Na Greyson Mwase
Leo tarehe 25
Novemba, 2018 Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amefanya ziara katika Mgodi
wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga lengo likiwa ni
kukagua shughuli za uchimbaji madini, kusikiliza na kutatua kero
mbalimbali zinazoukabili mgodi huo.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,
Anderson Msumba, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Timothy Ndaya, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kahama,
Mhandisi Abdulrahman Milandu, Afisa Mgodi Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Modest
Tarimo, Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini Mhandisi Frederick
Mwanjisi,wataalam kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na waandishi
wa habari.
Mara baada ya
kufanya ziara na kupokea taarifa ya hatua za kufunga mgodi wa Buzwagi,
Naibu Waziri Biteko alitoa maagizo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na:- mgodi kuwasilisha upya mpango wa ufungaji wa
shughuli zake kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini ili aweze kuwasilisha
kwenye Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji wa Migodi
kwa ajili ya kuidhinishwa ili utekelezaji wake uanze mara moja, pawepo na
utaratibu wa kupitia upya kiwango cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa
mazingira (rehabilitation bond) na kuweka mkakati wa kuhakikisha kuwa shughuli
za kiuchumi za wakazi wanaozunguka mgodi huo haziathiriki na ufungaji wa mgodi
husika.
Katika hatua
nyingine, Naibu Waziri Biteko aliutaka uongozi wa mgodi huo kufuata sheria na
kanuni za ufungaji wa mgodi kwa wakati na kuepuka kufanya kazi kwa zimamoto.
Meneja Mkuu wa Migodi
ya Dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Buzunzu alisema kama mgodi
wamepokea maelekezo na kuahidi kuwa watayafanyia kazi.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (kushoto) akimsikiliza Afisa Mgodi Mkazi wa Mkoa wa Kahama,
Modest Tarimo ( wa pili kulia) mara alipowasili kwenye ofisi yake iliyopo
katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama
Mkoani Shinyanga. Kulia ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kahama, Mhandisi
Abdulrahman Milandu.
Naibu Waziri wa
Madini, Doto Biteko (wa tatu kulia mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na
ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani
Shinyanga.
Mtaalam kutoka Mgodi
wa Dhahabu wa Buzwagi, Jonathan Joseph (kulia) akifafanua jambo kwa Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kushoto).
Sehemu ya Mgodi wa
Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Meneja Mkuu wa Migodi
ya Dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, Benedict Buzunzu (kushoto) akielezea
mikakati ya Mgodi wa Buzwagi kwenye ufungaji
wa shughuli zake kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia).
Uchimbaji wa wazi wa
dhahabu (open pit) ukiendelea katika Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliopo katika
Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
No comments:
Post a Comment