Na Greyson Mwase, Dar
es Salaam
Leo tarehe 30 Aprili,
2018 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua ripoti ya Nane ya ulinganishi
wa mapato ya Serikali na malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia kwa
mwaka wa fedha 2015/16 iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Uhamasishaji Uwazi
katika Mapato ya Madini, Gesi Asilia na Mafuta Tanzania (TEITI) kwa kushirikiana na Mtaalam Mwelekezi, Boas &
Associates na MM Attoneys.
Akizungumza katika
uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha wawakilishi kutoka Kamati
ya TEITI, Wizara ya Madini, makampuni ya mafuta na gesi, Waziri Kairuki
amepongeza Kamati ya TEITI na
Sekretarieti kwa mchango wake katika uandaaji
wa ripoti hiyo.
Mbali na Pongezi hizo, Kairuki ameiagiza Kamati
ya TEITI kuongeza nguvu katika
kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa mpana wa umuhimu na wajibu wa TEITI
kwa kutumia mbinu mbalimbali
ikiwa ni pamoja na warsha mbalimbali pamoja na vipindi vya redio na televisheni.
Amesisitiza kuwa, kipaumbele kiwekwe kwenye maeneo yaliyozungukwa na shughuli za utafutaji na
uzalishaji wa madini, mafuta na gesi asilia na kupata taarifa ndani ya kipindi
cha miezi miwili.
Awali akielezea
ripoti hiyo, Kairuki amesema kuwa ripoti
hiyo inahusu tathmini ya mapato ya madini katika kipindi cha
kuanzia tarehe 1 Julai, 2015 hadi tarehe 30 Juni, 2016 na kufafanua kuwa jumla
ya shilingi 434,627,874,380 zilipokelewa serikalini kutoka kwenye kampuni 55 za madini, mafuta na
gesi asilia zilizoshiriki zoezi la
ulinganishi.
Hata hiyo amesema
taarifa inaonesha kuwa kampuni zililipa kiasi cha shilingi 465,164,747,725 za
kitanzania serikalini na kusababisha tofauti kati ya malipo kuwa ni pungufu ya
shilingi 30,536,873,345 za kitanzania chini ya kiasi ambacho Serikali imekiri
kupokea.
“ Ni lazima tufahamu ni
vipi imejitokeza tofauti hii na ninachukua fursa hii kuelekeza taarifa hii
kupelekwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kwa ajiili ya uchunguzi
kama kifungu 18(1) cha Sheria ya TEITI ya mwaka 2015 kinavyotaka,”
alisema Waziri Kairuki.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amefafanua kuwa ripoti imeonesha
kuwa sekta ya madini imechangia
zaidi kwa asilimia 85 na sekta ya mafuta
na gesi ikionyesha kuchangia asilimia 15 ya mapato ya Serikali chini ya Sekta
ya Madini kwa mwaka 2015/16.
Akielezea mafanikio ya
Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya madini, Kairuki amesema kuwa ili
kuhakikisha madini yanakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi, Serikali
imeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya Sheria
ya Madini pamoja na kanuni zake.
Ametaja hatua
nyingine ambayo ni endelevu kuwa ni kufanya tathmini ya jinsi gani nchi inapata mapato yake kwenye sekta ya madini
kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa.
Ameendelea kusema
kuwa jukumu linafanywa na taasisi mbalimbali
za Serikali lakini TEITI nayo inatekeleza jukumu husika kwa kuhakikisha
taarifa za mapato ya madini zinatolewa kwa uwazi kwa wananchi na wadau
mbalimbali katika Serikali, Sekta
Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Katika hatua nyingine
Waziri Kairuki amezitaka kampuni nyingine ambazo hazikushiriki katika kipindi
cha ukaguzi kujitokeza katika ukaguzi unaofuata ili takwimu
halisi za mapato zifahamike.
Aidha, ametumia fursa
hiyo kukaribisha kampuni nyingine zenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya madini
kujitokeza kwa wingi ili sekta ya madini
iwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Wakati huo huo
akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa
Simon Msanjila amesema kuwa mara baada ya ripoti kuzinduliwa na kukabidhiwa kwa
Kamati ya TEITI hatua inayofuatia ni kamati ya TEITI kuwasilisha ripoti hiyo
kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili achukue hatua kwenye hoja
zilizotokana na ripoti hiyo.
No comments:
Post a Comment