Na
Rhoda James, DSM
Naibu Waziri wa Madini
Doto Biteko amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kujitathmini ili kujua kama
linatakiwa kuendelea kuwepo.
Naibu Waziri wa
Madini, Biteko ameyasema hayo tarehe 16 Januari, 2018, wakati wa ziara yake
Makao Makuu ya STAMICO ambayo ililenga kufahamiana na Bodi, Menejimenti pamoja
na Watumishi wa shirika hilo.
Biteko amesema
Serikali ililenga kulitumia shirika hilo ili kuhakikisha kuwa linasimamia na
kutekeleza miradi mbalimbali ya madini nchini ukiwemo Mgodi wa Buckreef. “Mnazungumzia
mradi wa Buckreef mmefanya nini kuhusu mradi huu? amehoji Biteko.
Vilevile, Biteko
katika kikao hicho ameitaka STAMICO kuhakikisha inadhibiti utoroshwaji wa
madini ya Tanzanite nchini kwa kuhakikisha kuwa inaweka mikakati madhubuti ya
kudhibiti utoroshaji huo.
“STAMICO ni mbia
katika Kampuni ya TanzaniateOne ni lazima muweke mikakati ya namna gani ya
kudhibiti utoroshwaji wa madini haya,” amesema Biteko.
Aidha, amewataka
watumishi wa STAMICO kufikiria namna ambayo itawezesha shirika husika kuchangia
katika Pato la Taifa kwa kuwa mchango wa Sekta ya Madini bado ni kidogo.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji anaye Kaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji
wa STAMICO, Alex Rutagwelela akitoa taarifa ya shirika hilo amesema kuwa lengo
kuu la STAMICO ni kuhakikisha kuwa inarudi kama ilivyokuwa hapo awali.
Rutagwelela amemweleza
Naibu Waziri kuwa, Shirika linafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kusimamia na
kutekeleza miradi mbalimbali, kutoa ushauri kwa wachimbaji wadogo pamoja na
biashara ya kukodisha mitambo ya Uchorongaji.
Ameongeza kuwa, STAMICO
inaendelea na uchimbaji wa Makaa ya Mawe katika eneo la Kiwira – Kabulo,
Kukarabati maabara ya Makaa ya Mawe ya Kiwira ambayo itatumika kupima ubora wa
makaa hayo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Balozi Alexander Muganda amemweleza Naibu Waziri
Biteko kuwa, watayafanyia kazi maagizo yote na kumshukuru kwa kutembelea
shirika hilo katika ziara ambayo imelenga kuboresha utendaji, kuongeza ubunifu
ili shirika hilo liweze kuchangia zaidi
katika pato la Taifa.
Kamishna wa Madini,
Profesa Shukrani Manya ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini
akifafanua jambo katika kikao hicho.
|
No comments:
Post a Comment