samamba, Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa
Kagera, Paschal Bundala na Mhandisi Migodi kutoka wizarani, Kungulu Kasongi.
Baadhi ya wafanyakazi
wa Kampuni ya Stamigold, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake
hivi karibuni.
|
Baadhi ya wafanyakazi
wa Kampuni ya Stamigold, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake
hivi karibuni.
|
Wafanyakazi
mbalimbali wa Kampuni ya Stamigold wakitoa maoni yao kwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini, Profesa Simon Msanjila (hayupo pichani) alipowatembelea hivi
karibuni.
|
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini, Profesa Simon Msanjila (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na
wafanyakazi wa Kampuni ya Stamigold alipowatembelea hivi karibuni.
|
No comments:
Post a Comment