Na
Nuru Mwasampeta,
Waziri wa Madini,
Doto Biteko ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico)
kuhakikisha kuwa sekta ya Madini kupitia shirika hilo inaongeza mchango wake
kwa pato la taifa kwa kulipa mrabaha na kodi mbalimbali za serikali na kuongeza
wigo wa ajira za watanzania kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi katika
kuendesha shirika hilo.
Ameyasema hayo wakati
wa ufunguzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo uliofanyika katika ukumbi wa
ofisi za Stamico zilizopo maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 12
February, 2019.
Biteko alisema
anautambua wazi umuhimu wa Bodi hiyo katika kufanya maamuzi, kupitia Sheria na
sera zinazohusiana na uendeshaji wa shirika hilo na ndio maana uundwaji wa bodi
hiyo ulipewa kipaumbele mara tu baada ya yeye kuteuliwa kushika wadhifa huo wa
Waziri wa Madini.
Ameendelea kwa
kusema, uteuzi wao haukuwa rahisi na ulizingatia uwezo na uzoefu wa wajumbe katika
kutekeleza majukumu ya Bodi pamoja na uzalendo walionao kwa taifa na kuwasihi
kuhakikisha wanakuwa wasimamizi wazuri wa shirika hilo kwa manufaa ya Taifa.
Alisema, kigezo
kikubwa kilichotumika katika uteuzi huo ni kuangalia ubunifu wa mtu mmoja
mmoja, mahali anakofanyia kazi au alipofanyia kazi, “ninyi katika ofisi
mlizopita mliacha mambo makubwa Imani yetu wizara ni kuwa mtatumia ubunifu huo
katika kusimamia na kubadilisha taswira ya shirika letu”. Alisisitiza.
Alikiri kuwa Serikali
imewaamini na kuwapa mamlaka ya kusimamia Shirika hilo tunaamini mnaweza ndio
maana katika wengi mliteuliwa ninyi.
Akibainisha majukumu
ya Bodi hiyo, Biteko alisema ni pamoja na Kuisimamia Menejimenti ya Shirika
katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku kwa mujibu wa Sheria.
Kusimamia sera ya
Shirika na kuanzisha mifumo ya udhibiti katika utekelezaji wa Sera hizo,
Kupitia na kuidhinisha miundo ya Maendeleo ya Watumishi wa Shirika, kupitia na
kuidhinisha mishahara na marupurupu ya watumishi wa shirika pamoja na kuanzisha
mfumo mzuri wa kutoa gawio kwa wana hisa wa Shirika.
Aidha, Biteko
alilipongeza shirika kwa hatua nzuri waliyoifikia katika kutekeleza baadhi ya
miradi ikiwa ni pamoja na uchimbwaji na uuzwaji wa makaa ya mawe wa Kabulo,
kuanza uchenjuaji wa mabaki ya mchanga wa dhahabu katika eneo la mradi wa
dhahabu wa Buhemba, kuzalisha na kuuza kokoto Ubena Zomozi, kuimarisha
usimamizi wa miradi ya ubia ya TanzaniteOne na Buckreef na kampuni tanzu ya
STAMIGOLD, na kuratibu shughuli za kuwaendeleza wachimbaji wadogo.
Biteko alikiri kuwa Serikali
imechoshwa na kupata hasara kupitia katika shirika hilo, na kusema badala ya
miradi inayoanzishwa katika shirika hilo kuzalisha faida inazalisha madeni na
kuliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya pesa.
Akitoa mfano wa watu
wawili waliokwenda vitani, mmoja akiwa na moyo wa vita bila silaha na mwingine
akiwa na silaha bila moyo wa kupigana Biteko alisema ni dhahiri yule mwenye
moyo wa vita atashinda na kuitaka bodi hiyo kuiga mfano huo katika kutekeleza
majukumu yake.
Aliendelea kusisitiza
kuwa Serikali anaamini wajumbe wa bodi hiyo wanao moyo wa kupigana vita bila
kubeba silaha na kuwasihi kuanzia hapohapokutekeleza majukumu yake, “anzeni
hivyo mlivyo, ipeni Serikali sababu ya kuishawishi serikali kuleta pesa”.
Alisisitiza.
Serikali ya awamu ya
tano inafanya vitu vilivyoshindikana, Vilee vitu ambavyo watu wanasema
haviwezekani ndivyo vinavyofanyika nasi tunaamini mmeteuliwa ili kurekebisha
madhaifu ya Stamico yaliyoshindikana kwa muda mrefu, wakurekebisha na kulifanya
shirika la Stamico kuwa bora ni ninyi bodi pamoja na menejimenti ya shirika.
Aidha, ameitaka bodi
hiyo kumtafuta popote pale mtu yeyote wanayedhani anaweza kulisaidia Shirika
kuzalisha faida na vile vile amewataka kumpeleka mtu yeyote mwenye cheo
chochote anayelirudisha shirika hilo nyuma ili atafutiwe kazi nyingine ya
kufanya.
“Haiwezekani shirika
kutoka kuundwa kwake mwaka 1972 halijawahi kutoa gawio, haiwezekani lipo kwa
ajili ya nini? Lakini watu wakizunguka wanalipwa posho lakini mwenye mali
hapati kitu”. Biteko aling’aka.
Aidha, Biteko
aliwataka wanabodi hao kubadilisha wimbo wa lawama unaosbabaishwa na shirika
hilo na kuimba wimbo wa sifa, amekiri kutaka matokeo na sio stori. Alisema kwa
namna anavyowafahamu wajumbe hao wa bodi wakishindwa kulibadilisha shirika hilo
kwa awamu hii yeye binafsi atakuwa wa kwanza kuomba shirika hilo lifutwe.
Aliwataka wajumbe hao
wa bodi kuifanya Stamico kuwa eneo la mataifa mengine kujifunzia namna bora ya
kuendesha mashirika ya umma ikiwa ni pamoja na kuwaacha kufanya maamuzi yao
kama shirika.
Alimuhakikishia Mwenyekiti
wa bodi hiyo kuifanyia kazi changamoto ya uhaba wa wafanyakazi unaolikabili
shirika mara tu baada ya kuurekebisha muundo wa uongozi wa shirika hilo
aliokiri kuwa na vyeo vingi kulioko uwezo na uzalishaji wa shirika.
Aliitaka bodi hiyo
kuhakikisha inabadilisha fikra na taswira ya shirika kwa kubadilisha namna ya
kufikiri kwa watendaji wake ili wafikiri kibiashara zaidi na si kimishahara.
Alisisitiza kuwa
anataka aibu ya Stamico ya miaka mingi iondolewe sasa na kama sio sasa basi
sasa hivi, na kuwataka kutoa taarifa wakati wowote wanapoona wanakwama katika
kutekeleza majukumu yao.
Aidha, Biteko
aliitaka bodi hiyo kwenda kufuatilia suala la hisa za kampuni ya Tanzania
Gemstone Industries Ltd (TGI) iliyosajiliwa mnamo mwaka 1969 ikiwa ni kampuni
Tanzu ya Stamico na kutoliingizia faida yeyote shirika licha ya uzalishaji
kufanyika na kuwa na umiliki wa hisa za kampuni ya Mundarara Mining Ltd kwa
asilimia 50.
Alihitimisha kwa
kusisitiza kuwa wizara haitaingilia masuala ya shirika lakini jicho lake
litakuwa Stamico kutokana na kwamba kushindwa kwa shirika ni kushindwa kwa
wizara na kushindwa kwa wizara ni kushindwa kwa Waziri kitu ambacho
hatakikubali.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mej. Gen (Mstaafu) Michael Isamuyo alitoa shukrani
zake kwa uteuzi uliofanywa wa kumpatia fursa ya kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo
ambapo alieleza kuwa aliyeteuliwa mwezi Disemba Tarehe 6 na baadaye kuteuliwa kwa
wajumbe wengine wa bodi ambao amekiri watafanya kazi kubwa kwa shirika na
taifa.
Alikiri kuwa wajumbe
wa bodi wametoka katika maeneo mbalimbali wakiwa na ujuzi na uzoefu tofauti
tofauti ambao wakikaa pamoja katika kutekeleza majukumu watafanya kitu kikubwa
na kusababisha mabadiliko makubwa kwenye Shirika kubwa la Taifa la madini.
Amekiri kuwa masuala
yote waliyoagizwa watatekeleza kama walivyoelekezwa “Majukumu yetu tunayafahamu
lakini haya majukumu ni muongozo tu, naamini tutatumia uwezo wetu, tutatumia
akili zetu, uzoefu tulionao katika maeneo mbalimbali kuhakikisha kuwa
tunatekeleza majukumu yetu kwa ufanisi kuhakikisha kwamba zile changamoto
ambazo zipo na zitakazoendelea kujitokeza tunazigeuza kuwa fursa na tunazitatua”.
Alisisitiza.
Amesema katika ameneo
yote changamoto hazikosekani, lakini kufanya kazi kwa mazoea ndiko
kunakorudisha nyuma mafanikio “huu mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea bila ubunifu
wowote utaturudisha nyuma alisema na haya ndiyo masuala uliyotushauri” amekiri
kuwa bodi yake ina utashi huo na watahakikisha kuwa wanakuwa na ubunifu wa hali
ya juu na kuifanya Stamico kujikwamua kutoka mahali walipo.
Akijibu hoja ya kuwa
na moyo wa vita kabla ya kupata silaha, Isamuyo alisema yapo matatizo mengi kwa
shirika ikiwa ni pamoja na suala la uhaba wa mitaji pamoja na wafanyakazi, na
kuiri kuwa kutokana na moyo wa vita walionano changamoto hizo zitageuzwa na
kuwa fursa.
Akitolea mfano ujenzi
wa nyumba zenye vioo zilivyowafanya wezi kuichukulia ujenzi huwa kama fursa kwa
kuwarahisishia kuingia ndani ndani ya
nyumba bila shida lakini pia hiyo kuwa ni fursa kwa wajenzi na wafanyabiashara
kuzalisha kuzalisha nondo na kujengea ili kuwapa wezi kazi ya kufanya pindi
wanapotaka kuvamia majengo ya watu kwa lengo la kuwaibia. Isamuyo ameahidi kugeuza
changamoto za Stamico kuwa fursa na kulipeleka shirika mbele.
Amemuhakikishia
Waziri wa Madini kuwa bodi hiyo haitashindwa kazi, “Hatutashindwa kwa sababu
hamkushindwa kututeua, mlikuwa na majina mengi yenye sifa zinazofanana na zetu
lakini hamkushindwa kututeua na kwa sababu ninyi hamkushindwa kututeua na sisi
hatutashindwa kuhakikisha kwamba tunasonga mbele katika kutekeleza majukumu ya
shirika” alisisitiza .
Amekiri kwamba kabla
ya kuomba silaha ya mizinga sehemu yeyote tutahakikisha kwamba silaha ndogo
zitafanya kazi na kuhakikisha adui anapigwa, amesema watumishi waliopo lazima
wahakikishe kuwa wanafanya kazi na kuliletea shirika faida bila kutegemea mtu
kutoka eneo lingine. Alisema waajiliwa wengine wakipatikana waje kuongeza nguvu
lakini si kwa sababu waliopo wameshindwa kazi.
Kuhusu Mikataba
isiyokuwa na tija, Isamuyo amewataka wanasheria kuhakikisha mikataba
inayoingiwa sasa hivi inazalisha faida tofauti na ilivyokuwa awali.
Kuhusu agizo la
kuhakikisha shirika linatoa gawio kwa serikali, Isamuyo amesema agizo hilo
limetolewa kwa mwanajeshi, hilo ni agizo na litatekelezwa vizuri sana na
kuahidi kufuatilia suala la kushughulikia hisa za kampuni ya Tanzania Gemstone
Industries Ltd(TGI) ambayo ni kampni tanzu ya Stamico itashughulikiwa ipasavyo.
Ameiomba serikali
kushughulikia changamoto za msingi na masuala mengine yanayopaswa kutatuliwa na
wizara kufanyiwa maamuzi mapema ikiwa ni pamoja na suala la ajira mpya na
kukiri kuwa shirika ni la kibiashara hivyo kila dakika inayopotea inazalisha
hasara kwa shirika.
Uzinduzi wa Bodi hiyo
ulishirikisha viongozi wote waandamizi wa wizara ikiwa ni pamoja na Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliyewataka Bodi hiyo kwenda kufanya kazi na
kuithibitisha Imani ya serikali kwao, Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Simon
Msanjila pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Issa Nchasi.
Waziri wa Madini,
Doto Biteko akitoa maelekezo kwa mwenyekiti wa Bodi ya Stamico na Menejimenti
ya shirika wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa shirika hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa
Shirika la Madini a Taifa, Kanali Sylvester Ghuliku Akizungumza jambo wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment