Na Greyson Mwase,
Ruangwa
Wananchi katika
kijiji cha Namungo kilichopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi wameiomba Serikali
kupitia Wizara ya Madini kuwapatia vifaa bora ili kuboresha uchimbaji wa madini na kuchangia kwenye pato
la taifa kupitia Sekta ya Madini.
Wameyasema hayo
leo tarehe 14 Desemba, 2018 katika
mkutano wa hadhara uliofanywa katika kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku mbili ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
mkoani Lindi yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na
kutatua kero mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba
ya wananchi wenzake, Dickson Baltazary ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini ya
dhahabu alisema kuwa, wamekuwa wakichimba madini kwa kutumia zana duni hali
inayowasababishia kushindwa kufikia malengo yao kwenye uzalishaji.
Baltazary aliongeza
kuwa, iwapo watapata fedha kupitia mikopo na ruzuku Serikalini kupitia Wizara
ya Madini wataweza kufanya shughuli zao za uchimbaji wa madini kwa ufanisi na
kuchangia zaidi kwenye mapato ya Serikali.
Akizungumza na
wachimbaji hao mara baada ya kupokea kero mbalimbali, Naibu Waziri Nyongo
alisema kuwa, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Sekta ya
Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia
wachimbaji wadogo ambapo mpaka sasa maeneo yameanza kutengwa kwa ajili ya
uchimbaji madini.
Aliendelea kusema
kuwa Serikali inaangalia utaratibu mzuri utakaowawezesha kupata ruzuku.
Wakati huohuo,
akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nangurugai Wilayani Ruangwa mkoani Lindi
Naibu Waziri Nyongo aliwataka wananchi kuunga mkono uwekezaji wa uchimbaji wa
madini ya kinywe (graphite) unaotarajiwa kufanya na kampuni ya utafiti wa
madini hayo ya Chilalo Graphite Mine.
Aidha, aliwapongeza
wananchi hao kwa kuunga mkono uwekezaji huo kwa kuwa na subira wakati wa
tathmini iliyofanywa miaka miwili iliyopita na kuitaka kampuni ya Chilolo
kurudia tathmini kwani thamani ya mali imebadilika.
Akielezea manufaa ya
mradi huo, Nyongo alieleza kuwa ni pamoja na ajira 480 kutolewa wakati wa
ujenzi wa mgodi na ajira 250 kutolewa mara baada ya uendeshaji wa mgodi kuanza.
Alieleza manufaa
mengine kuwa ni pamoja na kukua kwa uchumi wa Wilaya ya Ruangwa kutokana na ongezeko
la mapato yatokanayo na uzalishaji wa madini hayo.
“Madini ya kinywe
yana soko kubwa duniani kutokana na
kampuni nyingi kutumia madini hayo katika utengenezaji wa betri za magari, ni
vyema mkachangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa
mradi,” alifafanua Nyongo.
Katika hatua
nyingine, Nyongo aliutaka mgodi huo kuhakikisha unatoa ajira kwa wananchi wenye
sifa wanaozunguka karibu na mgodi kabla ya kufikiria kuajiri wageni kutoka
katika mikoa mingine.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akifafanua jambo alipofanya ziara katika
Mgodi wa Dhahabu wa Namungo uliopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku
mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini
pamoja na kutatua kero mbalimbali. Katikati ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Lindi, Sophia Omari.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akipata maelezo kuhusiana na shughuli
zinazofanywa na kampuni
inayojishughulisha na utafiti wa
madini ya Kinywe ya Ngwena Limited iliyopo Wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
Naibu Waziri wa
Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Nangurugai kilichopo Wilayani Ruangwa mkoani
Lindi.
Mmoja wa wachimbaji
wadogo wa madini ya dhahabu katika kijiji cha Namungo Wilayani Ruangwa mkoani
Lindi akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
(hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa Madini,
Stanslaus Nyongo (kulia) akikagua shughuli za uchenjuaji wa madini ya
dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu wa
Namungo uliopo Wilayani Ruangwa mkoani
Lindi.
|
No comments:
Post a Comment