Na Asteria Muhozya, Bariadi
Waziri wa Madini Angellah Kairuki ametembelea Kituo cha Umahiri cha Bariadi ili kukagua
maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kumhaidi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony
Mtaka kuwa, Wizara ya Madini itaangalia
namna ya kuusaidia mkoa huo katika uendelezaji wa madini ya Nikel na chumvi
yanayopatikana mkoani humo.
Pia, Waziri Kairuki ametoa pongezi
kwa Mkandarasi SUMAJKT anayejenga kituo hicho kwa kazi iliyofanyika na
kumtaka mkandarasi huyo kuzingatia muda wa kukamilisha ujenzi na ubora wake.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kuridhia kuondoa tozo 9 kati ya
16 zilizokuwa zikitozwa na Taasisi mbalimbali za serikali katika Sekta ya Madini.
Amesema uwepo wa kituo hicho mkoani
humo, utawezesha wachimbaji wadogo wa madini kuchimba kwa tija.
Pia, ametoa rai kwa wananchi walio
tayari kuwekeza katika Sekta ya Madini kuwekeza mkoani humo pamoja na maeneo
mengine nchini.
Vilevile, amewataka wale wenye
leseni za madini kutoshikilia leseni hizo bila kuziendeleza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo
Anthony Mtaka, ameishukuru Wizara kwa kuuchagua mkoa huo kuwa miongoni mwa
mikoa ambayo vituo hivyo vya umahiri vinajengwa.
Amesema kuwa, uwepo wa kituo
hicho utawezesha wachimbaji kupata mafunzo ya uchimbaji bora wenye tija
ikiwemo kupata mahali sahihi ambapo shughuli za uendelezaji Sekta ya
Madini utafanyika.
Aidha, ameleeza pia, kituo hicho
kitatumika kama sehemu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi
ikiwemo taarifa kuhusu bei elekezi ambazo wizara kupitia Tume ya Madini
imekua ikitoa kila mwezi.
Vituo vya Umahiri vinajengwa na mkandarasi kampuni ya SUMAJKT maeneo
mbalimbali nchini, kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini
(SMMRP) kupitia Mkopo wa Benki ya Dunia.
Vituo hivyo vya umahiri
vinalenga kutoa mafunzo ya jiolojia katika utafiti, mafunzo ya uchenjuaji wa
madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususan kemikali zisizotumia
zebaki.
Pia, vinalenga katka kutoa mafunzo ya biashara kwa wachimbaji wadogo,
mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo bora za utunzaji wa
mazingira kwenye migodi ya wachimbaji.
Mbali na Bariadi, kituo kama hicho kinachojengwa Bukoba, Mara, Chunya,
Handeni, Songea, na Chuo Cha Madini Dodoma.
Wakati huo huo, Waziri Kairuki jana
alitembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Handeni. Akiwa kituoni hapo,
Waziri Kairuki alisema wizara inaendelea kuweka jitihada kuhakikisha kwamba sekta
ya madini inachangia zaidi katika pato la taifa
na hivyo kuwataka watumishi katika sekta husika kuhakikisha kuwa
wanafanya kazi kwa weledi na kuongeza kuwa,“ mjue kuwa kosa moja mtakalofanya
katika sekta hii, linawakosesha watanzania wote manufaa.
Aliongeza kuwa, hatosita kumwondoa
afisa yoyote atakayekwamisha kazi ya
serikali na watanzania na kueleza kuwa, bado analikumbushia suala hilo kwa kuwa
ni wajibu wake na kusema kuwa, ni vema watumishi katika sekta ya madini
kuongeza nguvu katika utendaji kazi na
kuhakikisha kuwamba wanatoa kipaumbele kwa rasilimali hiyo ya madini.
“ Mwaka huu tumewekewa malengo ya
kukusanya shilingi bilioni 310, natamani
tufike makusanyo ya shilingi bilioni 500. Nitawapima Maafisa Maadini kwa hayo.
Sitasita kuchukua hatua kwa wanaolegalega,” alisisitiza Waziri Kairuki.
Pia, alizungumzia kuhusu wamiliki wa leseni na kueleza kuwa, wote
wanaomikili leseni hizo wanapaswa kuziendeleza badala ya kuzihodhi bila
kuzifanyia kazi na kusema kuwa “ lengo letu ni kuhakikisha kwamba leseni
zinachangia katika upatikanaji wa
mapato,” alisema Kairuki.
Aidha, alieleza kwamba, Serikali kupitia Wizara ya madini inaandaa
Jukwaa la uwekezaji kati ya nchi ya China na Tanzania ambalo linatarajiwa
kufanyika mwezi Disemba na hivyo kutoa wito kwa wadau wa sekta ya madini
kuchangamkia fursa hiyo.
Pia, aliendelea kusisitiza kuhusu wadau wa sekta ya madini kufuata
sheria na kuzingatia taratibu zilizopo wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe, alisema
kuwa, uwepo wa kituo hicho katika wilaya hiyo kutakuwa na manufaa makubwa ya
kiuchumi wilyani humo na hivyo kutoa wito kwa wale wenye ni ya kufanya biashara
ya madini wilayani humo kutosita kufanya hivyo.
Alisema Wilaya hiyo itasimamia kwa karibu maendeleo ya ujenzi wa kituo
hicho kutokana na manufaa yake kwa wilaya hiyo na kueleza kuwa, wilaya hiyo ni
mzalishaji mkubwa wa madini ya viwandani hivyo uwepo wa kituo hicho
kitahamasisha wawekezaji zaidi kuwekeza wilayani humo.
Mwisho alimtaka Mkandarasi SUMAJKT kuharakisha ujenzi huo kabla ya
msimu wa mvua na kumwomba Waziri Kairuki kuhakikisha kusaidia upatikanaji wa haraka wa fedha za
ujenzi.
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki akiangalia matofali yanayotumika kujenga Kituo cha
Umahiri cha Bariadi, alipokitembelea kituo hicho ili kukagua maendeleo ya
ujenzi wake. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka.
Sehemu
ya jengo la Kituo cha Umahiri Bariadi katika hatua zake za ujenzi.
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki na Mwenyeji
wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka wakimsikiliza Mkandarasi SUMAJKT (hayupo) akieleza maendeleo ya ujenzi
wa kituo cha Umahiri cha Simiyu. Waziri Kairuki alitembelea kituoni hapo kwa
ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo husika.
Waziri wa Madini Angellah
Kairuki akimsikiliza Mkandarasi SUMAJKT anayejenga kituo cha Umahiri cha
Handeni akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho. Anayefuatilia
ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe , uongozi wa Mkoa, watalaam wa Ofisi
ya Madini Handeni na Tanga na watalaam kutoka Wizara ya Madini.
Mafundi
wa SUMAJKT wakiendelea na ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Handeni.
Mkuu
wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe, akimtambulisha waziri wa Madini Angellah
Kairuki kwa viongozi wa Wilaya alipofika wilayani humo kukagua maendeleo ya
ujenzi wa Kituo cha Umahiri kinachojengwa Handeni.
Mafundi
wa SUMAJKT wakiendelea na ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Handeni.
No comments:
Post a Comment