Na Greyson Mwase,
Pwani
Mwenyekiti wa Tume ya
Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa madini ya ujenzi
aina ya kokoto katika mkoa wa Pwani kuwa na Mpango wa Ufungaji Mgodi
utakaotumika kama mwongozo wa kuhakikisha mazingira yanaachwa yakiwa katika
hali salama mara baada ya kumalizika kwa shughuli za uchimbaji wa madini hayo.
Profesa Kikula
aliyasema hayo leo tarehe 21 Februari, 2019 katika nyakati tofauti alipofanya
ziara yake katika migodi
inayojishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi aina ya
kokoto iliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani yenye lengo la kutembelea
wachimbaji wa madini hayo pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Profesa Kikula katika
ziara hiyo akiwa ameambatana na Kamishna - Tume ya Madini, Dkt. Athanas
Macheyeki, wataalam kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma, Ofisi
ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ofisi ya Afisa Migodi Mkazi wa
Lugoba pamoja na waandishi wa habari, Profesa Kikula alitembelea migodi ya
Sisti Mganga, Gulf Concrete Company Limited na
Yaate Company Limited iliyopo katika Wilaya ya Bagamoyo.
Akizungumza katika
nyakati tofauti mara baada ya kutembelea migodi hiyo, Profesa Kikula aliwataka
wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mipango ya ufungaji migodi mapema
badala ya kusubiri mpaka shughuli za uchimbaji madini zinapomalizika hivyo
kufanya zoezi la ufungaji wa migodi kuwa gumu huku wakiacha mazingira yakiwa
hatarishi.
“Ninapenda
kuwakumbusha kuwa suala la kuwa na Mpango wa Ufungaji wa Migodi ni la lazima
kulingana na Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake, hivyo ninawataka
kuhakikisha mnakuwa na mpango ili kuhakikisha mashimo hayaachwi wazi,” alisema Profesa
Kikula.
Awali akiwa katika
mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga Profesa Kikula alielezwa mafanikio ya mgodi huo ikiwa ni
pamoja na kokoto za mgodi huo kutumika
katika ujenzi wa daraja la Mto Wami uliopo mkoani Pwani, reli ya kisasa ya standard gauge na
utengenezaji wa marumaru kwa ajili ya soko la ndani ya nchi.
Katika hatua nyingine
Mganga alitaja changamoto zinazoukumba mgodi huo kuwa ni pamoja na tozo kubwa
kutoka katika halmashauri na tozo nyingine zinazotozwa na kijiji cha
Kihangaiko pasipo kuwa na risiti pamoja
na ukosefu wa vifaa vya kisasa.
Profesa Kikula
alisema kuwa, suala la tozo litafanyiwa kazi kwa kuliwasilisha mamlaka za juu
kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kusisitiza kuwa nia ya Serikali kupitia Tume ya
Madini, ni kuhakikisha wachimbaji wa madini hususan wadogo wanafanya kazi
katika mazingira mazuri yenye faida kubwa huku wakilipa kodi mbalimbali
Serikalini pasipo vikwazo vyovyote.
Wakati huo huo, akiwa
katika mgodi wa uzalishaji wa kokoto wa Gulf
Concrete Limited Profesa Kikula alitoa mwezi mmoja kwa uongozi wa mgodi
huo kuhakikisha wanarekebisha kasoro ya mazingira kwa kuhakikisha vumbi
linalotoka wakati wa shughuli za uchimbaji wa kokoto halisambai kwani
linaathiri wananchi wa vijiji vya jirani
katika mgodi huo.
Alisema ni vyema
wakazingatia Sheria ya Mazingira kwani vumbi mbali na kuathiri wananchi
wanaoishi katika vijiji vya jirani linaweza kuathiri wafanyakazi wa mgodi huo.
Aidha, alituaka mgodi
huo kuendelea kuhakikisha unatoa huduma kwa jamii inayozunguka mgodi huo na kutumia
huduma za ndani ya nchi kama vile bidhaa pamoja na ajira kwa wazawa.
Katika hatua
nyingine, Profesa Kikula akiwa katika mgodi wa kuzalisha kokoto wa Yaate Co.
Limited, mbali na kuupongeza mgodi kwa kuaminiwa na kupewa kazi ya kusambaza
kokoto kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya standard gauge unaotelekezwa
na kampuni ya Yapi Merkezi na kutoa
huduma mbalimbali kwa jamii inayouzunguka mgodi huo pamoja na ajira, aliutaka
mgodi huo kuendelea kununua bidhaa/huduma kutoka kwa wananchi.
“Kutoa huduma bora
kwa wananchi wanaozunguka mgodi kunaboresha mahusiano na kupunguza migogoro ya
mara kwa mara inayoweza kujitokeza.
Awali akielezea
mafanikio ya mgodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Yaate Co. Limited, Eugen Mikongoti
alisema mradi umenufaisha watanzania wengi
kwa kuchangia maendeleo ikiwa ni pamoja na ulipaji wa zaidi ya shilingi bilioni 1.31 ambazo
zimelipwa kama ushuru wa madini kati ya
kipindi cha mwezi Juni, 2018 hadi Januari, 2019 na shilingi milioni 338.8
zilizolipwa kama mrabaha.
Alieleza mafanikio
mengine kuwa ni pamoja na utoaji wa fursa za ajira kwa watanzania hususan
vijana wanaozunguka mgodi na kuziwezesha kampuni zinazomilikiwa na wazawa
kushiriki katika miradi mikubwa hivyo
kuzijengea uwezo wa kitaalam na kupata fursa.
Mikongoti alitaja mafanikio
mengine kuwa ni pamoja na kuwezesha maendeleo ya wanachi wanoishi karibu na
mgodi kupitia huduma za jamii ambapo mpaka
sasa mgodi huo unaendelea na
ujenzi wa nyumba za watumishi na kuhudumia wananchi katika zahanati iliyopo
mgodini.
Katika hatua nyingine
Mikongoti alipongeza kazi kubwa zinazofanywa na Tume ya Madini chini ya
Mwenyekiti wake Profesa Kikula ikiwa ni pamoja na kuwatembelea, kuwapa elimu na
kutatua changamoto mbalimbali.
Mwenyekiti wa Tume ya
Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) pamoja na Kamishna-Tume ya Madini, Dkt.
Athanas Macheyeki (katikati) wakiangalia moja ya bidhaa zinazotengenezwa na
mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga uliopo katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani
Pwani tarehe 21 Februari, 2019 ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo
yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya kokoto, kusikiliza na
kutatua kero za wachimbaji. Kushoto ni mmiliki wa mgodi huo, Sisti Mganga.
Mmoja wa watendaji wa
mgodi wa kuzalisha kokoto wa Gulf Concrete Company Limited, ulipo katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani,
Ramesh Annlahamadu (kushoto) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula (katikati) mara alipofanya ziara kwenye mgodi huo ikiwa ni
sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za
uchimbaji wa madini ya kokoto, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji tarehe
21 Februari, 2019. Kulia mbele ni Kamishna – Tume ya Madini, Dkt. Athanas
Macheyeki.
No comments:
Post a Comment