Thursday, May 3, 2018

Waziri Kairuki akutana na wafanyakazi wa STAMICO, alitaka kudhibiti wizi wa madini migodini


Na Coletha Njelekeka, STAMICO

Waziri wa Madini Angellah Kairuki ameitaka Menejimenti ya Shirika la Madini la Taifa  (STAMICO) na Wafanyakazi kuimarisha udhibiti wa wizi wa madini katika migodi yake ili kukuza mapato ya Shirika na Taifa kwa ujumla.

Kairuki alitoa rai hiyo wakati alipofanya ziara ya utambulisho kwa Menejimenti na Wafanyakazi wa STAMICO tarehe 27 Aprili, 2018, na kuzungumza na watumishi ikiwemo kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya STAMICO.

Katika kudhibiti wizi wa madini migodini yakiwemo ya vito, STAMICO aliitaka iteue timu za wataalam wenye ujuzi katika uthaminishaji wa madini na wenye uzalendo kwa nchi yao; kwa kuwa watasaidia kutambua thamani ya madini husika wakati wa mauzo, hatimaye kuweza kudhibiti wizi wa madini utokanao na uthaminishaji wa madini.

“Wataalam wenu STAMICO pia washiriki kikamilifu na kwa karibu zaidi katika shughuli za uzalishaji madini zinazoendelea katika makampuni tanzu ya Shirika kama vile uzalishaji na uuzaji wa madini ya Dhahabu katika Mgodi wenu wa Dhahabu wa Bihaharamulo unaoendeshwa na Kampuni tanzu ya Shirika yaani STAMIGOLD” alisisitiza Kairuki.

Aidha Waziri Kairuki aliitaka Menejimenti ya STAMICO pia kutumia uzoefu wa Usimamizi wa migodi na uendeshaji wa Makampuni tanzu ya madini yanayomilikiwa na Mashirika ya Madini ya Taifa ya nchi mbalimbali Barani Afrika; zikiwemo Namibia na Afrika ya Kusini; ili kuliwezesha Shirika kujizatiti katika uendeshaji endelevu wa migodi na makampuni yake tanzu.

Katika ziara yake hiyo ya utambulisho tangu alipoteuliwa rasmi kuwa Waziri wa Madini, Waziri Kairuki aliambatana na  Naibu Waziri Doto Biteko na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji majukumu ya STAMICO, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku, amemweleza Kairuki kuwa STAMICO itaendelea kuimarisha usimamizi wa miradi yake inayoisimamia kwa asilimia 100 na ile ya ubia; ili kuongeza mapato yatokanao ya madini na hivyo kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi na pato la Taifa.

“Utekelezaji wa shughuli za STAMICO za uchimbaji madini unahusisha uzalishaji wa Makaa ya Mawe katika mgodi wa Kabulo-Kiwira, uzalishaji wa madini ya Tanzanite katika mradi wa ubia wa TanzaniteOne uliopo Mirerani; uzalishaji wa madini ya dhahabu katika Kampuni tanzu STAMIGOLD-Biharamulo na uendelezaji wamiradi ya uchimbaji wa dhahabu wa Buhemba na Buckreef” Alifafanua Kanali Mhandisi Ghuliku.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila alisisitiza kuhusu suala zima la Watumishi kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji kwa manufaa ya Shirika na Taifa kwa ujumla.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akizungumza na wafanyakazi wakati wa ziara ya kutembelea Shirika la Madini la Taifa iliyolenga kuboresha miradi na ustawi wa Shirika. 


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akitoa maelekezo kwa viongozi wa Shirika kuhusu uboreshaji wa miradi ya STAMICO baada ya kupokea taarifa ya miradi ya STAMICO.


Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akisalimiana na viongozi wa STAMICO mara baada ya kuwasili katika ofisi za shirika hilo.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa STAMICO. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko. Wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila. Wa pili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku.

No comments:

Post a Comment