Na
Issa Mtuwa, Dodoma
Serikali kupitia
Wizara ya Madini imesema bado imeshikilia msimamo wake kuhusu muda uliotolewa kwa
Mgodi wa North Mara kutekeleza maagizo ya serikali yaliyotolewa kwenye kikao
cha Januari 9, 2019 kuhusu Bwawa la kuhifadhi topesumu (Tailings Storage Facility -TSF).
Hayo yamesemwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila Februari 26, 2019
wakati akizungumza katika mahojiano maalum ofisini kwake Jijini Dodoma, mara
baada ya kufungua kikao cha pamoja baina ya wajumbe kutoka serikalini na
wajumbe kutoka Mgodi wa North Mara waliokutana kujadili kuhusu hatua zilizofikwa
na Mgodi katika kutekeleza maagizo hayo.
Amesema serikali
haitoongeza muda zaidi ya ule uliotolewa katika kikao cha awali, na kusema kuwa
msimamo wa serikali utabaki kuwa hivyo.
“Ndugu zangu katika kikao hiki kilenge kutoa
majibu ya utekelezaji wa maagizo ya serikali kama yalivyowasilishwa kwenye
kikao cha Januari 9, 2019, ni kwa kiasi gani mmetekeleza maagizo hayo,” alisema
Prof. Msanjila.
Serikali kupitia
kikao chake cha Januari 9, 2019 chini ya Makatibu Wakuu wa wizara saba (Madini,
Makamu wa Rais Mazingira (NEMC), Ardhi, TAMISEMI, Afya, Fedha na Maji) kilitoa
maagizo mbalimbali yakiwemo: Kujenga TFS
mpya na Kukarabati TFS iliyopo kwa
aajili ya kudhibiti mtiririko wa topesumu, maagizo ambayo mgodi ulipewa
kuyatekeleza kwa muda wa miezi Nane (8) kuanzia Januari 9, 2019.
Akiongoza wakati wa
mjadala wa uwasilishaji wa mada mbalimbali wa kikao hicho, chini ya Mwenyekiti
wa kikao hicho Prof. Hudson Nkotaga aliwataka North Mara kueleza namna gani
wametekeleza maagizo ya serikali kwa lengo la kupata mrejesho wa utekelezaji.
Kuhusu utekelezaji wa
maagizo hayo, Meneja Usalama, Afya na Mazingira Reuben Ngusaru, kutoka mgodi wa
North Mara amesema mgodi umeanza kutekeleza maagizo hayo na bado wanaendelea
kutekeleza maagizo hayo na hata kikao cha tarehe 26 Februari ikiwa ni moja
mkakati wa kutekeleza maagizo hayo kwa ufanisi.
Akizungumzia kuhusu
hatua zilizochukuliwa na mgodi kudhibiti uvujaji unaoendelea kwenye (TSF)
mpaka kufikia siku ya kikao cha Februari 26, mambo yaliyotekelezwa ni
pamoja na: Kuondoa mawe na kusafisha mtaro uliopo upande wa Kaskazini mwa TSF. Kuvukiza (evaporation) maji yaliyotokana na uchenjuaji wa mawe
yanayotengeneza tindikali asili (PAF Rock) (leachate
water) badala ya kuyapeleka yote kwenye TSF
na Programu zote zilizokuwepo za kupunguza maji katika TSF bado zinaendelea.
Aidha, kuhusu
utekelezaji uliofikiwa katika kutekeleza agizo la Serikali la kujenga TSF mpya (Construction of a new TSF) Reuben
amesema mpaka kufika tarehe 26 Februari, mgodi umefanya utambuzi wa eneo
linalofaa kwa ajili ya ujenzi wa TSF mpya (Site
Identification) nau sanifu wa awali (Conceptual design) ambapo usanifu wa
awali umefanyika na ujenzi wa TSF mpya
unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani milioni 45 za tope sumu (tailings)
kavu kwa kadirio la ongezeko la tani 8200 kwa siku.
Maagizo ya serikali
kwa mgodi wa North Mara yalitokana na ukaguzi uliofanywa na serikali kwenye mgodi
huo uliohusisha timu kutoka ofisi mbalimbali za serikali zikiwemo, NEMC, Mkemia
Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini, na Wizara ya Afya, uliopelekea kutolewa kwa
maagizo yaliyolenga kudhibiti uharibifu wa mazingira uliokuwa unafanywa na
mgodi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila mwenye tai katikati kushoto akimsikiliza mmoja wa wajumbe wa kikao hicho wakati akichangia. |
No comments:
Post a Comment