Na Asteria Muhozya, Dodoma
Naibu wa Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo
amewataka watumishi wa Wizara ya Madini kujiepusha na vitendo vya rushwa
ikiwemo kuzuia rushwa katika sehemu zao za kazi kwani suala hilo linasababisha
migogoro kwenye sekta ya madini.
Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo Februari 13
wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi la wizara na kuongeza kuwa,
serikali inafuatilia mienendo ya watumishi wa sekta husika.
Alisema kuwa, wako watumishi wanaomiliki leseni
kwa dhuluma suala ambalo pia limechangia kuwepo kwa migogoro mingi kwenye sekta
na kueleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli
anasisitiza suala la kuzingatia maadili katika utumishi wa umma na hususan
katika sekta ya madini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo alilitaka
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhakikisha linajiendesha kwa faida na
kusisitiza kuwa Serikali inataka gawio.
Aidha, aliutaka uongozi wa STAMICO kuzingatia maslahi
ya watumishi kwa kutoa motisha mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo
lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi wa shirika kwa ujumla.
Akizungumzia mafanikio makubwa katika Sekta ya
Madini, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa ni pamoja na mabadiliko ya Sheria ya
Madini na kusisitiza kuwa kwa Afrika Tanzania imekuwa mfano kama nchi bora
inayosimamia vyema rasilimali za madini.
“Sifa bora kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini
zisitufanye tubweteke bali tuendelee kufanya kazi kwa ubunifu wa hali ya juu
huku tukizingatia maadili ya kazi,” alisema Nyongo
Nyongo aliendelea kusema kuwa, kama moja ya
mikakati ya kutoa motisha kwa watumishi, uongozi wa Wizara unatakiwa kutoa
fursa mbalimbali kwa watumishi ikiwa ni pamoja na mafunzo.
Wakati huo huo, akizungumza kwa niaba ya watumishi,
Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Tawi la Wizara
ya Madini, Joyce Manyama alisema kuwa watumishi kupitia chama chao watafanya
kazi bega kwa bega na uongozi wa Wizara ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini
inakuwa na viwanda vingi vya uongezaji thamani madini ili kufikia malengo ya Serikali
kupitia mchango wa Sekta ya Madini kwenye ukuaji wa Pato la Taifa.
Aidha, Manyama alichukua fursa hiyo kuishukuru
Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Shirika la Vyama vya Wachimbaji wa Madini
Nchini (FEMATA), wachimbaji wadogo kwa kuitisha mkutano uliofanyika hivi
karibuni baina yao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Magufuli
Vilevile, aliishukuru Wizara kwa kuanzisha mfumo
mpya wa utunzaji wa kumbukumbu za Wizara unaojulikana kama Electronic Filing Management System ambao utaboresha utunzaji wa
kumbukumbu na kurahisisha upatikanaji wake pindi zinapohitajika.
Pia, aliiomba Wizara kuendelea kusimamia zoezi la
upandishwaji wa vyeo ili watumishi waweze kupandishwa vyeo kulingana na sifa
wanazokuwa nazo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila alisema kuwa Wizara itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kazi
ili kila mtumishi afanye kazi kwa ubunifu zaidi.
Aliongeza kuwa, kwa sasa Wizara inafanya vizuri
ambapo Sekta ya Madini imekua kwa asilimia 18 huku mchango wa sekta kwa fedha
za kigeni ikiwa ya tatu nyuma ya Kilimo na Utalii na kueleza kwamba, pamoja na
mafanikio hayo, bado kuna rushwa na kukosekana uadilifu.
![]() |
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo
akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi
lililofanyika tarehe 13 Februari, 2019.
![]() |
Naibu Waziri wa Madini Sanslaus Nyongo na Viongozi
Waandamizi wa Wizara pamoja na Viongozi wa TUGHE Taifa na TUGHE Tawi la Wizara
ya Madini, wakiimba wimbo Maalum wa kuhamasisha Umoja wakati wa mkutano wa
Baraza la Wafanyakazi.
![]() |
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akiwa
katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo na Wawakilishi kutoka
Taasisi za Wizara.
![]() |
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi
wakifuatilia mkutano huo.
![]() |
Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na
Afya (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Joyce Manyama akizungumza jambo wakati
wa kikao hicho.
![]() |
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo katika
picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Madini.
![]() |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon
Msanjila akizungumza jambo wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara
ya Madini.
No comments:
Post a Comment