Tuesday, December 18, 2018

Prof. Msanjila akutana na ujumbe wa Serikali ya India

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amekutana na Ujumbe   wa Serikali kutoka nchini India pamoja na Kampuni ya National India Development Corporation (NMDC) jijini Dodoma, katika kikao ambacho pia kimeshirikisha watendaji kutoka Wizarani, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Tume ya Madini.

Ujumbe huo umefika wizarani kwa lengo la kuonana na uongozi wa Wizara kwa ajili ya kufanya majadiliano juu ya nia yao ya kufanya uwekezaji kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kupata maeneo mapya ya uchimbaji. Awali kampuni hiyo ilikutana na Shirika la STAMICO na kufanya majadiliano kuona ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana katika utekelezaji wa malengo yao kupitia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya madini nchini.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Desemba 18, Katibu Mkuu Prof. Msanjila amewakaribisha na kuwapongeza kwa nia yao ya kufanya uwekezaji nchini na kuueleza ujumbe huo kuwa, kampuni ya NMDC inayo fursa ya kuchagua kuwekeza ikiwa kama kampuni inayojitegemea ama kwa kuingia ubia na Shirika la Madini la Taifa la (STAMICO).

Aidha, ameuleza ujumbe huo kuwa, wizara inazo taasisi ambazo zinasimamia masuala yanayohusu leseni na shughuli za utafiti na kuusisitiza kujadiliana na Kamishna wa Madini, Mkurugenzi wa Sheria na Tume ya Madini kwa ajili ya kupata taratibu zinazotakiwa kisheria kuhusu masuala ya leseni na mahitaji mengine wanayotakiwa kutekeleza kabla ya kuwasilisha mpango huo kwenye ofisi yake. Aidha, aliutaka ujumbe huo kujadiliana na GST kwa masuala yanayohusu shughuli za utafiti wa madini.

Pia, Prof. Msanjila ameishauri kampuni husika kukata leseni ya utafiti kwanza ili kufanya utafiti katika maeneo waliyoyakatia leseni na kuwasilisha taarifa hizo katika ofisi ya GST ndipo waendelee na utaratibu wa kupata leseni ya uchimbaji. Vilevile, ameutaka ujumbe huo kuwa tayari kuwasiliana na wizara pindi unapohitaji kupata ufafanuzi wa masuala yote ya yanayohusu uwekezaji katika sekta husika.


Kampuni ya NMDC inajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa
 madini ya chuma na iko chini ya Wizara inayoshughulikia madini ya 
chuma ya India.  Pia kampuni hiyo pia inajishughulisha na utafiti wa 
madini mbalimbali kama vile madini ya chuma, shaba, phosphate, nk.
katika nchi mbalimbali na barani Afrika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akieleza jambo katika kikao kati yake na ujumbe wa Serikali ya India na Kampuni ya National India Development Corporation  (NMDC)

Sehemu ya ujumbe kutoka Serikali ya India na Kampuni ya NMDC pamoja na watendaji wa wizara wakifuatilia kikao hicho.

Sehemu ya Watendaji kutoka Tume ya Madini, Taasisi na Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia kikao hicho.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akiongoza kikao baia yake na ujumbe kutoka Serikali ya India kilichoshirikisha pia Watendaji kutoka Wizarani, Tume ya Madini na GST.

No comments:

Post a Comment