Na Nuru Mwasampeta,
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini, Prof. Simon Msanjila ameongoza kikao kilicholenga kupokea maoni juu
rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini.
Kikao hicho
kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa wizara kimewakutanisha, Makamishna
Wasaidizi wa Wizara, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA)
John Bina, viongozi wa shirikisho hilo pamoja na wawakilishi wa wachimbaji
wadogo kutoka mikoa ya kimadini nchini.
Akizungumza wakati wa
Ufunguzi wa kikao, Prof. Msanjila alisema maoni ya wajumbe hao ni muhimu kwa
watanzania na taifa kwa ujumla katika kuboresha kanuni hizo.
Aidha, Msanjila
amebainisha kuwa, wadau wengine wamekwisha kutoa maoni yao katika makundi
tofauti tofauti na pia maoni mengine yanaendelea kupokelewa kwa njia ya
maandishi na kuwataka maoni hayo yakamilishwe ndani ya kipindi cha wiki moja.
Kabla ya kupokea
maoni hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara, Edwin Igenge aliwasilisha
rasimu ya kanuni hizo ili kutoa uelewa wa kile wanachopaswa kuchangia katika
kutoa maoni yao.
Akiwasilisha rasimu
hiyo, Igenge alisema hii ni sheria ndogo inayotokana na sheria mama ya madini. “Kanuni
hizo zinatungwa kwa mujibu wa kifungu cha 27 (C) kifungu kidogo cha pili pamoja
na kifungu cha 129 cha sheria ya madini,” amesema Igenge.
Aidha, amesema mahala
patakapo kuwa na soko la madini kutakuwa na huduma zote zinazotakiwa ili
kurahisisha ubadilishwaji wa fedha na madini kama vile mabenki, ofisi za mamlaka ya
Mapato (TRA), ofisi za masuala ya ulinzi na usalama, pamoja na ofisi mbalimbali
za serikali.
Igenge amesema baada
ya kukamilika na kupitishwa kwa kanuni hizo zitatafsiriwa na kupatikana katika
lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wote kuelewa kanuni na mwongozo wa
masoko ya madini.
Akizungumzia baadhi
ya vipengele vilivyopo katika rasimu hiyo, Igenge alisema sehemu ya kwanza
inahusika na utangulizi yenye vifungu 3 cha kwanza ni jina la kanuni ambapo
litaitwa ‘Kanuni za masoko za mwaka 2019’, pili ni maelezo ya wapi kanuni hizo
zitatumika na kuratibiwa na kipengele cha mwisho kitatoa tafsiri ya maneno
mbalimbali yanayotumika ndani ya kanuni hizo.
Sehemu ya pili ya
kanuni inahusika na uanzishwaji wa masoko yenyewe, ambapo masoko yataanzishwa
katika maeneo yenye tawala za mikoa na kuipa maelekezo Tume ya Madini
kuhakikisha wanashirikiana na tawala za mikoa katika kuanzisha masoko hayo.
Aidha, alielezea msingi
wa kwanza ni msingi wa uwazi, msingi wa matangazo ili watu waweze kujua madini yanauzwa
na kununuliwa wapi, msingi wa haki ambao utazuia manunuzi haramu ya madini,
lakini pia msingi wa mwendelezo ikiwa na maana masoko hayo kuwa ni masoko ya
kudumu na si ya msimu.
Kwa upande wake, Rais
wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameiomba
serikali kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wawakilishi wa wachimbaji wadogo
ili kupata kitu kitakachokubalika na jamii nzima ya wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini.
Aidha, alikiri
kufurahishwa na ufafanuzi uliotolewa katika kila kipengele cha rasimu ya kanuni
za uanzishwaji wa masoko ya madini na kukiri kwamba wanaamini kuwa serikali ina
nia njema na wananchi wake.
Wajumbe wa mkutano wa kutoa na kupokea maoni juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini wakifuatilia mada. |
Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara, Edwin Igenge akiwasilisha rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini. |
Katibu Mkuu wa
Madini, Prof Simom Msanjila mbele (mwenye koti jeusi) akiongoza kikao cha kupokea
maoni juu ya rasimu ya uanzishwaji wa kanuni za masoko ya madini nchini.
|
No comments:
Post a Comment