Na
Mohamed Saif,
Kampuni
za Madini nchini zimetakiwa kufanya shughuli zake kwa uwazi sambamba na kufuata
Sheria za nchi ili kuepuka migongano.
Wito
huo umetolewa jijini Dar es Salaam Januari 29, 2018 na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini, Profesa Simon Msanjila kwenye mkutano na Balozi wa Canada nchini, Ian
Myles aliyeambatana na Mshauri masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii kwenye Tasnia
ya Uziduaji kutoka Serikali ya Canada, Jeffrey Davidson.
Ujumbe
huo ulimtembelea Katibu Mkuu Msanjila kwa lengo la kujadiliana masuala
mbalimbali kwenye Sekta ya Madini ikiwemo suala la Sheria ya Madini, masuala ya
uwajibikaji kwa jamii (CSR) yanayofanywa na kampuni mbalimbali zikiwemo za
kutoka nchini Canada na matarajio ya Serikali kwa kampuni (wawekezaji).
Profesa
Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazofanya shughuli zake nchini zinalazimika
kufuata taratibu na sheria za nchi ili kujijengea mazingira rafiki ya
utekelezaji wa shughuli husika.
Alisema
lengo la Serikali ni kuhakikisha Sekta ya Madini inanufaisha Taifa kwa ujumla
sambamba na wawekezaji na alibainisha kwamba lengo hilo litafikiwa ikiwa
kampuni husika zitatekeleza wajibu wake kwa uwazi kulingana na matakwa ya
sheria.
“Kampuni
zinazojihusisha na shuguli za madini zinapaswa kufanya shughuli zake kwa
usahihi na uwazi,” alisisitiza Profesa Msanjila.
Aidha,
Profesa Msanjila alisisitiza kuwa kampuni zinazojihusisha na shughuli za madini
nchini, zinapaswa kupata taarifa sahihi kutoka kwa Wataalam waliopo Serikalini ili
kupata mwelekeo sahihi wa dhamira ya Serikali.
“Kampuni
zinatakiwa kupata taarifa sahihi kutoka kwa vyanzo sahihi ili kufanya shughuli
zake kwa usahihi,” alisisitiza Profesa Msanjila.
Profesa
Msanjila vilevile alizungumzia dhamira ya Serikali ya kuhakikisha madini yanayochimbwa
nchini yanaongezwa thamani kabla hayajasafirishwa nje ili kukuza uchumi wa
Taifa.
“Madini
yakiongezwa thamani hapa nchini, faida ni nyingi ikiwemo ajira na pia mapato
yataongezeka kwani tutakuwa tumeelewa thamani halisi ya madini husika, kabla hayajasafirishwa,”
alisema.
Ili
kufikia dhamira hiyo, Profesa Msanjila alisema Serikali ipo kwenye mazungumzo
na kampuni zilizoonyesha nia ya kujenga viwanda vya kuyeyusha na kusafisha madini
(smelting and refining).
Mbali
na hilo, Profesa Msanjila alizungumzia suala la uwezeshaji wachimbaji wadogo wa
madini ambapo alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba wananufaika ipasavyo
na shughuli zao sambamba na mchango wao kwenye pato la Taifa kuonekana.
Alielezea
jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuwawezesha wachimbaji
wadogo ikiwemo uanzishaji wa vituo vya mafunzo vya mfano (centre of excellence)
ambavyo alivitaja baadhi yake kuwa ni Kituo cha Tanga, Geita na Mtwara.
Kwa
upande wake Balozi Myles alisema ni muhimu Serikali, Wawekezaji na Jamii kwa
ujumla kushirikiana na pia kuwa na lengo la wazi la namna ya kunufaika kutokana
na Sekta ya Madini.
Naye
Davidson aliahidi kuzungumza na kampuni za Canada kuelezea matarajio ya
Serikali kwao kwa namna mbalimbali ikiwemo suala la sheria, uwajibikaji kwa
jamii, mazingira na michango mbalimbali ya kampuni kwa maendeleo ya jamii.
“Nitawakumbusha
kwamba wanawajibika si kwa wanahisa wao peke yake bali pia kwa jamii wanapofanyia
shughuli zao,” alisema Davidson.
Mkutano
wa Katibu Mkuu wa Madini na Balozi wa Canada nchini ulihudhuriwa na watendaji
mbalimbali kutoka Wizara ya Madini akiwemo Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Kamisheni ya Madini, Profesa Shukrani Manya.
No comments:
Post a Comment