- · Ni baada ya kruhusu wananchi kijiji cha Mhandu kuendelea na uchimbaji dhahabu
Na Greyson Mwase,
Shinyanga
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko ameruhusu wananchi
wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga
kuendelea na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la utafiti wa madini
hayo lililokuwa linamilikiwa na Menan Sanga kwa kushirikiana na kampuni ya Lion Town.
Biteko aliyasema hayo
leo tarehe 24 Novemba, 2018 katika mkutano wa hadhara ulioshirikisha wananchi wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya
ya Kahama Mkoani Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kusikiliza na kutatua
changamoto za wachimbaji wa madini.
Katika ziara hiyo,
Biteko aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Mbunge wa
Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon
Berege, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Wataalam kutoka Wizara ya
Madini pamoja na waandishi wa habari.
Biteko alisema kuwa,
Serikali kupitia Wizara ya Madini
haiwezi kuruhusu mwekezaji kumiliki eneo pasipo kuliendeleza, kutokulipa
kodi inayohitajika Serikalini huku
wananchi wenye nia ya kuchimba katika eneo husika wakiendelea kuteseka.
Alisema kuwa, Serikali
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe
Magufuli imeweka mikakati mbalimbali ya uboreshaji wa Sekta ya Madini ikiwa ni
pamoja marekebisho ya Sheria ya Madini inayotambua madini kama rasilimali za
watanzania wote.
“Madini ni mali ya
watanzania wote, na sisi kama Serikali tumejipanga katika kuhakikisha kila
mwananchi anashiriki kwa kiasi kikubwa katika umiliki wa rasilimali za madini,
hivyo ninawaomba endeleeni kufanya kazi ya uchimbaji katika eneo hili wakati
taratibu nyingine zikiwa zinaendelea,” alisema Biteko huku akishangiliwa na
wananchi.
Katika hatua nyingine,
Naibu Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga
kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini waliopo katika eneo hilo pamoja na
kuwapatia leseni za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni za
madini ili wawe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta ya madini.
Pia alimtaka Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga kuandaa orodha ya wachimbaji wote wa madini
pamoja na taarifa za uzalishaji wa madini
yanayozalishwa na wachimbaji wa madini ikiwa ni pamoja na kodi mbalimbali wanazolipa
Serikalini.
Aliwataka wachimbaji
wadogo hao kufuata sheria na kanuni za madini ikiwa ni pamoja na ulipaji wa
kodi na tozo mbalimbali zinazohitajika Serikalini na kusisitiza kuwa, Serikali
haitasita kufuta leseni za madini pale watakapokiuka sheria na kanuni za
madini.
Awali wakizungumza
katika nyakati tofauti wananchi wa
kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga walisema
kuwa awali eneo hilo lilikuwa likimilikwa kampuni ya Lion Town tangu mwaka 1989
kabla ya kukabidhiwa kwa Menan Sanga ambaye amekuwa haendelezi uchimbaji katika eneo hilo huku akiwafukuza wananchi ambao wamekuwa
wakichimba madini ili kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba
ya wanakijiji hao Innocent Deus alisema kuwa wachimbaji wadogo wa madini
wanaochimba madini katika eneo hilo wamekuwa wakitishiwa maisha ikiwa ni pamoja
na kupigwa mara kwa mara na walinzi waliowekwa na mmiliki wa eneo hilo Menan Sanga.
Deus alisema awali
kikundi kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo kijulikanacho kwa jina la BMS
kiliundwa na kuomba leseni ya uchimbaji wa madini katika Wizara ya Madini
kupitia ofisi yake iliyopo mkoani Shinyanga lakini walishangaa kuambiwa kuwa
leseni husika imeshaombwa na kutolewa kwa Menan Manga.
Aliomba Serikali
kupitia Wizara ya Madini kuwapatia sehemu ya eneo hilo kwa ajili ya kuendelea
na shughuli za uchimbaji wa madini huku taratibu nyingine zikiendelea ikiwa ni
pamoja na urasimishaji na utoaji wa leseni ili waweze kuchangia kwenye pato la
Taifa.
Naye Mbunge wa
Msalala, Ezekiel Maige mbali na kutoa pongezi kwa Naibu Waziri wa Madini kwa
kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu aliiomba Wizara ya Madini kuwapatia maeneo yenye madini kwa ajili ya uchimbaji hususan katika
eneo husika kwa kuwa madini ni tegemeo pekee kwenye uchumi wao.
Alisema kuwa,
wananchi wengi wanaishi katika maisha magumu huku wakiwa na rasilimali za
madini ya kutosha ambazo zikitumiwa kikamilifu zinaweza kuwanufaisha na
kuimarisha huduma nyingine za jamii kama vile miundombinu ya barabara, umeme na
maji.
Wakati huohuo, Naibu
Waziri Biteko alifanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu ulioko
katika eneo la Kakola Wilayani Kahama mkoani Shinyanga lengo likiwa ni kuona shughuli za uchimbaji
madini na kufuatilia utekelezaji wa
maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki tarehe 24 Aprili,
mwaka huu.
Katika hatua
nyingine, Biteko aliutaka mgodi huo kuhakikisha unamaliza mgogoro kati yake na
wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa mchanga wa marudio ambao ni mali ya
wananchi wanaozunguka mgodi huo
waliouacha wakati wakipisha shughuli za uchimbaji kwa mgodi huo kwa kufuata
sheria na taratibu.
Aidha, aliutaka mgodi
kuandika barua kwenda Tume ya Madini kwa ajili ya kuomba mwongozo wa namna ya kutoa mchanga wa marudio na
kuwakabidhi wananchi ambao ndio wamiliki wa awali wa mchanga huo wakati
wakiendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo.
Aidha, Naibu Waziri
Biteko alikerwa na kitendo cha mgodi huo
kutokulipa kodi ya mapato kwa takribani miaka 19 na kuendesha shughuli zake kwa
kusuasua kwa kisingizio cha kuwa mgodi
umeamua kupunguza gharama za uendeshaji.
“Haiwezekani kama
mgodi mnaamua kupunguza gharama za uzalishaji pasipo kushirikisha Serikali huku
mkibadilisha umiliki wa leseni ya baruti wa kampuni nyingine na ni jambo ambalo
halikubaliki kabisa,” alisisitiza Biteko.
Alielekeza Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Sinyanga kuangalia iwapo kuna taratibu zimekiukwa ili
taratibu za kisheria zichukuliwe.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mhandu
kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga tarehe 24 Novemba, 2018
ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye mkoa huo yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za
wachimbaji wa madini.
Mmoja wa wananchi wa
kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga
akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kulia mbele) akiendelea na ziara katika eneo la uchimbaji wa chini ya ardhi kwenye Mgodi
wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo katika eneo la Kakola Wilayani Kahama mkoani
Shinyanga.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kushoto) akipata maelezo jinsi shughuli za uchimbaji wa madini ya
dhahabu zinavyofanyika chini ya ardhi
katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na msafara wake
pamoja na watendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu kabla ya kushuka chini ya
ardhi ili kujionea uchimbaji wa madini unavyofanyika.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (katikati mbele) akiendelea na ziara katika Mgodi
wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo katika eneo la Kakola Wilayani Kahama
mkoani Shinyanga.
No comments:
Post a Comment