Monday, February 18, 2019

Watumishi Wizara ya Madini watakiwa kutoa huduma stahiki kwa wadau wake


Na Nuru Mwasampeta,

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka watumishi wa wizara kuhakikisha wanatoa huduma stahiki kwa watanzania ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Pombe Joseph Magufuli.

Aidha, amewataka watumishi hao, kila mmoja kulingana na majukumu yake  kujipima utendaji wake binafsi kabla ya kungoja vipimo vilivyopo kwa kuzingatia miongozo na taratibu za Utumishi wa Umma.

Naibu Waziri Nyongo, ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akifungua Mkutano wa Wafanyakazi wa Wizara kwa niaba ya Waziri wa Madini, Doto Biteko aliyekuwa katika utekelezaji wa majukumu mengine ya kitaifa.

Aidha, Nyongo amewaeleza watumishi hao kuwa wanao wajibu wa kuzingatia dhana nzima ya kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya Taifa na watanzania kwa ujumla.

Pamoja na rai ya kila mtumishi kujipima utendaji wake, Nyongo amewakumbusha kuzingatia matumizi ya Opras katika kutekeleza na kujipima namna kila mmoja anavyotekeleza majukumu yake.

Amesema Opras ni hitaji la kisheria kila mmoja hanabudi kulizingatia.
“Wote tnafahamu kuwa ipo miongozo mbalimbali inayotumika katika utendaji wetu wa kila siku hivyo ni rai yangu kuwa tuizingatie ili kutoa huduma stahiki kwa watanzania kwa ufanisi na viwango vinavyotakiwa.” Alisisitiza.

Aidha, Nyongo alieleza wajibu wa Wizara kwa kuzingatia miongozo iliyopo ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kazi yatakayowawezesha watumishi wake kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Pamoja na hilo, alikazia suala la kuwaendeleza watumishi, kuwajengea uwezo katika kazi zao pamoja na kushughulikia na kutatua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi.

Zaidi ya hapo, Nyongo alisisitiza suala la kuimarisha mawasiliano baina ya watumishi wa wizara lakini pia mawasiliano baina ya wizara na taasisi zilizo chini ya wizara na wadau wote wa sekta ya madini ili kuongeza ufanisi hatimaye kuongeza tija katika utendaji wa wizara.

Kuhusu kuzingatia suala la afya za watumishi, Nyongo ameipongeza wizara kwa kuratibu mara kwa mara suala la upimaji wa afya kwa hiari kwa watumishi wake na kutoa rai kwa kila mmoja kutumia fursa hiyo na kujitokeza kupima afya zao kwa hiari.

Akihitimisha hotuba yake,  Nyongo amewasihi  watumishi wa wizara kuongeza juhudi na kuelekeza fikra zao katika kupelekea serikali ya viwanda kutokana na ukweli kwamba sekta ya madini ni mojawapo ya nguzo ya uchumi wa viwanda na kuwa itasaidia katika kuifikisha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Kutokana na uwepo wa wastaafu katika mkutano huo, Nyongo alitumia fursa hiyo kuwapongeza sana wastaafu watano walijumuika katika mkutano na hafla fupi ya kuwaaga na kuwatakia maisha mema katika hatua nyingine ya maisha.

Kwa uande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Nsajigwa Kabigi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila alisema mkutano huo umelenga katika kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji ya wizara ili kupata mwelekeo wa namna bora ya kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu na shughuli za kila siku za wizara pamoja na kubadilishana mawazo, kufurahi pamoja na kuwaaga wastaafu.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwa katika picha pamoja na makundi mbalimbali yaliyoshiriki mkutano wa wizara na hafla ya kuwaaga wastaafu kutoka Chuo Cha Madini (MRI) na Wizara ya Madini Makao Makuu 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwa katika picha pamoja na makundi mbalimbali yaliyoshiriki mkutano wa wizara na hafla ya kuwaaga wastaafu kutoka Chuo Cha Madini (MRI) na Wizara ya Madini Makao Makuu 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwa katika picha pamoja na makundi mbalimbali yaliyoshiriki mkutano wa wizara na hafla ya kuwaaga wastaafu kutoka Chuo Cha Madini (MRI) na Wizara ya Madini Makao Makuu 



Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwa katika picha pamoja na makundi mbalimbali yaliyoshiriki mkutano wa wizara na hafla ya kuwaaga wastaafu kutoka Chuo Cha Madini (MRI) na Wizara ya Madini Makao Makuu
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwa katika picha pamoja na makundi mbalimbali yaliyoshiriki mkutano wa wizara na hafla ya kuwaaga wastaafu kutoka Chuo Cha Madini (MRI) na Wizara ya Madini Makao Makuu

Kampuni ya Jervois yaonesha nia kuwekeza Kabanga


Na Asteria Muhozya,

Waziri wa Madini Doto Biteko amekutana na Wawakilishi wa Kampuni ya Jervois Mining Limited ya Australia ambayo imeonesha nia ya kuwekeza katika mradi wa Nikel- Colbat, Kabanga. 

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko ameendelea kusisitiza kuhusu kufuatwa kwa Sheria na taratibu kwa wenye nia ya kuwekeza katika Sekta ya Madini na kueleza kuwa, kwa upande wa Wizara, inafanya jitihada za kuondoa urasimu kwenye uwekezaji katika sekta husika.

“Tunataka mwekezaji mwenye nia anapoonesha dhamira ya kuwekeza baada ya taratibu zote kukamilika basi aanze mara moja,” amesema Waziri Biteko.

Akizungumza katika kikao hicho mmoja wa wawakilishi wa kampuni hiyo Balozi Mstaafu Andrew Mcalister, amesema kuwa, nchi ya Tanzania inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa madini ya Colbat kutokana na ubora wake na mazingira ya uwekezaji yaliyopo nchini ikiwemo uwazi.

Mbali na Waziri Biteko, wengine waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, na wataalam wengine wa wizara.

Waziri wa Madini Doto Biteko (kulia) akimsikiliza mwakilishi wa kampuni ya Jervois Mining Limited ya Australia   Balozi Mstaafu Andrew Mcalister (katikati). Kushoto ni Naibu Waziri Stanslaus Nyongo. Wengine ni wawakilishi wa kampuni hiyo.

Waziri wa Madini Doto Biteko akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jervois Mining Limited ya Australia Brye Croker.

Baadhi ya Wataalam wa Wizara ya Madini wakifuatilia kikao baina ya Waziri wa Madini na wawakilishi wa kampuni ya Jervois Mining Limited.

Thursday, February 14, 2019

Nyongo ataka Watumishi madini kuepuka rushwa


Na Asteria Muhozya, Dodoma

Naibu wa Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amewataka watumishi wa Wizara ya Madini kujiepusha na vitendo vya rushwa ikiwemo kuzuia rushwa katika sehemu zao za kazi kwani suala hilo linasababisha migogoro kwenye sekta ya madini.

Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo Februari 13 wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi la wizara na kuongeza kuwa, serikali inafuatilia mienendo ya watumishi wa sekta husika.

Alisema kuwa, wako watumishi wanaomiliki leseni kwa dhuluma suala ambalo pia limechangia kuwepo kwa migogoro mingi kwenye sekta na kueleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli anasisitiza suala la kuzingatia maadili katika utumishi wa umma na hususan katika sekta ya madini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo alilitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhakikisha linajiendesha kwa faida na kusisitiza kuwa Serikali inataka gawio.

Aidha, aliutaka uongozi wa STAMICO kuzingatia maslahi ya watumishi kwa kutoa motisha mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi wa shirika kwa ujumla.

Akizungumzia mafanikio makubwa katika Sekta ya Madini, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa ni pamoja na mabadiliko ya Sheria ya Madini na kusisitiza kuwa kwa Afrika Tanzania imekuwa mfano kama nchi bora inayosimamia vyema rasilimali za madini.

“Sifa bora kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini zisitufanye tubweteke bali tuendelee kufanya kazi kwa ubunifu wa hali ya juu huku tukizingatia maadili ya kazi,” alisema Nyongo

Nyongo aliendelea kusema kuwa, kama moja ya mikakati ya kutoa motisha kwa watumishi, uongozi wa Wizara unatakiwa kutoa fursa mbalimbali kwa watumishi ikiwa ni pamoja na mafunzo.

Wakati huo huo, akizungumza kwa niaba ya watumishi, Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Joyce Manyama alisema kuwa watumishi kupitia chama chao watafanya kazi bega kwa bega na uongozi wa Wizara ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na viwanda vingi vya uongezaji thamani madini ili kufikia malengo ya Serikali kupitia mchango wa Sekta ya Madini kwenye ukuaji wa Pato la Taifa.

Aidha, Manyama alichukua fursa hiyo kuishukuru Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Shirika la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Nchini (FEMATA), wachimbaji wadogo kwa kuitisha mkutano uliofanyika hivi karibuni baina yao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli

Vilevile, aliishukuru Wizara kwa kuanzisha mfumo mpya wa utunzaji wa kumbukumbu za Wizara unaojulikana kama Electronic Filing Management System ambao utaboresha utunzaji wa kumbukumbu na kurahisisha upatikanaji wake pindi zinapohitajika.

Pia, aliiomba Wizara kuendelea kusimamia zoezi la upandishwaji wa vyeo ili watumishi waweze kupandishwa vyeo kulingana na sifa wanazokuwa nazo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema kuwa Wizara itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kazi ili kila mtumishi afanye kazi kwa ubunifu zaidi.

Aliongeza kuwa, kwa sasa Wizara inafanya vizuri ambapo Sekta ya Madini imekua kwa asilimia 18 huku mchango wa sekta kwa fedha za kigeni ikiwa ya tatu nyuma ya Kilimo na Utalii na kueleza kwamba, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna rushwa na kukosekana uadilifu.


Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi lililofanyika tarehe 13 Februari, 2019. 

Naibu Waziri wa Madini Sanslaus Nyongo na Viongozi Waandamizi wa Wizara pamoja na Viongozi wa TUGHE Taifa na TUGHE Tawi la Wizara ya Madini, wakiimba wimbo Maalum wa kuhamasisha Umoja wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi. 

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo na Wawakilishi kutoka Taasisi za Wizara. 

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakifuatilia mkutano huo. 

Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Joyce Manyama akizungumza jambo wakati wa kikao hicho. 

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Madini. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Madini. 

Wednesday, February 13, 2019

Biteko ameitaka bodi ya STAMICO kuhakikisha inachangia pato la taifa kabla ya mwezi Juni, 2019


Na Nuru Mwasampeta,

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kuhakikisha kuwa sekta ya Madini kupitia shirika hilo inaongeza mchango wake kwa pato la taifa kwa kulipa mrabaha na kodi mbalimbali za serikali na kuongeza wigo wa ajira za watanzania kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi katika kuendesha shirika hilo.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za Stamico zilizopo maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 12 February, 2019.

Biteko alisema anautambua wazi umuhimu wa Bodi hiyo katika kufanya maamuzi, kupitia Sheria na sera zinazohusiana na uendeshaji wa shirika hilo na ndio maana uundwaji wa bodi hiyo ulipewa kipaumbele mara tu baada ya yeye kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Waziri wa Madini.

Ameendelea kwa kusema, uteuzi wao haukuwa rahisi na ulizingatia uwezo na uzoefu wa wajumbe katika kutekeleza majukumu ya Bodi pamoja na uzalendo walionao kwa taifa na kuwasihi kuhakikisha wanakuwa wasimamizi wazuri wa shirika hilo kwa manufaa ya Taifa.

Alisema, kigezo kikubwa kilichotumika katika uteuzi huo ni kuangalia ubunifu wa mtu mmoja mmoja, mahali anakofanyia kazi au alipofanyia kazi, “ninyi katika ofisi mlizopita mliacha mambo makubwa Imani yetu wizara ni kuwa mtatumia ubunifu huo katika kusimamia na kubadilisha taswira ya shirika letu”. Alisisitiza.

Alikiri kuwa Serikali imewaamini na kuwapa mamlaka ya kusimamia Shirika hilo tunaamini mnaweza ndio maana katika wengi mliteuliwa  ninyi.

Akibainisha majukumu ya Bodi hiyo, Biteko alisema ni pamoja na Kuisimamia Menejimenti ya Shirika katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku kwa mujibu wa Sheria.

Kusimamia sera ya Shirika na kuanzisha mifumo ya udhibiti katika utekelezaji wa Sera hizo, Kupitia na kuidhinisha miundo ya Maendeleo ya Watumishi wa Shirika, kupitia na kuidhinisha mishahara na marupurupu ya watumishi wa shirika pamoja na kuanzisha mfumo mzuri wa kutoa gawio kwa wana hisa wa Shirika.

Aidha, Biteko alilipongeza shirika kwa hatua nzuri waliyoifikia katika kutekeleza baadhi ya miradi ikiwa ni pamoja na uchimbwaji na uuzwaji wa makaa ya mawe wa Kabulo, kuanza uchenjuaji wa mabaki ya mchanga wa dhahabu katika eneo la mradi wa dhahabu wa Buhemba, kuzalisha na kuuza kokoto Ubena Zomozi, kuimarisha usimamizi wa miradi ya ubia ya TanzaniteOne na Buckreef na kampuni tanzu ya STAMIGOLD, na kuratibu shughuli za kuwaendeleza wachimbaji wadogo.

Biteko alikiri kuwa Serikali imechoshwa na kupata hasara kupitia katika shirika hilo, na kusema badala ya miradi inayoanzishwa katika shirika hilo kuzalisha faida inazalisha madeni na kuliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya pesa.

Akitoa mfano wa watu wawili waliokwenda vitani, mmoja akiwa na moyo wa vita bila silaha na mwingine akiwa na silaha bila moyo wa kupigana Biteko alisema ni dhahiri yule mwenye moyo wa vita atashinda na kuitaka bodi hiyo kuiga mfano huo katika kutekeleza majukumu yake.

Aliendelea kusisitiza kuwa Serikali anaamini wajumbe wa bodi hiyo wanao moyo wa kupigana vita bila kubeba silaha na kuwasihi kuanzia hapohapokutekeleza majukumu yake, “anzeni hivyo mlivyo, ipeni Serikali sababu ya kuishawishi serikali kuleta pesa”. Alisisitiza.

Serikali ya awamu ya tano inafanya vitu vilivyoshindikana, Vilee vitu ambavyo watu wanasema haviwezekani ndivyo vinavyofanyika nasi tunaamini mmeteuliwa ili kurekebisha madhaifu ya Stamico yaliyoshindikana kwa muda mrefu, wakurekebisha na kulifanya shirika la Stamico kuwa bora ni ninyi bodi pamoja na  menejimenti ya shirika.

Aidha, ameitaka bodi hiyo kumtafuta popote pale mtu yeyote wanayedhani anaweza kulisaidia Shirika kuzalisha faida na vile vile amewataka kumpeleka mtu yeyote mwenye cheo chochote anayelirudisha shirika hilo nyuma ili atafutiwe kazi nyingine ya kufanya.

“Haiwezekani shirika kutoka kuundwa kwake mwaka 1972 halijawahi kutoa gawio, haiwezekani lipo kwa ajili ya nini? Lakini watu wakizunguka wanalipwa posho lakini mwenye mali hapati kitu”. Biteko aling’aka.

Aidha, Biteko aliwataka wanabodi hao kubadilisha wimbo wa lawama unaosbabaishwa na shirika hilo na kuimba wimbo wa sifa, amekiri kutaka matokeo na sio stori. Alisema kwa namna anavyowafahamu wajumbe hao wa bodi wakishindwa kulibadilisha shirika hilo kwa awamu hii yeye binafsi atakuwa wa kwanza kuomba shirika hilo lifutwe.

Aliwataka wajumbe hao wa bodi kuifanya Stamico kuwa eneo la mataifa mengine kujifunzia namna bora ya kuendesha mashirika ya umma ikiwa ni pamoja na kuwaacha kufanya maamuzi yao kama shirika.

Alimuhakikishia Mwenyekiti wa bodi hiyo kuifanyia kazi changamoto ya uhaba wa wafanyakazi unaolikabili shirika mara tu baada ya kuurekebisha muundo wa uongozi wa shirika hilo aliokiri kuwa na vyeo vingi kulioko uwezo na uzalishaji wa shirika.

Aliitaka bodi hiyo kuhakikisha inabadilisha fikra na taswira ya shirika kwa kubadilisha namna ya kufikiri kwa watendaji wake ili wafikiri kibiashara zaidi na si kimishahara.

Alisisitiza kuwa anataka aibu ya Stamico ya miaka mingi iondolewe sasa na kama sio sasa basi sasa hivi, na kuwataka kutoa taarifa wakati wowote wanapoona wanakwama katika kutekeleza majukumu yao.

Aidha, Biteko aliitaka bodi hiyo kwenda kufuatilia suala la hisa za kampuni ya Tanzania Gemstone Industries Ltd (TGI) iliyosajiliwa mnamo mwaka 1969 ikiwa ni kampuni Tanzu ya Stamico na kutoliingizia faida yeyote shirika licha ya uzalishaji kufanyika na kuwa na umiliki wa hisa za kampuni ya Mundarara Mining Ltd kwa asilimia 50.

Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa wizara haitaingilia masuala ya shirika lakini jicho lake litakuwa Stamico kutokana na kwamba kushindwa kwa shirika ni kushindwa kwa wizara na kushindwa kwa wizara ni kushindwa kwa Waziri kitu ambacho hatakikubali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mej. Gen (Mstaafu) Michael Isamuyo alitoa shukrani zake kwa uteuzi uliofanywa wa kumpatia fursa ya kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo ambapo alieleza kuwa aliyeteuliwa mwezi Disemba Tarehe 6 na baadaye kuteuliwa kwa wajumbe wengine wa bodi ambao amekiri watafanya kazi kubwa kwa shirika na taifa.

Alikiri kuwa wajumbe wa bodi wametoka katika maeneo mbalimbali wakiwa na ujuzi na uzoefu tofauti tofauti ambao wakikaa pamoja katika kutekeleza majukumu watafanya kitu kikubwa na kusababisha mabadiliko makubwa kwenye Shirika kubwa la Taifa la madini.

Amekiri kuwa masuala yote waliyoagizwa watatekeleza kama walivyoelekezwa “Majukumu yetu tunayafahamu lakini haya majukumu ni muongozo tu, naamini tutatumia uwezo wetu, tutatumia akili zetu, uzoefu tulionao katika maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa tunatekeleza majukumu yetu kwa ufanisi kuhakikisha kwamba zile changamoto ambazo zipo na zitakazoendelea kujitokeza tunazigeuza kuwa fursa na tunazitatua”. Alisisitiza.

Amesema katika ameneo yote changamoto hazikosekani, lakini kufanya kazi kwa mazoea ndiko kunakorudisha nyuma mafanikio “huu mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea bila ubunifu wowote utaturudisha nyuma alisema na haya ndiyo masuala uliyotushauri” amekiri kuwa bodi yake ina utashi huo na watahakikisha kuwa wanakuwa na ubunifu wa hali ya juu na kuifanya Stamico kujikwamua kutoka mahali walipo.

Akijibu hoja ya kuwa na moyo wa vita kabla ya kupata silaha, Isamuyo alisema yapo matatizo mengi kwa shirika ikiwa ni pamoja na suala la uhaba wa mitaji pamoja na wafanyakazi, na kuiri kuwa kutokana na moyo wa vita walionano changamoto hizo zitageuzwa na kuwa fursa.

Akitolea mfano ujenzi wa nyumba zenye vioo zilivyowafanya wezi kuichukulia ujenzi huwa kama fursa kwa kuwarahisishia kuingia  ndani ndani ya nyumba bila shida lakini pia hiyo kuwa ni fursa kwa wajenzi na wafanyabiashara kuzalisha kuzalisha nondo na kujengea ili kuwapa wezi kazi ya kufanya pindi wanapotaka kuvamia majengo ya watu kwa lengo la kuwaibia. Isamuyo ameahidi kugeuza changamoto za Stamico kuwa fursa na kulipeleka shirika mbele.

Amemuhakikishia Waziri wa Madini kuwa bodi hiyo haitashindwa kazi, “Hatutashindwa kwa sababu hamkushindwa kututeua, mlikuwa na majina mengi yenye sifa zinazofanana na zetu lakini hamkushindwa kututeua na kwa sababu ninyi hamkushindwa kututeua na sisi hatutashindwa kuhakikisha kwamba tunasonga mbele katika kutekeleza majukumu ya shirika” alisisitiza .

Amekiri kwamba kabla ya kuomba silaha ya mizinga sehemu yeyote tutahakikisha kwamba silaha ndogo zitafanya kazi na kuhakikisha adui anapigwa, amesema watumishi waliopo lazima wahakikishe kuwa wanafanya kazi na kuliletea shirika faida bila kutegemea mtu kutoka eneo lingine. Alisema waajiliwa wengine wakipatikana waje kuongeza nguvu lakini si kwa sababu waliopo wameshindwa kazi.

Kuhusu Mikataba isiyokuwa na tija, Isamuyo amewataka wanasheria kuhakikisha mikataba inayoingiwa sasa hivi inazalisha faida tofauti na ilivyokuwa awali.

Kuhusu agizo la kuhakikisha shirika linatoa gawio kwa serikali, Isamuyo amesema agizo hilo limetolewa kwa mwanajeshi, hilo ni agizo na litatekelezwa vizuri sana na kuahidi kufuatilia suala la kushughulikia hisa za kampuni ya Tanzania Gemstone Industries Ltd(TGI) ambayo ni kampni tanzu ya Stamico itashughulikiwa ipasavyo.

Ameiomba serikali kushughulikia changamoto za msingi na masuala mengine yanayopaswa kutatuliwa na wizara kufanyiwa maamuzi mapema ikiwa ni pamoja na suala la ajira mpya na kukiri kuwa shirika ni la kibiashara hivyo kila dakika inayopotea inazalisha hasara kwa shirika.

Uzinduzi wa Bodi hiyo ulishirikisha viongozi wote waandamizi wa wizara ikiwa ni pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliyewataka Bodi hiyo kwenda kufanya kazi na kuithibitisha Imani ya serikali kwao, Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Issa Nchasi.


Waziri wa Madini, Doto Biteko akitoa maelekezo kwa mwenyekiti wa Bodi ya Stamico na Menejimenti ya shirika wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shirika hilo. 



Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini a Taifa, Kanali Sylvester Ghuliku Akizungumza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo jijini Dodoma. 


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa, Mej. Gen (Mstaafu) Michael Isamuyo akizugumza jambo mara baada ya Waziri wa Madini Doto Biteko kuzindua rasmi bodi hiyo na kuipa meno kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Shirika.

Waziri wa Madini, Doto Biteko (Kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Stamico  Mej. Gen (Mstaafu) ichael Isamuyo nyenzo ikiwa ni mwongozo katika kutekeleza majukumu ya bodi kwa shirika hilo.

Monday, February 11, 2019

Mlolongo wa kodi sekta ya madini kuondolewa-Biteko


Na Samwel Mtuwa, Mwanza

Mchakato wa kuondoa Mlolongo wa Kodi na Tozo kwa wachimbaji Wadogo wa Madini upo katika hatua za mwisho na ndani ya muda mfupi ujao, baadhi ya kodi na tozo hizo zitafutwa katika Sekta ya Madini.

Hayo yamesemwa Februari 11, 2019 na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akifungua Warsha kuhusu namna ya kuanzisha masoko ya madini nchini inayofanyika Jijini Mwanza.

Warsha hiyo inayolenga katika kutoa elimu ya namna ya kuanzisha masoko ya madini imeanza leo na itafanyika kwa siku mbili hadi Februari 12, 2019 ikiwashirikisha Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo.

Waziri Doto ameeleza, warsha hiyo ni muhimu kwa wizara  nan  nchi kwa ujuml kutokana na  lengo ililojiwekea wizara hivi sasa ya kuhakikisha mchango wa sekta ya madini kwenye Uchumi na maisha ya wananchi unaongezeka.

Ameongeza kuwa, ana imani kwamba kwa kuondoa baadhi ya tozo na kodi kwa wachimbaji wadogo zitawezesha kuziba mianya ya utoroshaji wa madini na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye pato la taifa.

Waziri Biteko amefafanua kuwa, Mchakato wa kuandaa Kanuni za Masoko ya madini umezingatia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujifunza kutoka nchi zenye masoko ya madini.

Ameeleza kuwa, Halmashauri zinaowajibu wa kuendelea kuwajenga, kuwalea, na kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa sababu mazao yao ndio yanayotegemewa kuuzwa katika masoko hayo.

Ametaka njia pekee ya kujibu na kutolea ufanunuzi wa taarifa potofu ni kutumia maelekezo yaliyopo katika sheria ya Madini ya 2010 na Marekebisho yake ya 2017.

“Pamoja na changamoto zilizopo kwenye usimamizi wa  sekta ya Madini nchini namshukuru Mungu kwani rasilimali hizi hazijageuka kuwa balaa,” amesema Biteko.

Katika hatua nyingne, amesema kuwa, Maafisa madini watakaokuwa kikwazo katika uanzishwaji wa masoko ya madini watachukuliwa hatua za kisheria.

Wadau katika warsha hiyo ni kutoka Mikoa ya Mwanza Dodoma, Arusha, Geita, Shinyanga, Mara, Manyara, Kagera, Tabora, Singida, Mbeya, Morogoro,na Ruvuma.

Warsha hiyo imeandaliwa na wizara ya Madini kwa ushirikiano na Taasisi ya Uongozi.


Waziri wa Madini Doto Biteko katika picha ya pamoja na wadau wanaoshiriki Warsha ya kuanzisha masoko ya Madini Nchini. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akiteta jambo na baadhi ya Watendaji Waandamizi wa Wizara na Wadau wa warsha hiyo, mara baada ya kuifungua. 

Waziri wa Madini Doto Biteko katika picha ya pamoja na wadau wanaoshiriki Warsha ya kuanzisha masoko ya Madini Nchini.

Friday, February 8, 2019

Naibu Waziri Nyongo afungua warsha kujadili mpango ufungaji migodi


Na Nuru Mwasampeta, Dodoma

Kufuatia kutokuwepo kwa mwongozo wa ufungaji wa migodi pindi shughuli za uchimbaji zinapofikia kikomo, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeandaa rasimu ya mwongozo ambayo inajadiliwa na wadau kutoka Taasisi za Kiserikali na wadau mbalimbali wa madini zikiwemo makampuni za uchimbaji kutoka Chamber of Mine.

Akifungua warsha ya kujadili rasimu hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amewataka washiriki na waalikwa wote kufanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa ili kuuboresha mwongozo huo.

Amesema, mwongozo huo utawasaidia wawekezaji watakaokuwa na nia ya kuwekeza nchini kujua taratibu na namna wanavyopaswa kufanya pindi wanapoandaa mpango wao wa kufunga mgodi ambao kwa mujibu wa taratibu, unapaswa kuwasilishwa serikalini kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji nchini.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 206 ya Sheria ya Madini ya 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2107, kila mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini wa kati na mkubwa anatakiwa kuandaa mpango wa ufungaji migodi na kuwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa leseni ambaye ataandaa mkutano wa kamati ya kitaifa ya ufungaji migodi ambayo hupitia, kuujadili na kupitisha mpango huo.

Naibu Waziri Nyongo ameongeza kuwa, Mpango huo wa ufungaji wa migodi unaeleza kwa kina namna migodi itakavyofungwa na kurudisha eneo katika hali inayoweza kufaa kwa matumizi mengine.

Aidha, amesema kuwa, mipango hiyo huelezea namna wamiliki wa migodi watakavyowawezesha wafanyakazi pamoja na jamii inayozunguka eneo la migodi waliokuwa wakifanya kazi katika migodi hiyo pindi migodi hiyo inapofungwa.

Amesema mwongozo huo utaweka wazi namna bora ya kuandaa mpango wa kufunga mgodi pamoja na kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Madini na Sheria nyingine zinavyoelekeza.

Naibu Waziri, Nyongo amesema anatarajia mpango huo uendane na mazingira ya Tanzania na mwongozo ikiwemo kuhakikisha kuwa unajali vizazi na vizazi vitakavyofuata baada ya madini kuisha na kusema “Lazima tujue kwamba kuna vizazi vitakavyokuja baadaye, madini tunayo ni rasilimali yetu, lakini lazima tujue kuna vizazi vingine vinakuja,”

Ameongeza kuwa, uchimbaji unaendana na uharibifu wa mazingira, lakini ni lazima kuwaza namna ambavyo vizazi vinavyokuja vitakavyoishi.

Amebainisha kuwa, hatua hiyo ni muhimu ambayo kama taifa linategemea kikao hicho kiwe na manufaa kwa taifa la leo na vizazi vijavyo.

Akizungumza na washiriki wa warsha hiyo inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ufundi (Veta) kwa siku mbili, Nyongo ameupongeza uongozi wa Tume ya Madini kwa hatua nzuri waliyoifikia katika kuandaa mwongozo huo.

Aidha, nyongo amesema Tume ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Madini kupitia mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP), iliandaa rasimu ya kwanza ya mwongozo wa huo ambao unajadiliwa na wajumbe hao ili wamekutana ili kupata mwongozo unaokubalika kwa taifa.

Aidha, Nyongo ameeleza kuwa, maoni yaliyotolewa na wadau kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati wa Mkutano wa kisekta uliofanyika mwezi Januari, yanafanyiwa kazi na hivyo kuahidi kuwa wadau wa madini na taifa watapata mrejesho wa kile kilichowasilishwa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini, Dkt. Abdurahman Mwanga amesema katika nchi mbalimbali duniani suala la ufungaji wa migodi limekuwa ni gumu, hivyo, mwongozo unaoandaliwa utaonesha nini hasa kinapaswa kufanyika mara baada ya mgodi kufungwa.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Neoroika, Honest Mrema, ulioko katika mkoa wa Songwe unaomilikiwa na Shanta mining, amesema rasimu hiyo ni nzuri na imetoa nafasi nzuri kwa wadau kukaa meza moja na watendaji wa serikali kujadili changamoto zinazowakabili kuhakikisha wanapochimba wanapata kile wanachotarajia.

Aidha, amebainisha kuwa, madini ni rasilimali, na pindi yanapochimbwa kuna uharibifu unatokea hivyo katika uharibifu kurudisha mazingira katika hali yake ya kawaida ni kuifanyia ardhi hivyo masuala muhimu.

Akielezea umuhimu wa maandalizi ya mwongozo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini (TAWOMA), Eunice Negele, amesema rasimu inayojadiliwa itaisaidia jamii pamoja na vizazi vijavyo kwa kuwa, itawafanya wawekezaji kuhakikisha wanaiacha ardhi yenye kufaa kwa matumizi mengine tofauti na uchimbaji.


Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dr. Abdurahman Mwanga akiwasilisha rasimu ya ufungaji wa migodi kwa wadau waliojumuika kwa lengo la kuiboresha. 

Kamishna Msaidizi wa migodi na Maendeleo ya Madini Ali S. Ali akijitambulisha kabla ya ufunguzi wa warsha ya maandalizi ya mwongozo wa ufungaji wa migodi unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma. 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa kwanza kushoto) akifuatana na Katibu Mtendaji wa Tume ya madini, Prof. Shukrani Manya na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dr. Abdurahman Mwanga wakati wa ufunguzi wa warsha ya kuandaa mwongozo wa ufungaji wa migodi inayofanyika katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma. 

Wadau mbalimbali wa madini walioshiriki katika warsha ya maandalizi ya mwongozo wa ufungaji wa migodi unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma wakimsikiliza Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dr. Abdurahman Mwanga akiwasilisha rasimu hiyo tayari kwa majadiliano. 

Wadau mbalimbali wa madini walioshiriki katika warsha ya kujadili rasimu ya mwongozo wa ufungaji wa migodi inayofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma.