Tuesday, April 17, 2018

Uzinduzi wa ukuta Mirerani


ü RAIS MAGUFULI ATOA AJIRA KWA VIJANA 2,038 WALIOJENGA
ü SERIKALI YATOA TSH. MILIONI 100 KWA ALIYEVUMBUA TANZANITE
ü MRABAHA KUTOKA  KWA WACHIMBAJI  WAPANDA

Na Asteria Muhozya, Mirerani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John  Magufuli ametoa ajira kwa Vijana wa JKT 2,038 wa Operesheni Kikwete na Operesheni Magufuli, waliojenga Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa Sherehe ya Uzinduzi wa ukuta iliyofanyika eneo la geti la kuingilia ndani ya ukuta huo tarehe 6 Aprili, 2018 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Viongozi wa dini, waandishi wa habari na wananchi wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na mikoa jirani.

Aliongeza kuwa, vijana hao wa JKT wameonesha uzalendo wa hali juu hivyo kuwezesha kukamilika kwa ukuta huo kwa wakati na kuongeza " mmejiuza wenyewe, sijakataa wale watakaokuwa tayari tutawatumia katika majeshi yetu yote," alisisitiza Rais Magufuli.

Pi, alitumia fursa hiyo kulipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo lilijenga ukuta huo kupitia SUMA JKT na kuongeza kuwa, anajivunia jeshi hilo  na kwamba anajisikia furaha kuwa Mtanzania.

"Mwaka 2018, naliona Jeshi lililomtoa Nduli. Nazishukuru na kuzipongeza Wizara ya Madini kuanzia Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Kamishna na Watendaji wote na ninaishukuru Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na  Majeshi yote," alisema  Rais Magufuli.

Akieleza kukamilika kwa ukuta huo, Rais Magufuli alisema kuwa, umekamilika ndani ya kipindi kifupi kutokana na uzalendo mkubwa na juhudi za jeshi hilo na kusema kuwa, awali ilipangwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita lakini ulikamilika kwa muda wa miezi 3.

Akizungumzia suala la wachimbaji wadogo na kuwataka  kutokuwa na wasiwasi kutokana na kujengwa kwa ukuta na kueleza kuwa, Serikali itajenga mazingira mazuri kuhakikisha kuwa wachimbaji wote wakubwa na wadogo wananufaika na madini hayo ikiwemo Serikali.

"Hakuna kitakachoharibika. Kampuni zote zitaingia mkataba na Serikali watanunua hapa hapa na watakaouza watayauzia hapa hapa. Tutafungua mabenki, tutaanzisha utalii wa madini. Nia ya Serikali ni kuweka mazingira mazuri kwa Mirerani, Simanjiro, Manyara na hatimaye watanzania wanufaike," alisisitiza Rais Magufuli.

Akitaja faida za ukuta huo, Rais Magufuli alisema kuwa,  utaiamarisha usalama na thamani ya fedha itaonekana miongoni mwa wananchi na Taifa.

Wakati huo huo, Rais Magufuli alitoa kiasi cha shilingi millioni 100  kwa kugharimia matibabu kwa Mzee Jumanne Ngoma aliyevumbua madini hayo mnamo mwaka 1967.

Aidha,  aliwataka watanzania kuthamini mazuri yanayofanywa na watanzania kwa nchi na kuongeza kuwa, jambo hilo ni mwanzo mzuri wa kuwakumbuka mashujaa wa nchi akiwemo Mzee Ngoma aliyeweka jina la Tanzanite.

Naye, Mzee Jumanne Ngoma alimshukuru Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake wa uvumbuzi wa madini hayo na kusema kuwa, baada ya kuona ukuta umejengwa ameona thamani ya madini ya Tanzanite ikiongezeka.

Awali, akizungumza katika sherehe hizo Waziri wa Madini Angellah Kairuki alisema kuwa, Wizara inaandaa Kanuni za Mirerani Controlled Area  za mwaka 2018 ambazo zitatoa mwongozo wa namna shughuli za uchimbaji, biashara ya madini  na huduma za jamii zitakavyoendeshwa ndani ya ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya Tanzanite, ambazo zitakamilishwa wiki ijayo.

Kairuki alilishukuru jeshi na kulipongeza kwa nidhamu, utii na weledi mkubwa ambao umewezesha ukuta huo kukamilika  kabla ya muda uliopangwa, na kuongeza ukuta huo umeiweka Tanzania katika Dunia  na ukombozi wa kiuchumi.

" Mhe Rais uongozi wako dhabiiti umeleta mabadiliko katika sekta ya madini. Umiliki na udhibiti wa madini haya ni nguzo muhimu na Mhe. Rais umeonesha kwa vitendo kulinda rasilimali ," alisema Kairuki.

Aliongeza kuwa, kwa miaka mingi uwepo wa madini hayo hakulinufaisha taifa ipasavyo ikilinganishwa na thamani ya madini hayo na kuongeza kuwa, udhibiti wake haukuwa mkubwa na hivyo kupekelea madini mengi kupelekewa nje ya nchi
Akizungumzia mapato baada ya kuweka udhibiti Waziri Kairuki alisema  malipo ya mrabaha kutoka mwezi Januari hadi 17 Machi, 2018 yalikuwa shilingi milioni 714.6 kwa miezi mitatu tu ambayo yamezidi  wastani wa malipo kwa miaka 2015,2016 na 2017

"Haya ni matokeo chanya ya udhibiti wa shughuli za uzalishaji katika migodi ya Tanzanite Mirerani.  Ukuta huu utaongeza zaidi uwezo wetu wa usimamizi wa rasilimali hii." alisema Waziri Kairuki.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri Kairuki, Huko nyuma, malipo ya mrabaha kutoka kwa wachimbaji wa Mirerani ukiondoa Tanzanite One na STAMICO yalikuwa Shilingi 166.8 milioni kwa mwaka 2015, Shilingi 71.8 milioni kwa mwaka 2016 na Shilingi 147.1 milioni kwa mwaka 2017.

Maelekezo ya ujenzi wa ukuta huo yalitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, kujenga  uzio wa  ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite Mirerani tarehe 20 Septemba, 2017 kwenye uzinduzi wa Barabara ya KIA kwenda Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Ukuta wa mirerani una urefu wa kilomita 24.5 na umejengwa kwa kipindi cha miezi mitatu tofauti na ilivyopangwa awali  wa kujengwa miezi sita.

Uzinduzi wa ukuta ulikwenda sambamba na maonesho ya madini ya vito ambapo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), zilishiriki maonesho hayo, Kituo cha Jemolojia  Tanzania (TGC) pamoja na kampuni mbalimbali zinazofanya shughuli za uchimbaji na uuzaji wa madini hayo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akikata utepe kuashirikia uzinduzi wa ukuta uliojengwa kuzunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani. Wa tatu kutoka kushoto ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki. Wa pili kulia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, wa kwanza kulia ni Mke wa Rais Magufuli Mama Janeth Magufuli. Wengine wanaoshuhudia ni viongozi mbalimbali wa Serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akionesha ufunguo ya mfano kuashirikia uzinduzi wa Ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya Tanzanite, Mirerani. Wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Alexander Mnyeti.
Jiwe la Msingi lililowekwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli  kushoto akiteta jambo la Mzee Jumanne Ngoma (katikati) aliyevumbua Madini ya Tanzanite mwaka 1967. Kulia ni Mke wa Rais Magufuli, Mama Janeth Magufuli.

No comments:

Post a Comment