Na
Nuru Mwasampeta, Dodoma
Kufuatia kutokuwepo
kwa mwongozo wa ufungaji wa migodi pindi shughuli za uchimbaji zinapofikia
kikomo, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeandaa rasimu ya mwongozo ambayo
inajadiliwa na wadau kutoka Taasisi za Kiserikali na wadau mbalimbali wa madini
zikiwemo makampuni za uchimbaji kutoka Chamber
of Mine.
Akifungua warsha ya
kujadili rasimu hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amewataka
washiriki na waalikwa wote kufanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa ili kuuboresha
mwongozo huo.
Amesema, mwongozo huo
utawasaidia wawekezaji watakaokuwa na nia ya kuwekeza nchini kujua taratibu na
namna wanavyopaswa kufanya pindi wanapoandaa mpango wao wa kufunga mgodi ambao
kwa mujibu wa taratibu, unapaswa kuwasilishwa serikalini kabla ya kuanza shughuli
za uchimbaji nchini.
Kwa mujibu wa Kanuni
ya 206 ya Sheria ya Madini ya 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2107, kila
mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini wa kati na mkubwa anatakiwa kuandaa
mpango wa ufungaji migodi na kuwasilisha kwa Mkaguzi Mkuu wa leseni ambaye
ataandaa mkutano wa kamati ya kitaifa ya ufungaji migodi ambayo hupitia, kuujadili
na kupitisha mpango huo.
Naibu Waziri Nyongo ameongeza
kuwa, Mpango huo wa ufungaji wa migodi unaeleza kwa kina namna migodi
itakavyofungwa na kurudisha eneo katika hali inayoweza kufaa kwa matumizi
mengine.
Aidha, amesema kuwa,
mipango hiyo huelezea namna wamiliki wa migodi watakavyowawezesha wafanyakazi
pamoja na jamii inayozunguka eneo la migodi waliokuwa wakifanya kazi katika
migodi hiyo pindi migodi hiyo inapofungwa.
Amesema mwongozo huo utaweka
wazi namna bora ya kuandaa mpango wa kufunga mgodi pamoja na kuhifadhi
mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Madini na Sheria nyingine zinavyoelekeza.
Naibu Waziri, Nyongo
amesema anatarajia mpango huo uendane na mazingira ya Tanzania na mwongozo
ikiwemo kuhakikisha kuwa unajali vizazi na vizazi vitakavyofuata baada ya
madini kuisha na kusema “Lazima tujue kwamba kuna vizazi vitakavyokuja baadaye,
madini tunayo ni rasilimali yetu, lakini lazima tujue kuna vizazi vingine
vinakuja,”
Ameongeza kuwa, uchimbaji
unaendana na uharibifu wa mazingira, lakini ni lazima kuwaza namna ambavyo vizazi
vinavyokuja vitakavyoishi.
Amebainisha kuwa,
hatua hiyo ni muhimu ambayo kama taifa linategemea kikao hicho kiwe na manufaa
kwa taifa la leo na vizazi vijavyo.
Akizungumza na
washiriki wa warsha hiyo inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha
Ufundi (Veta) kwa siku mbili, Nyongo ameupongeza uongozi wa Tume ya Madini kwa
hatua nzuri waliyoifikia katika kuandaa mwongozo huo.
Aidha, nyongo amesema
Tume ya Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Madini kupitia mradi wa Usimamizi
Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP), iliandaa rasimu ya kwanza ya mwongozo wa
huo ambao unajadiliwa na wajumbe hao ili wamekutana ili kupata mwongozo
unaokubalika kwa taifa.
Aidha, Nyongo
ameeleza kuwa, maoni yaliyotolewa na wadau kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Magufuli wakati wa Mkutano wa kisekta uliofanyika mwezi Januari,
yanafanyiwa kazi na hivyo kuahidi kuwa wadau wa madini na taifa watapata
mrejesho wa kile kilichowasilishwa.
Akizungumza na
waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa
Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini, Dkt. Abdurahman Mwanga amesema katika
nchi mbalimbali duniani suala la ufungaji wa migodi limekuwa ni gumu, hivyo,
mwongozo unaoandaliwa utaonesha nini hasa kinapaswa kufanyika mara baada ya
mgodi kufungwa.
Kwa upande wake, Meneja
Mkuu wa Mgodi wa Neoroika, Honest Mrema, ulioko katika mkoa wa Songwe
unaomilikiwa na Shanta mining, amesema rasimu hiyo ni nzuri na imetoa nafasi
nzuri kwa wadau kukaa meza moja na watendaji wa serikali kujadili changamoto
zinazowakabili kuhakikisha wanapochimba wanapata kile wanachotarajia.
Aidha, amebainisha
kuwa, madini ni rasilimali, na pindi yanapochimbwa kuna uharibifu unatokea
hivyo katika uharibifu kurudisha mazingira katika hali yake ya kawaida ni
kuifanyia ardhi hivyo masuala muhimu.
Akielezea umuhimu wa
maandalizi ya mwongozo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini
(TAWOMA), Eunice Negele, amesema rasimu inayojadiliwa itaisaidia jamii pamoja
na vizazi vijavyo kwa kuwa, itawafanya wawekezaji kuhakikisha wanaiacha ardhi
yenye kufaa kwa matumizi mengine tofauti na uchimbaji.
Mkurugenzi wa Ukaguzi
wa Migodi na Mazingira, Dr. Abdurahman Mwanga akiwasilisha rasimu ya ufungaji
wa migodi kwa wadau waliojumuika kwa lengo la kuiboresha.
Kamishna Msaidizi wa
migodi na Maendeleo ya Madini Ali S. Ali akijitambulisha kabla ya ufunguzi wa
warsha ya maandalizi ya mwongozo wa ufungaji wa migodi unaofanyika kwa siku
mbili katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (wa kwanza kushoto) akifuatana na Katibu Mtendaji wa
Tume ya madini, Prof. Shukrani Manya na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na
Mazingira, Dr. Abdurahman Mwanga wakati wa ufunguzi wa warsha ya kuandaa
mwongozo wa ufungaji wa migodi inayofanyika katika ukumbi wa VETA jijini
Dodoma.
Wadau mbalimbali wa
madini walioshiriki katika warsha ya maandalizi ya mwongozo wa ufungaji wa
migodi unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma
wakimsikiliza Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dr. Abdurahman
Mwanga akiwasilisha rasimu hiyo tayari kwa majadiliano.
Wadau mbalimbali wa
madini walioshiriki katika warsha ya kujadili rasimu ya mwongozo wa ufungaji wa
migodi inayofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment