Na
Asteria Muhozya, Dodoma
Serikali
kupitia Wizara ya Madini inakamilisha taratibu za utoaji wa Leseni kwa Migodi Mikubwa
ambazo hazijawahi kutolewa nchini, huku migodi hiyo ikitarajiwa kuanzishwa hivi
karibuni.
Hayo
yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila
alipokutana na viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi ofisini
kwake, jijini Dodoma.
Viongozi hao
walikutana na Prof. Msanjila Februari 26, kwa lengo la kujitambulisha, kuelewa
shughuli za serikali upande wa sekta ya madini, kupata uelewa kuhusu mabadiliko
ya Sheria ya Madini na namna pande hizo mbili zinavyoweza kushirikiana katika
kuendeleza sekta husika.
Prof. Msanjila
aliwakaribisha viongozi hao kwenye sekta ya madini huku akiwataka kuzishawishi
kampuni mbalimbali kuwekeza nchini hususani katika shughuli za uongezaji thamani
madini na kueleza kuwa, suala hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo serikali
inayapa kipaumbele ikiwemo ujenzi wa vinu vya kusafisha na kuyeyusha madini.
Akizungumzia
Sheria Mpya ya Madini ya Mwaka 2017, Prof. Msanjila amesema hakuna tatizo lolote
katika utekelezaji wa sheria na kueleza kuwa, serikali kupitia wizara ya madini
inapokea wawekezaji wengi wenye utayari na nia ya kuwekeza nchini huku utekelezaji
wa sheria hiyo ukiwa si kikwazo na kuongeza kwamba, “hakuna mahali ambapo serikali
inatengeneza sheria kwa ajili ya kumkandamiza mfanya biashara”.
“Hakuna tatizo
lolote kwenye sheria ya madini. Hata wageni huwa tunakaa nao tunawaelimisha na
wanatuelewa vizuri. Kama kuna dosari ni
vitu ambavyo tunaweza kuvirekebisha na tayari tumekwishakufanya hivyo kwa
baadhi ya maeneo,” alisema Prof. Msanjila.
Aidha, katika
kikao hicho Prof. Msanjila alitoa ushauri kwa viongozi hao kujitangaza zaidi
kuhusu kazi zao huku akiwataka kutafuta wasaa kwa ajili ya pande hizo mbili kukutana
ili wizara iweze kutoa elimu zaidi kwa Jumuiya hiyo kuhusu sekta ya madini
ikiwemo fursa za uwekezaji zilizopo.
Pia, Prof.
Msanjila alisema kuwa suala la kuaminiana linaweza kujengwa huku akiwataka
watanzania kuwa wazalendo na namna wanavyotumia fedha za umma. Prof. Msanjila
alizungumzia jambo hilo baada ya mmoja wa viongozi hao kueleza kuwa, bado kuna
hali ya kutokuaminiana baina ya serikali na taasisi binafsi.
Kwa upande
wake, mmoja wa viongozi wa jumuiya hiyo, Francis Nanai ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Mwananchi Communications Limited amemweleza Prof. Msanjila kuwa, kama
viongozi wa umoja huo, wamezipokea changamoto zilizotolewa kwao na Prof. Msanjila
ikiwemo ushauri wa kukutana na wizara kwa lengo la kupata ufafanuzi na
elimu zaidi kuhusu sekta ya madini.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila (kulia) akizungumza jambo wakati wa kikao
baina yake na Viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi.
Kushoto ni mmoja wa viongozi hao.
Mmoja wa Viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa
Taasisi Binafsi akizungumza jambo katika kikao hicho. Kulia ni Kamishna
Msaidizi wa Wizara ya Madini, Godfrey Nyamrunda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon
Msanjila wakijadiliana jambo na baadhi
Viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi.
Mmoja wa viongozi wa jumuiya Jumuiya ya Watendaji
Wakuu wa Taasisi Binafsi, Francis Nanai ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Mwananchi Communications Limited, akizungumza jambo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon
Msanjila katika picha ya pamoja na Viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu
wa Taasisi Binafsi.
No comments:
Post a Comment