Na Greyson Mwase,
Leo tarehe 26
Novemba, 2018 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amefanya ziara katika machimbo
ya dhahabu ya wachimbaji wadogo yaliyopo
wilayani Mbogwe mkoani Geita lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji
madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali
zinazowakabili wachimbaji wadogo. Katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko
aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi, Mbunge wa Jimbo la
Mbogwe, Augustino Masele, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbogwe, Christopher
Bahali, na Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita,
Christopher Kadeo.
Wengine ni pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel
Mapunda, Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini Mhandisi Frederick Mwanjisi,
Wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini, Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Wilaya ya Mbogwe pamoja na waandishi wa habari.
Mara baada ya
kukamilisha ziara yake katika migodi ya kuchenjua dhahabu ya Isanja Badugu, na
Magimi Gold Partners iliyopo katika eneo la Buluhe wilayani Mbogwe mkoani
Geita, Naibu Waziri Biteko alielekeza migodi husika kuhakikisha inahifadhi
nyaraka zote mgodini kama sheria ya madini inavyotaka.
Katika hatua nyingine,
Naibu Waziri Biteko alifanya ziara katika mgodi wa dhahabu wa Nyakafulu uliopo
Wilayani Mbogwe Mkoani Geita unaomilikiwa na
kikundi cha Isanja Badugu na kufanya mkutano wa hadhara ulioshirikisha
wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini katika eneo la mgodi huo
na kutatua kero zao hapo hapo.
Mara baada ya kusikiliza
na kutatua kero mbalimbali
zilizowasilishwa na wachimbaji wadogo hao, Naibu Waziri Biteko alitoa maelekezo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe kwa kushirikiana na
vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha inafanya uchunguzi dhidi wizi uliofanywa na mmoja wa viongozi wa kikundi cha Isanja
Badugu na kuchukua hatua za kisheria, wachimbaji wadogo kuhakikisha wanalipa
kodi za madini Serikalini, wamiliki wa
machimbo kuhakikisha hawawanyanyasi wachimbaji wadogo na kufanya nao kazi kwa
mikataba na wamiliki wa machimbo kuhakikisha hawatoi rushwa.
Kero zilizowasilishwa
na wachimbaji wadogo hao awali ni pamoja na
baadhi ya wachimbaji wa madini kufanya kazi pasipokuwa na mikataba
rasmi, ukosefu wa nishati ya umeme kwa ajili ya kuendeshea mitambo na baadhi ya
wachimbaji wadogo kutokulipwa mara baada ya kusimamishwa kazi.
Afisa Madini Mkazi wa
Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda (kushoto) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa
Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita, Christopher Kadeo (kulia) kabla
ya kuanza kwa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko kwenye machimbo ya
dhahabu ya wachimbaji wadogo yaliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita. Katikati ni
Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini Mhandisi Frederick Mwanjisi.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (katikati) akikagua nyaraka katika mgodi wa kuchenjua
dhahabu unaomilikiwa na kikundi cha Isanja Badugu, uliopo Wilayani Mbogwe
mkoani Geita.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kushoto mbele) pamoja na msafara wake akiendelea na ziara
katika mgodi wa kuchenjua dhahabu unaomilikiwa na kampuni ya Magimi Gold
Partners uliopo wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kushoto) akitoa maelekezo kwa mkurugenzi wa mgodi wa kuchenjua dhahabu unaomilikiwa na
kampuni ya Magimi Gold Partners, Juma Galehe (hayupo pichani). Wengine kutoka
kulia ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa
Geita, Daniel Mapunda na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (katikati) akimsikiliza mmoja wa wachimbaji wa madini ya
dhahabu katika machimbo ya Nyakafulu yaliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (katikati) akisalimiana na mmoja wa wachimbaji wadogo
kwenye machimbo ya Nyakafulu yaliyopo wilayani Mbogwe mkoani Geita.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko akizungumza na sehemu ya wachimbaji wadogo wanaojishughulisha
na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika machimbo ya Nyakafulu yaliyopo
wilayani Mbogwe mkoani Geita.
No comments:
Post a Comment