Tuesday, April 17, 2018

Taifa limeweka historia - Mkuu wa Majeshi


Na Asteria Muhozya, Mirerani

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo amesema  ujenzi wa ukuta wa Mirerani umeweka Historia ambayo itadumu kwa miongo mingi.

Jenerali Mabeyo aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wakati wa sherehe ya Uzinduzi wa ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite Mirerani uliofanyika tarehe 6 Aprili,2018.

Alisema kuwa, utayari wa Jeshi na vijana wa JKT umeonesha taaluma zote  huku vijana 2,038 waliojenga ukuta huo wakiwa alama ya uzalendo kwa Taifa la Tanzania.

Jenerali Mabeyo aliongeza uwezo wa jeshi wa kutumia wataalam wake wa ndani na kufanya kazi kwa moyo kumepelekea mafanikio ya ujenzi wa ukuta huo  na hivyo, kuwataka watanzania wote kujivunia nchi yao, kulinda rasilimali zote za nchi ikiwemo madini na amani ya taifa.

Pia, alisema kuwa, nidhamu ya jeshi imezingatia weledi, uharaka jambo ambalo limepelekea shughuli hiyo kufanyika kwa kipindi kifupi.
" Daima tuko imara kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na utu wetu ndiyo nguzo kubwa,"alisema Jenerali Mabeyo.

Jenerali Mabeyo alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Mirerani kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Jeshi hilo kwa kipindi chote cha ujenzi wa ukuta huo na kueleza kuwa, ushirikiano huo umeoneshwa na watanzania wapenda maendeleo.

Alisema kuwa, ukuta huo umejengwa na wahandisi wa ujenzi kutoka JKT, JWTZ wakiwemo Maafisa 34, Askari 287 na Vijana 2,038 wa Operesheni Kikwete na Opereshi Magufuli.

"Mheshimiwa Rais inawezekana  kuna watu wakaona kuwa shilingi bilioni 5.645,843,163.55 ni nyingi sana lakini baada ya rasilimali hizi kutumika kikamilifu  huenda fedha hizi zikawa kidogo. Hii ndiyo nguvu kazi ya Watanzania na uwezo wa Jeshi letu," alisema Jenerali Mabeyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa  Dkt. Hussein Mwinyi, alisema kuwa  ujenzi wa ukuta huo unadhihirisha ulinzi wa rasilimali za nchi na kuwa umeweka historia mpya.

Dkt.Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Mirerani kuwapokea vizuri wanajeshi  na pia kuwashukuru vijana wa JKT kwa namna walivyojituma na hatimaye kufanikisha ujenzi huo.

Pia,  Waziri  Dkt. Mwinyi alisema kuwa, jeshi litaendelea kuwa imara  na makini katika kutekeleza maagizo na majukumu yake wakati wote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akipokea hati ya ukuta kutoka kwa Waziri wa Ulinzi Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza jambo wakati wa Sherehe ya Uzinduzi wa ukuta kuzunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza jambo wakati wa Sherehe ya Uzinduzi wa ukuta kuzunguka Migodi ya Tanzanite, Mirerani.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo akizungumza jambo wakati wa Sherehe za uzinduzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite, Mirerani.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Martin Busungu (kulia) wakati wa sherehe ya uzinduzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa Tanzanite, Mirerani.

No comments:

Post a Comment