Thursday, March 14, 2019

Kamati ya Bunge yaipongeza Wizara ya Madini


Na Issa Mtuwa, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Madini kwa utekelezaji wa Ujenzi wa Jengo la Taaluma la chuo cha Madini Dodoma (MRI) na Ujenzi wa Jengo la Ofisi za Wizara ya Madini lilipo eneo la Mji wa Serikali Ihumwa, Jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa  Machi 13, 2019 na Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa kikao cha majumuhisho kilichofanyika kwenye jengo la wizara ya Madini Ihumwa, mara baada ya kukagua majengo yote mawili na kupewa taarifa ya ujenzi wake.

Wakiwa kwenye jengo la taaluma la chuo cha madini, wajumbe wamepongeza na kuridhishwa na  hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kupongeza SUMA JKT  kujenge jengo hilo.

Jengo la Taaluma ni la ghorofa tatu lenye ofisi, vyumba vya kufundishia na ukumbi wa mikutano. Ujenzi huo utagharimu jumla ya shilingi 2, 863, 161, 369.00 hadi kukamilika kwake  na unatekelezwa chini ya chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Raslimali Madini (SMMRP) kwa mkopo kutoka Benki ya  Dunia. 

Akizungumzia ujenzi wa jengo la Wizara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amewaeleza wajumbe wa kamati kuwa, ujenzi huo ulianza tarehe 4/12/2018 na ulitakiwa kukamilika tarehe 31/01/2019, hata hivyo mkandarasi hakuweza kukamilisha ndani ya muda huo kutokana na sababu mbalimbali. Prof. Msanjila ameongeza kuwa, kwa kuzingatia ushauri wa msimamizi wa ujenzi huo, walifikia makubaliano ya kumuongezea muda mkandarasi hadi kufikia tarehe 28/02/2019.

Prof. Msanjila ameongeza kuwa, mpaka sasa ujenzi huo umefikia asilimia 80 na mwezi ujao wizara itakuwa tayari kuhamia. Amesema ujenzi huo umegharimu Jumla ya shilingi Milioni 975,360,028.10 zitatumika katika ujenzi huo.

Naye, Waziri wa Madini Doto Biteko ameiambia kamati kuwa, mkandarasi wa ujenzi huo, alipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha ujenzi wake ili wafanyakazi wa Wizara hiyo waanze kulitumia. Waziri emeleza kuwa wizara inaridhishwa na kasi ya mkandarasi katika ujenzi huo.

Biteko ameongeza kuwa, wizara imedhamiria kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kuthibitisha hilo wizara imemteuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Raslimaliwatu, Nsajigwa Kabigi ambae yupo muda wote wote eneo la ujenzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dunstan Kitandula amesema pamoja na wabunge kuipongeza wizara kwa kazi nzuri, ameishauri wizara na mkandarasi wa ujenzi huo, Mzinga Holdings Company kujielekeza kwenye manunuzi ya vifaa vinavyopatikana hapa nchini.

Wakichangia wajumbe wa kamati hiyo, Joseph Musukuma na Ally Keissy wakichangia wakati wa majumuhisho waliipongeza wizara na mkandarasi, hata hivyo, walishangaa muda waliopewa na hatua iliyofikia, msukuma alisema ni kazi ya kupongeza na  wameeleza pamoja na mkandarasi kutokamilisha kazi yake kwa wakati bado utendaji wake wa kazi unaridhisha na kasi  yake inaonekana.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo aliwaambia wajumbe wa kamati kuwa, ujenzi wa jengo hilo la wizara unafanana ramani na wizara nyingine ikiwemo kiasi cha fedha zilizotolewa na serikali zote zikiwa na kiwango cha shilingi Bilioni moja.

Amesema muda uliotolewa ulilenga kutimiza azma ya wizara kuhamia eneo hilo kwa wakati. Aliwashukuru wajumbe kwa ushauri wao na kueleza kwamba kama wizara watauzingatia.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa na viongozi wa juu wa wizara ya madini wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya jingo la Wizara Ihumwa Dodoma.  
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Danstan Kitandula wa kwanza kushoto akisikiliza maelezo ya ujenzi wa jengo la taaluma la chuo cha Madini (MRI) kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Chuo Fredrick Mangasini wa kwanza kulia na wapili yake ni Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteo. 


Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Danstan Kitandula wa kwanza kushoto akimueleza jambo Waziri wa Madini Doto Biteko, anae mtazama na wa kwanza kushoto ni Issa Nchasi Mkurugezi wa Utawala na Raslimali Watu Wizara ya Madini. 

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na viongozi wa Wizara ya Madini wakiwa kwenye kikao cha majumuisho baada ya kutembelea miradi

Wednesday, March 13, 2019

Waziri Biteko azitaka nchi za Maziwa Makuu kudhibiti rasilimali ardhi


Na Issa Mtuwa Dodoma

Nchi Wanachama wa Maziwa Makuu zimetakiwa kushikamana kuunganisha nguvu katika kulinda na kusimamia matumizi ya raslimali ardhi ikiwemo madini ili kunufaisha nchi hizo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akifungua mkutano wa Kimataifa wa nchi Wanachama wa Maziwa Makuu (International Conference on the Great Lakes Region - ICGLR) unaofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 11-12 Machi 2019 katika Hotel ya Morena jijini Dodoma.

Biteko amezitaka nchi hizo kuunganisha nguvu ya pamoja katika kudhibiti raslimali ardhi ikiwemo madini na kujiwekea utaratibu utakao dhibiti shughuli za uzalishaji na biashara ya madini ili raslimali hizo zinufaishe mataifa yao na zisitumike vibaya.

“Unganisheni nguvu kwa pamoja, wekeni utaratibu utakao wafanya nchi wanachama kunufaika na raslimali ardhi/madini. Jitahidini kuhakikisha raslimali hizo hazitumiki vibaya kama ilivyo kubaliwa kwenye itifaki, hivyo lazima kuwe na utaratibu na sheria kwa kila nchi namna ya kudhibiti uzalishaji na biashara ya madini,” amesema Biteko.

Naye, Mtaalam kutoka Wizara ya Madini, Mhandisi Assah Mwakilembe amesema Mkutano huo unalenga kujadili na kupitia mfumo wa udhibitisho wa mnyororo wa madini kwa lengo la kudhibiti uzalishaji na biashara ya madini katika nchi za maziwa makuu kufuatia kuwepo tetesi zilizo kuwa zinahusisha raslimali ardhi (Madini) na ufadhili wa vita katika nchi za aaziwa makuu. (Region Certification Manual).

Akizungumza mara baada ya kuwasilisha mada kuhusu marekebisho ya Sheria Madini ya Mwaka 2017 Mkurugenzi wa Idara ya Sheria kutoka Wizara ya Madini, Edwin Igenge amesema kwa upande wa Tanzania, imetekeleza itifaki ya pamoja ya nchi wanachama wa Maziwa Makuu kama ilivyo kubaliwa.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa itifaki kwa Tanzania ni pamoja na marekebisho ya sheria ya Madini ya Mwaka 2017 yaliyopelekea kuundwa kwa Tume ya Madini ambapo shuguli zote za usimamizi wa raslimali madini zimepewa Tume ya Madini ambapo kabla ya hapo shuguli hizo zilikuwa chini ya Kamishna wa Madini.

Igenge amesema kuanzishwa kwa itifaki katika nchi za maziwa makuu kulitokana na tetesi za uwepo wa matumizi mabaya ya raslimali ardhi ikiwemo madini ambapo kipato cha raslimali hizo inasadikika kuwa zilikuwa zinatumika kufadhili shuguli za za kivita katika nchi za maziwa makuu, hivyo kupelekea kuanzishwa kwa itifaki ya pamoja kwa lengo la kudhibiti.

Mkutano huo wa kimataaifa unahudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania, Burundi, Rwanda na wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Sekretariati ya nchi wanachama wa Maziwa Makuu. Kwa upande wa  Tanzania inawakilishwa na Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Shirikisho la Wachimbaji Tanzania (FEMATA), Chama cha Wanunuzi  na Wauzaji wa  Madini Tanzania  (TAMIDA), Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa  Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST).

Katika mkutano huo, Waziri Biteko aliambatana na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Kamishna wa Madini Mhandisi Daivid Mulabwa, Mkurugenzi wa Sheria kutoka Wizara ya Madini Edwin Igenge na baadhi ya maafisa kutoka wizara ya Madini. 
Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo akiongea na wajumbe wa mkutano wa kimataaifa wa nchi wanachama wa Maziwa Makuu jijini Dodoma.
Mjumbe kutoka Burundi Gerard Nayuburundi akiwasilisha mada kwenye mkutano wa kimataifa wa nchi wanachama wa Maziwa Makuu kwenye Hotel ya Morena Jijini Dodoma.

Tuesday, March 12, 2019

Waziri Biteko ateta na wenye nia ya kuwekeza nchini


Na Asteria Muhozya,

Waziri wa Madini Doto Biteko amekutana na Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer ambaye amemweleza Waziri Biteko kuhusu ujio wa kampuni zipatazo 3 kutoka mataifa mbalimbali zenye nia ya kuwekeza katika sekta ya madini.

Dkt. Gollmer amesema kampuni hizo zimeonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya madini hususan katika masuala ya utafiti na uchimbaji wa madini kutokana na ushawishi unaofanywa na Balozi wa Tanzania nchini Urusi Meja Jenerali Mstaafu Simon Mumwi  ambaye amekuwa akihamasisha watu wa mataifa mbalimbali nchini humo kuwekeza nchini.

Pia, ameeleza kwamba, kampuni hizo hazina shaka ya kuwekeza Tanzania kutokana na mazingira tulivu ya kisisasa yaliyopo nchini pamoja na utajiri wa rasilimali madini ambayo Tanzania imejaliwa kuwa nayo.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Biteko amemweleza Dkt. Gollmer kuwa kikao hicho ni muhimu na kwamba milango kwa ajili ya wawekezaji wenye dhamira ya dhati ya kuwekeza nchini iko wazi na kuongeza kuwa, kama wizara inaratajia kukutana na kampuni hizo.
Wengine walioshiriki kikao hicho ni Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa, Mkurugeni wa Idara ya Sera na Mipango, Augustine Ollal na Katibu wa Waziri Kungulu Kasongi.


Waziri wa Madini Doto Biteko akimsikiliza Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer. 

Kamishna wa Madini David Mulabwa akizungumza jambo wakati wa kikao baina ya Waziri wa Madini Doto Biteko na Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza jambo na Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer. Anayefuatilia ni Mkurugenzi wa Ssera na Mipango Wizara ya Madini, Augustine Ollal. 

Waziri wa Madini Doto Biteko akiteta jambo na Rais wa Kampuni ya Amtec Resources Management Ltd ya nchini Uingereza, Dkt. Peter Gollmer. Kulia wanaofuatilia ni Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa na Katibu wa Waziri, Kungulu Kasongi.

Monday, March 11, 2019

Nyongo abainisha changamoto zinazoikabili sekta ya madini


Na Nuru Mwasampeta,

Licha ya kwamba Wizara ya Madini kuwa miongoni mwa wizara nyeti katika kufikia uchumi wa viwanda, inakutana na changamoto nyingi.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki katika mkutano wa hadhara na wananchi wa jimbo hilo Tarehe 9 Machi, 2019.

Naibu Waziri Nyongo alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na utoroshwaji wa Madini unaosababisha Taifa kutokupata kodi stahiki, uwepo wa mikataba isiyolinufaisha Taifa, hali mbaya ya wachimbaji wadogo na hali ya wachimbaji kufanya shughuli zao bila kuzingatia suala zima la usalama. 

Pamoja na changamoto hizo, Naibu Waziri Nyongo alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilifanyia marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 mnamo mwaka 2017.

"Mimi pamoja na uongozi wote wa wizara ya Madini tumepewa dhamana kusimamia sheria hiyo ili Madini yaliyopo nchini yanufaishe Taifa na watu wake", alisema Nyongo.

Awali kabla ya mkutano huo, Naibu Waziri Nyongo alifanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.


Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika eneo ambako ujenzi wa barabara unaendeshwa ili kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama Tawala cha CCM

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwasili katika eneo panakojengwa shule na kupokelewa na Diwani wa kata ya Nyalikungu JosephBundara.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwasili katika hospitali ya wilaya ya Maswa na kupokelewa na uongozi wa hospitali ili kujiridhisha na eneo lililochaguliwa kwa ajili ya kujenga wodi ya wanawake 

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akifuatilia hotuba ya Katibu wa CCM wa Wilaya ya Maswa alipokuwa katika mkutano wa hadhara ili kusikilia na kutatua changamoto ya wananchi wa wilaya hiyo

Nyongo akagua miradi ya maendeleo jimboni Kwake Maswa


Na Nuru Mwasampeta,

Katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na utekelezaji wa ahadi za chama kwa wananchi, Naibu Waziri wa Madini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki Stanslaus Nyongo leo amekagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo lake.

Nyongo alitembelea mradi wa ujenzi wa shule unaoendelea katika kata ya Nyalikungu na kuagiza shule hiyo ya  msingi ianze kupokea wanafunzi kuanzia mwezi huu ili kuwapa nafuu wanafunzi wanaotembea mwendo mrefu kutafuta elimu.

Aidha, Nyongo ameelekeza mwenge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakapopita katika wilaya ya Maswa, ndipo shule hiyo ifunguliwe rasmi ili kuruhusu masuala mengine ya kimaendeleo kutekelezwa.

Mara baada ya kukamilisha ukaguzi katika eneo hilo, Nyongo alielekea katika kijiji cha  ambako alikagua maendeleo ya ujenzi wa zahanati ambao haukuwa wakuridhisha aidha, alitembelea hospitali ya Wilaya ya Maswa kujionea eneo lililopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto ambalo mchakato wa ujenzi na upatikanaji wa pesa umekamilika.

Akizungumzia changamoto wanazokutana nazo katika eneo hilo la shule, Diwani wa Kata ya Nyalikungu, Joseph Bundara, alisema ni kutokuwa na barabara, huduma ya maji, umeme pamoja na ombi lakujengewa nyumba ya mwalimu ili kuishi karibu na mazingira ya shule.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi wa shule iliyopo katika kata hiyo ya Nyalikungu Katibu wa CCM wilaya ya Maswa Mwl. Mathius Filagisa alimtaka Diwani wa kata hiyo kuhakikisha wakati wa ziara za viongozi wa juu wa Chama na CCM viongozi wote na watendaji wote wa Serikali wawepo katika ziara na mikutano   ili kujibu hoja zitakazoibuka wakati wa mikutano hiyo.

Tunatekeleza Ilani ya CCM kuleta makaimu kwenye ziara za waheshimiwa haifai mjitahidi mwaunge mkono viongozi wenu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao wawapo majimboni” alikazia.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Maswa Mwl. Mathius Filagisa akizungumza jambo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo iliyofanywa na  Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo (kushoto).

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kulia) akiambatana na wajumbe wa Chama na mhandisi wa barabara akikagua ujenzi wa Barabara ya km 1.5 ikiwa ni moja ya ahadi za chama

Naibu Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki akiongea na wananchi wa jimbo hilo mara baada ya kukamilisha zoezi la ukaguzi wa miradi ya maendeleo ili kusikiliza kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi

Serikali yakasirishwa na tabia ya uongozi wa mgodi


Na Issa Mtuwa, Tarime

Waziri wa madini Mhe. Doto Biteko ameonyesha kukerwa na tabia zinazofanywa na uongozi wa juu wa mgodi wa Acacia North Mara kwa serikali  kwa kushindwa kuhudhuria vikao mbalimbali vinavyo andaliwa baina ya pande hizo mbili, licha ya baadhi ya vikao kuongozwa na Waziri wa Madini lakini viongozi wa juu wa mgodi ambao ndio wafanya maamuzi na watekelezaji wa maagizo ya serikali wamekuwa wakishindwa kuhudhuria.

Biteko amesema hayo wakati akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara jana Machi 5, 2019 katika kijiji cha Nyamongo  wilayani Tarime ikiwa  ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi kwenye migodi ya North Mara na Buhemba. Biteko amesema anakerwa na tabia za uongozi wa mgodi huo kwa kushindwa kuhudhuria mara kwa mara mikutano mbalimbali ya ndani na ile ya hadhara badala yake wamekuwa wakituma wawakilishi.

“Kuanzia leo, haki ya mungu, haki ya mungu, haki ya mungu, mimi Waziri wa Madini leo ni siku ya mwisho kukaa na hawa wawakilishi kwenye vikao, hasa kama hivi vinavyo husu hatima ya maisha ya watu alafu wafanya maamuzi hawahudhurii. Niwambie ukweli nasikitishwa sana na tabia hii. Hawa walipo sio saizi yangu, kama ni hawa hata mimi ningewaleta maafisa wa wizara tena wale wanaolingana na hawa.

Wanataka wawepo hadi afike Rais…!? nendeni mkawambie kwenye ngazi ya Wizara mimi ndio wamwisho katika kufanya maamuzi, kama mimi nipo kwa nini wao wasiwepoo…!? nyinyi mliokuja hapa nendeni mkawaambie hii ni mara ya mwisho wasifikiri serikali hii wanaweza kuiweka mfukoni, haikubaliki, hii tabia lazima ifike mwisho” alisema Biteko huku akisikitika sana.

Amesema kwa ujumla hafurahishwi na namna mambo yanavyokwenda mgodini hapo ukilinganisha na migodi mingine. Mgodi wa North Mara umezungukwa na matatizo mengi sana yakiwemo ya malipo yafidiaza wananchi, utiririshaji wa maji yenye sumu kwenda kwenye makazi ya wananchi.


Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko wa tatu kulia akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mara wakielekea kwenye eneo la uchimbaji wa TSF kulia kwake ni mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Kigoma Malima.  
Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Nyamongo wilayani  Tarime.

Biteko-Maisha ya watu yanathamani kubwa kuliko shuguli za Mgodi


Na Issa Mtuwa, Tarime

Serikali imesema itaufunga mgodi wa North Mara ifikapo Machi 30, 2019 endapo mgodi huo utashindwa kuyadhibiti maji yenye sumu yanayo tiririka kutoka kwenye mabwawa ya kuhifadhia maji (topesumu) (Tailings Storage Facility -TSF) ya mgodi huo kuelekea kwenye makazi ya watu.

Hayo yamesemwa leo machi 5, 2019 na Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko alipotembelea mgodini hapo kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea mabwawa wa topesumu (TSF) na kuzungumza na uongozi wa mgodi na baadae na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nyamongo wilaya ya Tarime kuzungumzia hatima ya malipo ya fidia za wananchi waliohamishwa kupisha shuguli  za mgodi.

Biteko amesema serikali hairidhishwi na namna mgodi wa North Mara kwa jinsi wanavyo zingatia swala la utunzaji wa maji yenye sumu kwenye (TSF) zao. Amesema serikali inathamini sana maisha ya watu na mtu mmoja mmoja, na kwamba maisha ya mtu mmoja ni bora kuliko shuguli zote za mgodi.

“Naomba niseme ukweli, tena kutoka moyoni, sijaridhishwa na hili jambo la utiririshaji wa maji yenye sumu kuelekea kwenye makazi ya watu. Serikali hii ya awamu ya tano ya Dkt. John Pombe Magufuli inathamini sana maisha ya watu wake kuliko kitu chochote. Thamani yamaisha ya mtanzania mmoja ni bora kuliko kinachochibwa hapa. Nitoe rai kwa mgodi ifikapo Machi 30, mwaka huu, hili jambo liwe limekwisha, kinyume cha hapo, nitafunga mgodi mpaka pale mtakapo tekeleza jambo hili” alisema Biteko.

Kwa upande wa uongozi wa mgodi umesema, utatekeleza agizo hilo na kwamba juhudi za kudhibiti topesumu kuelekea kwenye makazi ya watu limepewa kipaumbele na kwamba ndani ya muda huo litakuwa limekamilika.

Katika ziara hiyo, Waziri Biteko aliambatana na baadhi ya Maafisa wa Wizara hiyo akiwemo Kamishna wa Madini Mha. David Mlabwa na Afisa Madini mkoa wa Mara Mha. Nyaisara Mgaya, wengine ni kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa mara wakiongwa na mwenyekiti wake ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Mara bwana Adam Kigoma Malima.

Ziara hiyo inafuatia vikao mbalimbali vya awali vilivyofanyika mwaka huu vikilenga masuala mbalimbali yanoyo husu mgodi huo likiwemo swala la udhibiti wa maji yenye sumu (topesumu) yanayo lalamikiwa na wananchi wanaoishi kuzunguka mgodi huo, kikao cha kwanza kilifanyika Januari 19, chini ya makatibu wakuu wa wizara saba ((Madini, Makamu wa Rais Mazingira (NEMC), Ardhi, TAMISEMI, Afya, Fedha na Maji)) ambapo serikali ilitoa miezi nane kutekeleza maagizo yaliyopewa.


Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko wa kwanza kulia akimsikiliza mwenyekiiti wa kamati ya ulinzi na usalama na mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima wa kwanza kushoto akitoa taarifa fupi ya hali ya mkoa wake wakiwa kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Tarime. 

Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko akionyesha kwa kuuliza mwisho wa mpaka wa eneo la ujenzi  wa TSF mpya, kushoto kwake ni Mkuu  wa Wilaya Tarime.