Na Greyson Mwase,
Kilwa
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo ameitaka Tume ya Madini kufanya uchunguzi kuhusu
mgogoro kati ya kampuni inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya jasi ya
Kizimbani inayomilikiwa na Seleman Mohamed na wananchi wa kijiji cha Hotel Tatu
kilichopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi.
Naibu Waziri Nyongo
ametoa agizo hilo leo tarehe 15 Desemba, 2018 katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika kijiji hicho wakati wa utatuzi wa mgogoro huo ikiwa ni
sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Lindi yenye lengo la kukagua
shughuli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Alisema kuwa, baada
ya kusikiliza pande zote mbili imeonekana kuna haja ya Tume ya Madini kufanya uchunguzi ili kubaini
namna utoaji wa leseni ya uchimbaji wa madini ya jasi kwa kampuni ya Kizimbani
ulivyofanyika kabla ya kufanya maamuzi kwa mujibu wa sheria na kanuni za
madini.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri Nyongo alisisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini
haitasita kuwaondoa maafisa madini wakazi wa mikoa watakaobainika kuwa ndio
chanzo cha migogoro kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini.
“Kama Serikali
tunataka kuhakikisha leseni za utafiti na uchimbaji wa madini zinatolewa kwa
kufuata sheria na kanuni za madini bila kuwepo kwa migogoro ya aina yoyote,
aidha hatutasita kumwondoa afisa madini mkazi yeyote atakayebainika kuwa chanzo
cha migogoro kwenye shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini,” alisema Naibu
Waziri Nyongo huku akishangiliwa na wananchi.
Awali wakielezea
mgogoro huo kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa walikuwa na mgogoro
wa muda mrefu kati yao na Seleman Mohamed aliyedai kuwa mmiliki halali wa eneo
husika hali iliyopelekea mgogoro kuwasilishwa kwenye Ofisi ya Madini Mtwara,
ambapo mtaalam kutoka ofisi hiyo alifika
kwa ajili ya kuchukua alama za eneo husika kwa ajili ya kwenda kuhakiki umiliki
wa eneo husika.
Waliendelea kusema
kuwa, walifika katika Ofisi hiyo baada ya siku mbili na kuelezwa kuwa eneo hilo
lilishaombewa leseni na kutolewa kwa mmiliki wa kampuni ya Kizimbani, Seleman
Mohamed.
Walisema kuwa tangu
kuzuka kwa mgogoro huo mwaka 2013, wamekwenda katika ngazi mbalimbali kuanzia
ngazi ya Wilaya hadi Mkoa pasipo mafanikio yoyote na kusisitiza kuwa wanahitaji
eneo hilo kwa ajili ya uwekezaji kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ya jasi
kwa kutumia mwekezaji na kujipatia
kipato pamoja na kulipa kodi Serikalini.
Kwa upande wake
mmiliki wa leseni hiyo, Seleman Mohamed alidai kuwa aliomba leseni kwa kufuata
sheria na kanuni za madini na kupatiwa leseni yake.
Wakati huo huo
akizungumza katika nyakati tofauti kupitia mikutano na wazalishaji wa chumvi
iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi na katika eneo la Kilwa
Masoko Wilayani Kilwa mkoani Lindi, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, Serikali
kupitia Wizara ya Madini inatambua mchango wa wazalishaji wa chumvi hususan
katika mkoa wa Lindi kwenye Sekta ya Madini hivyo imeweka mikakati mbalimbali
ya kuwasaidia.
Alieleza mikakati
hiyo kuwa ni pamoja na kuondoa tozo mbalimbali tisa kisheria zilizokuwa
zinatozwa na halmashauri ili uzalishaji wao uwe na tija na kuinua uchumi wa
mkoa wa Lindi.
Alieleza kuwa
mikakati mingine kuwa, ni pamoja na kuendelea kushughulikia changamoto zilizopo
kwenye uzalishaji chumvi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha
chumvi katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi mara baada ya kupata eneo na fedha
kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini.
(SMMRP) uliopo chini ya Wizara ya Madini.
Aliendelea kusema
kuwa mahitaji ya chumvi nchini ni takribani tani laki tatu na nusu kwa mwaka
ambapo asilimia 70 ya chumvi inaagizwa kutoka nje ya nchi na kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya
Madini imejipanga katika uboreshaji wa uzalishaji wa chumvi nchini.
“Kama Wizara ya
Madini tunataka ifike mahali tuzalishe chumvi bora ya kutosha na kuuza ya ziada
nje ya nchi na kujiingizia fedha za kigeni,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Katika hatua nyingine
Naibu Waziri Nyongo aliwataka wazalishaji wa chumvi hao kufuata sheria na
kanuni za madini.
Wakizungumza katika
nyakati tofauti wazalishaji wa chumvi mkoani Lindi waliwasilisha changamoto
mbalimbali ikiwa ni pamoja na tozo zilizoondolewa kisheria kwenye madini ya
chumvi kuendelea kutozwa na halmashauri, ukosefu wa mitaji pamoja na masoko.
Changamoto nyingine
ni pamoja na miundombinu duni kwenye maeneo yenye uzalishaji wa chumvi, madini
joto yanayotumika kwenye uzalishaji wa chumvi kuuzwa kwa gharama kubwa na
kutotambuliwa katika halmashauri na taasisi
nyingine za kifedha.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiangalia madini ya chumvi katika eneo la
Jangwani kwa Chinja lililopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi.
|
No comments:
Post a Comment