Thursday, November 29, 2018

Waziri Kairuki ataka kaguzi za mara kwa mara Migodini


Na Asteria Muhozya, Chunya

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amewataka Maafisa Madini nchini kuhakikisha wanafanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya wachimbji wadogo ikiwemo kutoa elimu ya uchimbaji, masuala ya afya na usalama kazini ili kuongeza tija katika shughuli hizo.

Waziri Kairuki aliyasema hayo Novemba 27, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Chunya kinachojengwa na Mkandarasi kampuni ya SUMAJKT.

Alisema, wachimbaji wadogo wanatakiwa kulelelewa ili watoke katika uchimbaji mdogo wa madini kwenda uchimbaji wa  Kati na hatimaye kuwa wachimbaji  wakubwa, na kueleza kuwa, ili kufikia azma hiyo  elimu ya mara kwa mara kwa wachimbaji ni muhimu  ikatolewa  kwani itawezesha serikali kupata mapato kutokana na kufuata uchimbaji sahihi.

Pia, aliwataka Maafisa hao kuhakikisha kuwa wanatatua migogoro katika maeneo yao kwani suala hilo litawezesha uzalishaji zaidi na kupelekea serikali kunufaika na shughuli hizo, ikiwemo ongezeko la ajira na ustawi wa jamii.

Vilevile, Waziri Kairuki alieleza kuwa, pamoja na kwamba katika Mwaka wa Fedha 2018/19 wizara yake imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 310, lakini kama anataka makusanyo hayo yafikie shilingi bilioni 500 na kuongeza kwamba, Maafisa madini watapimwa kutokana na ukusanyo huo wa maduhuli.

“ Sisi tumepangiwa kukusanya shilingi bilioni 310. Lakini na mimi nataka makusanyo hayo yafikie shilingi bilioni 500 na nitawapima maafisa madini kwa ukusanyaji wa maduhuli,” alisema Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine, amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashaurina na Wizara ya madini katika masuala yote yanayohusu kodi za madini kabla ya kuyatolea maamuzi kwa kuwa, isipofanyika  hivyo inachangia taasisi za serikali kukinzana katika utoaji wa maamuzi.

Alisema, wizara inaandaa utaratibu wa kukutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali   na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kulijadili suala la  kodi katika sekta ya madini.

Akizungumzia umuhimu wa Kituo cha Umahiri, alisema kuwa, kitawezesha wachimbaji kujua taratibu zinazotakiwa katika  utekelezaji wa majukumu yao katika sekta ya madini na kwamba, wizara inaangalia uwekezano wa kuwa na vituo hivyo katika kila mikoa ikiwemo ofisi za kisasa na vituo vya mafunzo ili kuwezesha  kuwepo na tija zaidi katika sekta ya madini.

“Tumeanza na vituo vya mahiri lakini upo umuhimu wa maafisa wetu kuwa na nyumba za kuishi lakini  pia kuhakikisha kwamba maafisa wetu hawakai katika eneo moja kwa kipindi kirefu,” alisema.  

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Wilaya ya Chunya Athumani Kwariko alimweleza Waziri Kairuki kuwa, leseni nyingi wilayani humo hazifanyiwi kazi kutokana na wamiliki wake kukosa mitaji na uwepo wa migogoro.  Hata hivyo amesema kuwa, tayari ofisi hiyo imewasiliana  na  wamiliki hao ili kuhakikisha kwamba wanaziendeleza leseni hizo.

Akizungumzia madini yanayopatikana  wilayani humo  hiyo  aliyataja kuwa ni  pamoja na   ya  dhdhabu, chuma,  bati, ulanga, chokaa na kokoto na mchanga.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji Mkoa wa Mbeya Leonard Manyesha akielezea umuhimu wa kituo hicho alisema kwamba kitawawezesha  kupata maelekezo ya kitaalam kuhusu uchimbaji na hivyo kuwawezesha kupata mazao bora ya dhahabu na yenye tija.

Aidha, alipongeza kwa hatua ya serkali ya kutaka kuhamasisha Mikoa kutenga maeneo kwa ajili ya uanzishaji wa masoko ya madini na kueleza kuwa, uwepo wa masoko hayo utasaidia tatizo la wachimbaji kuficha mapato kuisha.


Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia ramani ya jengo la Kituo cha Umahiri Chunya litakavyokuwa mara baada ya kukamilika kwake. Jengo hilo linajengwa na Mkandarasi SUMAJKT. 

Sehemu ya jengo la  Kituo cha Umahiri Chunya  likiwa katika maendeleo ya ujenzi wake. 

Sehemu ya viongozi wa Wilaya, viongozi wa  Ofisi za Madini Mbeya na Chunya pamoja na wadau wa madini wilayani humo wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani). 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akisikiliza jambo kutoka kwa Mkandarasi SUMAJKT  alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri Chunya. Wengine ni Wataalam kutoka Ofisi za Madini Mbeya na Chunya, wataalam kutoka Wizara ya Madini, na uongozi wa Wilaya ya Chunya.

No comments:

Post a Comment