Thursday, May 3, 2018

Waziri Kairuki akutana na wafanyakazi wa STAMICO, alitaka kudhibiti wizi wa madini migodini


Na Coletha Njelekeka, STAMICO

Waziri wa Madini Angellah Kairuki ameitaka Menejimenti ya Shirika la Madini la Taifa  (STAMICO) na Wafanyakazi kuimarisha udhibiti wa wizi wa madini katika migodi yake ili kukuza mapato ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

Kairuki alitoa rai hiyo wakati alipofanya ziara ya utambulisho kwa Menejimenti na Wafanyakazi wa STAMICO tarehe 27 Aprili, 2018, na kuzungumza na watumishi ikiwemo kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya STAMICO.

Katika kudhibiti wizi wa madini migodini yakiwemo ya vito, STAMICO aliitaka iteue timu za wataalam wenye ujuzi katika uthaminishaji wa madini na wenye uzalendo kwa nchi yao; kwa kuwa watasaidia kutambua thamani ya madini husika wakati wa mauzo, hatimaye kuweza kudhibiti wizi wa madini utokanao na uthaminishaji wa madini.

“Wataalam wenu STAMICO pia washiriki kikamilifu na kwa karibu zaidi katika shughuli za uzalishaji madini zinazoendelea katika makampuni tanzu ya Shirika kama vile uzalishaji na uuzaji wa madini ya Dhahabu katika Mgodi wenu wa Dhahabu wa Bihaharamulo unaoendeshwa na Kampuni tanzu ya Shirika yaani STAMIGOLD” alisisitiza Kairuki.

Aidha Waziri Kairuki aliitaka Menejimenti ya STAMICO pia kutumia uzoefu wa Usimamizi wa migodi na uendeshaji wa Makampuni tanzu ya madini yanayomilikiwa na Mashirika ya Madini ya Taifa ya nchi mbalimbali Barani Afrika; zikiwemo Namibia na Afrika ya Kusini; ili kuliwezesha Shirika kujizatiti katika uendeshaji endelevu wa migodi na makampuni yake tanzu.

Katika ziara yake hiyo ya utambulisho tangu alipoteuliwa rasmi kuwa Waziri wa Madini, Waziri Kairuki aliambatana na  Naibu Waziri Doto Biteko na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji majukumu ya STAMICO, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku, amemweleza Kairuki kuwa STAMICO itaendelea kuimarisha usimamizi wa miradi yake inayoisimamia kwa asilimia 100 na ile ya ubia; ili kuongeza mapato yatokanao ya madini na hivyo kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi na pato la Taifa.

“Utekelezaji wa shughuli za STAMICO za uchimbaji madini unahusisha uzalishaji wa Makaa ya Mawe katika mgodi wa Kabulo-Kiwira, uzalishaji wa madini ya Tanzanite katika mradi wa ubia wa TanzaniteOne uliopo Mirerani; uzalishaji wa madini ya dhahabu katika Kampuni tanzu STAMIGOLD-Biharamulo na uendelezaji wamiradi ya uchimbaji wa dhahabu wa Buhemba na Buckreef” Alifafanua Kanali Mhandisi Ghuliku.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila alisisitiza kuhusu suala zima la Watumishi kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji kwa manufaa ya Shirika na Taifa kwa ujumla.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akizungumza na wafanyakazi wakati wa ziara ya kutembelea Shirika la Madini la Taifa iliyolenga kuboresha miradi na ustawi wa Shirika. 


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akitoa maelekezo kwa viongozi wa Shirika kuhusu uboreshaji wa miradi ya STAMICO baada ya kupokea taarifa ya miradi ya STAMICO.


Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akisalimiana na viongozi wa STAMICO mara baada ya kuwasili katika ofisi za shirika hilo.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa STAMICO. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila. Wa pili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku.

Wizara za Nishati na Madini zilivyoadhimisha Mei Mosi, Dar es Salaam


Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam

Watumishi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini katika matukio mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Maandamano ya Wafanyakazi walioshiriki maadhimisho hayo kutoka Wizara, Idara, Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, yalianzia viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo sherehe hizo zilifanyika katika Ngazi ya Mkoa.




Wednesday, May 2, 2018

Nishati, Madini waadhimisha Mei Mosi kwa mafanikio


Na Veronica Simba, Dodoma

Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini, walioko Makao Makuu Dodoma, wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha sikukuu ya Mei Mosi.

Katika kuadhimisha sikukuu hiyo muhimu, wafanyakazi hao walishiriki maandamano yaliyoanzia katika viwanja vya bunge na kuhitimishwa katika uwanja wa Jamhuri, ambapo walipokewa na Mgeni Rasmi; Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge.

Pamoja na mambo mengine yaliyofanyika wakati wa sherehe hizo, wafanyakazi bora walipatiwa zawadi na vyeti vya kutambua mchango wao.

Baadhi ya Wafanyakazi bora kutoka Idara mbalimbali za Wizara ya Nishati ni Mwamvita Mkakile kutoka Idara ya Nishati, Margaret Vava (Utawala) na Vera Sikana (Sera na Mipango). Taratibu za kuwapata wafanyakazi bora wengine kutoka Idara zilizosalia zinakamilishwa ili waweze kupatiwa vyeti pamoja na zawadi zao.

Kwa upande wa Wizara ya Madini, wafanyakazi bora ni Happy Ndunguru kutoka Idara ya Utawala ambaye pia ndiye mfanyakazi bora wa Wizara. Wengine ni Eugenia Mashoko (Uhasibu), Godfrey Nyamsenda (Sheria), Zuwena Msuya (Mawasiliano Serikalini), Josephat Mbwambo (Sera na Mipango), Christopher Mwita (TEHAMA), Dorothy Mtweve (Madini), Eric Kwesigabo (Ugavi) na Hassan Ngwandu (Ukaguzi wa Ndani).


Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini waliopo Makao Makuu Dodoma, wakishiriki maandamano ya Mei Mosi, 2018.


Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini waliopo Makao Makuu Dodoma, wakishiriki maandamano ya Mei Mosi, 2018.


Baadhi ya wafanyakazi bora kutoka Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini, wakipokea cheti na zawadi kutoka kwa Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge wakati wa maadhimisho ya sherehe ya wafanyakazi (Mei Mosi).


Baadhi ya wafanyakazi bora kutoka Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini, wakipokea cheti na zawadi kutoka kwa Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge wakati wa maadhimisho ya sherehe ya wafanyakazi (Mei Mosi).


Baadhi ya wafanyakazi bora kutoka Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini, wakipokea cheti na zawadi kutoka kwa Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge wakati wa maadhimisho ya sherehe ya wafanyakazi (Mei Mosi).


Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini walioko Makao Makuu Dodoma, wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa maadhimisho ya sherehe ya wafanyakazi (Mei Mosi).


Baadhi ya wafanyakazi bora wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini walioko Makao Makuu Dodoma, (walioshika vyeti) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wenzao, mara baada ya kukabidhiwa zawadi na vyeti rasmi wakati wa maadhimisho ya sherehe ya wafanyakazi (Mei Mosi).


Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini walioko Makao Makuu Dodoma, wakiwa katika Ofisi za Wizara, muda mfupi kabla ya kuanza maandamano ya sherehe ya wafanyakazi (Mei Mosi).


Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini walioko Makao Makuu Dodoma, wakiwa katika Ofisi za Wizara, muda mfupi kabla ya kuanza maandamano ya sherehe ya wafanyakazi (Mei Mosi).

Waziri Kairuki azindua ripoti ya nane ya TEITI


Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Leo tarehe 30 Aprili, 2018 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta Tanzania (TEITI) kwa  kushirikiana na Mtaalam Mwelekezi, Boas & Associates na MM Attoneys.

Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha  wawakilishi  kutoka Kamati  ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi, Waziri Kairuki amepongeza  Kamati ya TEITI na Sekretarieti kwa mchango wake katika uandaaji  wa ripoti hiyo.

Mbali na  Pongezi hizo, Kairuki ameiagiza Kamati ya  TEITI kuongeza nguvu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa mpana wa umuhimu na wajibu  wa TEITI  kwa kutumia mbinu mbalimbali  ikiwa ni pamoja na warsha mbalimbali pamoja na vipindi vya redio na  televisheni.

Amesisitiza kuwa,  kipaumbele kiwekwe kwenye maeneo  yaliyozungukwa na shughuli za utafutaji na uzalishaji wa madini, mafuta na gesi asilia na kupata taarifa ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Awali akielezea ripoti hiyo,  Kairuki amesema kuwa ripoti hiyo  inahusu tathmini  ya mapato ya madini katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai, 2015 hadi tarehe 30 Juni, 2016 na kufafanua kuwa jumla ya shilingi 434,627,874,380 zilipokelewa serikalini  kutoka kwenye kampuni 55 za madini, mafuta na gesi  asilia zilizoshiriki zoezi la ulinganishi.

Hata hiyo amesema taarifa inaonesha kuwa kampuni zililipa kiasi cha shilingi 465,164,747,725 za kitanzania serikalini na kusababisha tofauti kati ya malipo kuwa ni pungufu ya shilingi 30,536,873,345 za kitanzania chini ya kiasi ambacho Serikali imekiri kupokea.

“ Ni lazima tufahamu ni vipi imejitokeza tofauti hii na ninachukua fursa hii kuelekeza taarifa hii kupelekwa kwa Mkaguzi Mkuu  wa Hesabu za Serikali  kwa ajiili ya  uchunguzi  kama kifungu 18(1) cha Sheria ya TEITI ya mwaka 2015 kinavyotaka,” alisema Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine,  Waziri Kairuki  amefafanua kuwa ripoti  imeonesha  kuwa sekta ya madini  imechangia zaidi kwa asilimia 85 na sekta  ya mafuta na gesi ikionyesha kuchangia asilimia 15 ya mapato ya Serikali chini ya Sekta ya Madini kwa mwaka 2015/16.

Akielezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya madini, Kairuki amesema kuwa ili kuhakikisha madini yanakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, Serikali imeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

Ametaja hatua nyingine ambayo ni endelevu kuwa ni kufanya tathmini ya jinsi gani nchi  inapata mapato yake kwenye sekta ya madini kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa.

Ameendelea kusema kuwa jukumu linafanywa na taasisi mbalimbali  za Serikali lakini TEITI nayo inatekeleza jukumu husika kwa kuhakikisha taarifa za mapato ya madini zinatolewa kwa uwazi kwa wananchi na wadau mbalimbali katika Serikali,  Sekta Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.

Katika hatua nyingine Waziri Kairuki amezitaka kampuni nyingine ambazo hazikushiriki katika kipindi cha ukaguzi kujitokeza katika ukaguzi unaofuata ili  takwimu  halisi za mapato zifahamike.

Aidha, ametumia fursa hiyo kukaribisha kampuni nyingine zenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya madini kujitokeza kwa wingi  ili sekta ya madini iwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Wakati huo huo akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa mara baada ya ripoti kuzinduliwa na kukabidhiwa kwa Kamati ya TEITI hatua inayofuatia ni kamati ya TEITI kuwasilisha ripoti hiyo kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili achukue hatua kwenye hoja zilizotokana na ripoti hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akifafanua jambo kwenye uzinduzi wa ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha wawakilishi kutoka Kamati ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi tarehe 30 Aprili, 2018.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki akisoma hotuba ya uzinduzi wa ripoti ya Nane ya  ulinganishi wa mapato ya  Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha wawakilishi kutoka Kamati ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi tarehe 30 Aprili, 2018.

Kutoka kulia mbele, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Augustina Rutaihwa wakifuatilia ripoti ya Nane ya  ulinganishi wa mapato ya  Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 iliyokuwa inawasilishwa na mtaalam mwelekezi kutoka kampuni ya Boas & Associates na MM Attoneys, Symphorian Malingumu (hayupo pichani).

Mtaalam mwelekezi kutoka kampuni ya Boas & Associates na MM Attoneys, Symphorian Malingumu akiwasilisha ripoti ya Nane ya  ulinganishi wa mapato ya  Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16 kwenye uzinduzi huo.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (wa pili kulia mbele) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi kutoka Kamati na Sekretarieti ya TEITI mara baada ya kuzindua ripoti hiyo.

Tuesday, April 17, 2018

Uzinduzi wa ukuta Mirerani


ü RAIS MAGUFULI ATOA AJIRA KWA VIJANA 2,038 WALIOJENGA
ü SERIKALI YATOA TSH. MILIONI 100 KWA ALIYEVUMBUA TANZANITE
ü MRABAHA KUTOKA  KWA WACHIMBAJI  WAPANDA

Na Asteria Muhozya, Mirerani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John  Magufuli ametoa ajira kwa Vijana wa JKT 2,038 wa Operesheni Kikwete na Operesheni Magufuli, waliojenga Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa Sherehe ya Uzinduzi wa ukuta iliyofanyika eneo la geti la kuingilia ndani ya ukuta huo tarehe 6 Aprili, 2018 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Viongozi wa dini, waandishi wa habari na wananchi wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na mikoa jirani.

Aliongeza kuwa, vijana hao wa JKT wameonesha uzalendo wa hali juu hivyo kuwezesha kukamilika kwa ukuta huo kwa wakati na kuongeza " mmejiuza wenyewe, sijakataa wale watakaokuwa tayari tutawatumia katika majeshi yetu yote," alisisitiza Rais Magufuli.

Pi, alitumia fursa hiyo kulipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo lilijenga ukuta huo kupitia SUMA JKT na kuongeza kuwa, anajivunia jeshi hilo  na kwamba anajisikia furaha kuwa Mtanzania.

"Mwaka 2018, naliona Jeshi lililomtoa Nduli. Nazishukuru na kuzipongeza Wizara ya Madini kuanzia Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Kamishna na Watendaji wote na ninaishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na  Majeshi yote," alisema  Rais Magufuli.

Akieleza kukamilika kwa ukuta huo, Rais Magufuli alisema kuwa, umekamilika ndani ya kipindi kifupi kutokana na uzalendo mkubwa na juhudi za jeshi hilo na kusema kuwa, awali ilipangwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita lakini ulikamilika kwa muda wa miezi 3.

Akizungumzia suala la wachimbaji wadogo na kuwataka  kutokuwa na wasiwasi kutokana na kujengwa kwa ukuta na kueleza kuwa, Serikali itajenga mazingira mazuri kuhakikisha kuwa wachimbaji wote wakubwa na wadogo wananufaika na madini hayo ikiwemo Serikali.

"Hakuna kitakachoharibika. Kampuni zote zitaingia mkataba na Serikali watanunua hapa hapa na watakaouza watayauzia hapa hapa. Tutafungua mabenki, tutaanzisha utalii wa madini. Nia ya Serikali ni kuweka mazingira mazuri kwa Mirerani, Simanjiro, Manyara na hatimaye watanzania wanufaike," alisisitiza Rais Magufuli.

Akitaja faida za ukuta huo, Rais Magufuli alisema kuwa,  utaiamarisha usalama na thamani ya fedha itaonekana miongoni mwa wananchi na Taifa.

Wakati huo huo, Rais Magufuli alitoa kiasi cha shilingi millioni 100  kwa kugharimia matibabu kwa Mzee Jumanne Ngoma aliyevumbua madini hayo mnamo mwaka 1967.

Aidha,  aliwataka watanzania kuthamini mazuri yanayofanywa na watanzania kwa nchi na kuongeza kuwa, jambo hilo ni mwanzo mzuri wa kuwakumbuka mashujaa wa nchi akiwemo Mzee Ngoma aliyeweka jina la Tanzanite.

Naye, Mzee Jumanne Ngoma alimshukuru Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake wa uvumbuzi wa madini hayo na kusema kuwa, baada ya kuona ukuta umejengwa ameona thamani ya madini ya Tanzanite ikiongezeka.

Awali, akizungumza katika sherehe hizo Waziri wa Madini Angellah Kairuki alisema kuwa, Wizara inaandaa Kanuni za Mirerani Controlled Area  za mwaka 2018 ambazo zitatoa mwongozo wa namna shughuli za uchimbaji, biashara ya madini  na huduma za jamii zitakavyoendeshwa ndani ya ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya Tanzanite, ambazo zitakamilishwa wiki ijayo.

Kairuki alilishukuru jeshi na kulipongeza kwa nidhamu, utii na weledi mkubwa ambao umewezesha ukuta huo kukamilika  kabla ya muda uliopangwa, na kuongeza ukuta huo umeiweka Tanzania katika Dunia  na ukombozi wa kiuchumi.

" Mhe Rais uongozi wako dhabiiti umeleta mabadiliko katika sekta ya madini. Umiliki na udhibiti wa madini haya ni nguzo muhimu na Mhe. Rais umeonesha kwa vitendo kulinda rasilimali ," alisema Kairuki.

Aliongeza kuwa, kwa miaka mingi uwepo wa madini hayo hakulinufaisha taifa ipasavyo ikilinganishwa na thamani ya madini hayo na kuongeza kuwa, udhibiti wake haukuwa mkubwa na hivyo kupekelea madini mengi kupelekewa nje ya nchi
Akizungumzia mapato baada ya kuweka udhibiti Waziri Kairuki alisema  malipo ya mrabaha kutoka mwezi Januari hadi 17 Machi, 2018 yalikuwa shilingi milioni 714.6 kwa miezi mitatu tu ambayo yamezidi  wastani wa malipo kwa miaka 2015,2016 na 2017

"Haya ni matokeo chanya ya udhibiti wa shughuli za uzalishaji katika migodi ya Tanzanite Mirerani.  Ukuta huu utaongeza zaidi uwezo wetu wa usimamizi wa rasilimali hii." alisema Waziri Kairuki.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Kairuki, Huko nyuma, malipo ya mrabaha kutoka kwa wachimbaji wa Mirerani ukiondoa Tanzanite One na STAMICO yalikuwa Shilingi 166.8 milioni kwa mwaka 2015, Shilingi 71.8 milioni kwa mwaka 2016 na Shilingi 147.1 milioni kwa mwaka 2017.

Maelekezo ya ujenzi wa ukuta huo yalitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, kujenga  uzio wa  ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite Mirerani tarehe 20 Septemba, 2017 kwenye uzinduzi wa Barabara ya KIA kwenda Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Ukuta wa mirerani una urefu wa kilomita 24.5 na umejengwa kwa kipindi cha miezi mitatu tofauti na ilivyopangwa awali  wa kujengwa miezi sita.

Uzinduzi wa ukuta ulikwenda sambamba na maonesho ya madini ya vito ambapo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), zilishiriki maonesho hayo, Kituo cha Jemolojia  Tanzania (TGC) pamoja na kampuni mbalimbali zinazofanya shughuli za uchimbaji na uuzaji wa madini hayo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akikata utepe kuashirikia uzinduzi wa ukuta uliojengwa kuzunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani. Wa tatu kutoka kushoto ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki. Wa pili kulia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, wa kwanza kulia ni Mke wa Rais Magufuli Mama Janeth Magufuli. Wengine wanaoshuhudia ni viongozi mbalimbali wa Serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akionesha ufunguo ya mfano kuashirikia uzinduzi wa Ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya Tanzanite, Mirerani. Wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Alexander Mnyeti.
Jiwe la Msingi lililowekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli  kushoto akiteta jambo la Mzee Jumanne Ngoma (katikati) aliyevumbua Madini ya Tanzanite mwaka 1967. Kulia ni Mke wa Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli.

Taifa limeweka historia - Mkuu wa Majeshi


Na Asteria Muhozya, Mirerani

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo amesema  ujenzi wa ukuta wa Mirerani umeweka Historia ambayo itadumu kwa miongo mingi.

Jenerali Mabeyo aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wakati wa sherehe ya Uzinduzi wa ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite Mirerani uliofanyika tarehe 6 Aprili,2018.

Alisema kuwa, utayari wa Jeshi na vijana wa JKT umeonesha taaluma zote  huku vijana 2,038 waliojenga ukuta huo wakiwa alama ya uzalendo kwa Taifa la Tanzania.

Jenerali Mabeyo aliongeza uwezo wa jeshi wa kutumia wataalam wake wa ndani na kufanya kazi kwa moyo kumepelekea mafanikio ya ujenzi wa ukuta huo  na hivyo, kuwataka watanzania wote kujivunia nchi yao, kulinda rasilimali zote za nchi ikiwemo madini na amani ya taifa.

Pia, alisema kuwa, nidhamu ya jeshi imezingatia weledi, uharaka jambo ambalo limepelekea shughuli hiyo kufanyika kwa kipindi kifupi.
" Daima tuko imara kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utu wetu ndiyo nguzo kubwa,"alisema Jenerali Mabeyo.

Jenerali Mabeyo alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Mirerani kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Jeshi hilo kwa kipindi chote cha ujenzi wa ukuta huo na kueleza kuwa, ushirikiano huo umeoneshwa na watanzania wapenda maendeleo.

Alisema kuwa, ukuta huo umejengwa na wahandisi wa ujenzi kutoka JKT, JWTZ wakiwemo Maafisa 34, Askari 287 na Vijana 2,038 wa Operesheni Kikwete na Opereshi Magufuli.

"Mheshimiwa Rais inawezekana  kuna watu wakaona kuwa shilingi bilioni 5.645,843,163.55 ni nyingi sana lakini baada ya rasilimali hizi kutumika kikamilifu  huenda fedha hizi zikawa kidogo. Hii ndiyo nguvu kazi ya Watanzania na uwezo wa Jeshi letu," alisema Jenerali Mabeyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  Dkt. Hussein Mwinyi, alisema kuwa  ujenzi wa ukuta huo unadhihirisha ulinzi wa rasilimali za nchi na kuwa umeweka historia mpya.

Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Mirerani kuwapokea vizuri wanajeshi  na pia kuwashukuru vijana wa JKT kwa namna walivyojituma na hatimaye kufanikisha ujenzi huo.

Pia,  Waziri  Dkt. Mwinyi alisema kuwa, jeshi litaendelea kuwa imara  na makini katika kutekeleza maagizo na majukumu yake wakati wote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akipokea hati ya ukuta kutoka kwa Waziri wa Ulinzi Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza jambo wakati wa Sherehe ya Uzinduzi wa ukuta kuzunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza jambo wakati wa Sherehe ya Uzinduzi wa ukuta kuzunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo akizungumza jambo wakati wa Sherehe za uzinduzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite, Mirerani.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Martin Busungu (kulia) wakati wa sherehe ya uzinduzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite, Mirerani.

Ujenzi wa ukuta umefanyika kwa ubora-Meja Jenerali Busungu


Na Asteria Muhozya, Mirerani

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Martin Busungu amesema kuwa ujenzi wa ukuta  unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani wenye urefu wa kilomita 24.5, umefanyika kwa ubora na viwango vya juu.

"Vijana wamefanya kazi kwa uzalendo wa hali ya juu na kujitolea. Tumetekeleza kwa ukamilifu weledi na chini ya muda uliopangwa," alisisitiza Meja Jenerali Busungu.

Meja Jenerali Busungu aliyasema hayo wakati wa sherehe za uzinduzi wa ukuta huo uliofanyika tarehe 6 Aprili, 2018, eneo la geti la kuingilia ukuta huo Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara na kuongeza kuwa, ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 5.645,843,163.55.

Meja Jenerali Busungu aliongeza kuwa, matokeo ya ujenzi huo kuwa na ubora na kuchukua kipindi kifupi yalitokana na uadilifu mkubwa wa jeshi na hilo linaonesha kuwa, kazi ya Jeshi si  tu kulinda mipaka, Katiba ya nchi  bali pia kujenga nchi ya Tanzania na kuhakikisha kuwa, rasilimali za zinakuwa salama kwa vizazi vijavyo.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi na wenyeji wa mji wa Mirerani kwa kutoa historia ya eneo hilo ikiwemo mapitio ya maji na njia za wanyama jambo ambalo liliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Pia, alisema kuwa, ukuta huo ulijengwa na vikosi 20 vya jeshi vikijumuisha wataalam wa ujenzi, Wahandisi, Vijana wa JKT wa Operesheni Kikwete na Operesheni Magufuli na Watumishi wa umma.


Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Martin   Busungu akiongea jambo wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Ukuta kuzunguka migodi ya tanzanite Mirerani
Vijana wa JKT wakiendelea na ujenzi wakati wa hatua mbalimbali za ujenzi wa ukuta kuzunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani.

Vijana wa JKT wakiendelea na ujenzi wakati wa hatua mbalimbali za ujenzi wa ukuta kuzunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani.