Tuesday, December 18, 2018

Mgodi wa Wachimbaji Wadogo Mahenge Wafunguliwa


Ø Ni baada ya kufungwa kwa miezi Mitano
Ø Biteko azidua Ofisi ya Madini Ulanga

Na Rhoda James, Mahenge

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameufungua mgodi wa Wachimbaji Wadogo wa Mahenge baada ya kufungwa kwa takribani miezi Mitano tangu   Julai 10, 2018.

Mgodi huo wa madini ya Vito aina ya Spino uliopo Wilayani Ulanga ulisimamishwa kutokana na kukiukwa kwa taratibu za uchimbaji wa madini ikiwemo  kutolipa kodi za Serikali.

Akizungumza katika mkutano kati yake na wachimbaji Biteko alisema kuwa, Sekta ya Madini haipo kwa ajili ya kufunga migodi, na kuongeza kuwa, hakuna mchimbaji yeyote atakayeruhusiwa kuchimba katika eneo hilo hadi pale atakapokuwa amelipa madeni yake angalau ya awamu ya kwanza.

Pia, alisema kuwa, ikiwa kuna mchimbaji ambaye atakiuka taratibu za uchimbaji, atachukuliwa hatua za kisheria  na si kwa kufungiwa mgodi tu bali atapelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

 “Nyie ni wadau muhimu katika sekta ya maendeleo, na mkilipa kodi, ikaonekana imefanya nini, hata wawekezaji hawatakwepa kulipa kodi,” alisema Biteko.

Aliwataka Wachimbaji Wadogo wa Mahenge kubadilika na kufuata taratibu zilizowekwa kisheria na kusema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano haitaki rushwa hususan kwenye Sekta ya Madini.

Aidha, pamoja na kufuungua mgodi huo, Biteko pia alizidua Ofisi ya Afisa  Madini Mkazi wa Mahenge, ikiwa ni mojawapo ya mahitaji ya awali ili shughuli za uchimbaji madini katika Mji wa Mahenge ziende  kama inavyotakiwa.

Pia, Biteko alimtaka Afisa Mkazi wa Mahenge, Tandu Jirabi kuhakikisha leseni za dealers zinasainiwa ili  pamoja na kutoa utaratibu kwa wadau hao kuhusu namna ambavyo wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kabla ya  kupatiwa leseni.

“Mzawa lazima awe na mashinetano na mwekezaji kuwa na mashine 30,” alisema Biteko.

Aidha, Biteko alitoa wito kwa viongozi wa Halmashauri ya Mahenge kuhakikisha kuwa fedha zinazolipwa kama kodi zinatumika ipasavyo katika kuwezesha huduma mbalimbali za jamii ikiwemo kujenga Zahanati, Shule, Barabara na kadhalika.

Kwa Upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mahenge Goodluck Mlinga alimshukuru Naibu Waziri Biteko kwa kufugua mgodi huo wa wachimbaji wadogo na kuwataka wananchi wa Mahenge kufuata taratibu zinazotakiwa ili kuepusha usubufu kama huo uliojitokeza hapo awali.

Mlinga alisisitiza kuwa, kodi inayolipwa na Wachimbaji Wadogo lazima itekeleze majukumu yaliyopangwa na kumwakikishia Naibu Waziri kuwa wachimbaji watalipa kodi kwa kishindo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya alisema kuwa Rais Magufuli anataka kila mwananchi afaidike na rasilimali za madini, hivyo, kuwataka wananchi na Wachimbaji wote wa Mahenge  kufuata taratibu zilizopo ili kila mmoja wao afaidike na rasilimali hiyo.


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja baada ya kuzidua Ofisi ya Madini Wilayani Ulanga katika Mji wa Mahenge uliofanyika tarehe 14 Desemba, 2018. Kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo la Mahenge Goodluck Mlinga na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akikata utepe kuashiria uziduzi wa Ofisi ya Madini Wilayani Ulanga katika Mji wa Mahenge uliofanyika tarehe 14 Desemba, 2018. 

Mbunge wa Jimbo la Mahenge Goodluck Mlinga akiwahutubia wananchi pamoja na wachimbaji wadogo wa madini (hawapo pichani) wilayani Ulanga katika mji wa Mahenge, wakati wa ziara ya Naibu Waziri Biteko. 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akimtambulisha Afisa Mkazi mpya wa Madini wa Mahenge kwa wananchi (hawapo pichani) baada ya kuzidua Ofisi ya Madini ya Mahenge tarehe 14 Desemba, 2018. 

Wananchi wa Mahenge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) wakati alipofanya mkutano wa hadhara katika mji wa Mahenge wilayani Ulanga. 

Wananchi wa Mahenge wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) wakati alipofanya mkutano wa hadhara katika mji wa Mahenge wilayani Ulanga. 

Kamshina wa Madini, Dk. Athenes Macheyeki akitia saini katika kitabu cha Afisa Mkazi wa Madini Mahenge baada ya kuziduliwa kwa Ofisi hiyo tarehe 14 Desemba, 2018. Wanaoshuhudia ni Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko aliyekaa na Mbunge wa Jimbo la Mahenge, Goodluck Mlinga kulia.

No comments:

Post a Comment