Tuesday, April 17, 2018

Ujenzi wa ukuta umefanyika kwa ubora-Meja Jenerali Busungu


Na Asteria Muhozya, Mirerani

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Martin Busungu amesema kuwa ujenzi wa ukuta  unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani wenye urefu wa kilomita 24.5, umefanyika kwa ubora na viwango vya juu.

"Vijana wamefanya kazi kwa uzalendo wa hali ya juu na kujitolea. Tumetekeleza kwa ukamilifu weledi na chini ya muda uliopangwa," alisisitiza Meja Jenerali Busungu.

Meja Jenerali Busungu aliyasema hayo wakati wa sherehe za uzinduzi wa ukuta huo uliofanyika tarehe 6 Aprili, 2018, eneo la geti la kuingilia ukuta huo Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara na kuongeza kuwa, ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 5.645,843,163.55.

Meja Jenerali Busungu aliongeza kuwa, matokeo ya ujenzi huo kuwa na ubora na kuchukua kipindi kifupi yalitokana na uadilifu mkubwa wa jeshi na hilo linaonesha kuwa, kazi ya Jeshi si  tu kulinda mipaka, Katiba ya nchi  bali pia kujenga nchi ya Tanzania na kuhakikisha kuwa, rasilimali za zinakuwa salama kwa vizazi vijavyo.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi na wenyeji wa mji wa Mirerani kwa kutoa historia ya eneo hilo ikiwemo mapitio ya maji na njia za wanyama jambo ambalo liliwezesha jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Pia, alisema kuwa, ukuta huo ulijengwa na vikosi 20 vya jeshi vikijumuisha wataalam wa ujenzi, Wahandisi, Vijana wa JKT wa Operesheni Kikwete na Operesheni Magufuli na Watumishi wa umma.


Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Martin   Busungu akiongea jambo wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Ukuta kuzunguka migodi ya tanzanite Mirerani
Vijana wa JKT wakiendelea na ujenzi wakati wa hatua mbalimbali za ujenzi wa ukuta kuzunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani.

Vijana wa JKT wakiendelea na ujenzi wakati wa hatua mbalimbali za ujenzi wa ukuta kuzunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani.

No comments:

Post a Comment