Monday, October 29, 2018

Hotuba ya Waziri wa Madini Mheshimiwa Angellah J. Kairuki (Mb.) akifungua jukwaa la sekta ya uziduaji Tanzania, lililoandaliwa na hakirasilimali


HOTUBA YA WAZIRI WA MADINI MHESHIMIWA ANGELLAH J. KAIRUKI (MB.) AKIFUNGUA JUKWAA LA SEKTA YA UZIDUAJI TANZANIA, LILILOANDALIWA NA HAKIRASILIMALI - MTANDAO WA ASASI ZA KIRAIA UNAOFANYA KAZI ZA UCHECHEMUZI KATIKA SEKTA YA UZIDUAJI HAPA TANZANIA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA HOTELI YA AFRICAN DREAMS, DODOMA
TAREHE 24 OKTOBA 2018

Waandaaji wa Jukwaa la Sekta ya Uziduaji Tanzania 2018;

Watoa mada kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania;

Wawakilishi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Fedha;

Madhehebu ya Dini (BAKWATA, CCT and TEC);

Wawakilishi wa Mashirika ya Vyama na Asasi za Kijamii;

Washirika wa Kimaendeleo;

Waandishi wa Habari;

Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Habarini za asubuhi na Karibuni katika Jiji la Dodoma.

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana siku ya leo katika ufunguzi wa Jukwaa la Sekta ya Uziduaji Tanzania ambalo limewaleta pamoja wadau mbalimbali kutoka nyanja zote ndani na nje ya Tanzania, kwa kusudi la kujadili, kujifunza na kushirikishana uzoefu katika utetezi na ushawishi wa michakato ya maamuzi yatokanayo na sekta ya uziduaji ili kuleta maendeleo endelevu yanayotarajiwa na sekta hii kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla. Jukwaa hili limeandaliwa wakati muafaka kwani katika kipindi hiki, tumefanya mageuzi makubwa nchini na tunaendelea na mageuzi mbalimbali lengo ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na hivyo kulazimika kuweka mkazo katika kuihuisha sekta ya uziduaji na ajenda ya viwanda kwa ifikapo mwaka 2025.

Ndugu Washiriki, Usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia ni chachu ya maendeleo ya Tanzania. Mabadiliko ya Sera, Sheria, Taratibu na Kanuni yamefanyika kuinua uzalendo, kurudisha uhuru wa umiliki na usimamizi wa rasilimali za nchi.

Ndugu Washiriki, Nachukua fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuonesha uzalendo katika kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya watanzania. Hii imejidhihirisha kupitia Serikali kuendesha majadiliano na kampuni za uchimbaji madini ili kuhakikisha Tanzania inanufaika kupitia rasilimali zake lakini pia kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.

Sekta ya uziduaji nchini inatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu, hususan kutokana na ongezeko kubwa la uwekezaji. Hivyo, upo umuhimu wa kuendelea kupanua wigo wa majadiliano na kusimamia rasilimali kwani kama ambavyo Mheshimiwa Rais anasisitiza mara kwa mara kuwa uzoefu katika nchi nyingine unaonesha rasilimali hizi zinaweza kugeuka na kuwa laana itakayoharibu na kudunisha matokeo ya maendeleo na kuleta umasikini mkubwa.

Ndugu Washiriki, Ni muhimu kwa Tanzania kuweka zana thabiti ili kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji na usimamizi endelevu wa sekta za madini, mafuta na gesi asilia. Hii inajumuisha kuwepo kwa ufanisi wa ushirikishwaji wa wadau kutoka nyanja mbalimbali zikiwemo ASASI ZA KIRAIA.

Sisi kama Serikali, kupitia Wizara zote mbili ya Madini na ya Nishati, jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kuwa tunaendelea kusimamia utendaji kazi kwenye sekta ya uziduaji kwa kuzingatia kikamilifu utekelezaji wa Sera, Sheria na mahitaji ya udhibiti wa kitaifa na kimataifa. Lakini pia, kuendelea kushirikiana na wadau ili kuweza kuishauri Serikali njia sahihi zitakazoiwezesha Nchi kunufaika na rasilimali hizi. Mbali na hayo, kuwa na jitihada za kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia na makundi maalum yanapata fursa kushiriki kikamilifu katika Sekta ya uziduaji.

Ndugu Washiriki, Kwa upande wa Wizara ya Madini, katika suala hili la usimamizi wa rasilimali za nchi na hususan katika Sekta ya Madini ninayoisimamia, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Spika wa Bunge la Tanzania kwa kuunda Kamati ambazo zilishughulikia changamoto zilizopo katika Sekta ya Madini. Mapendekezo ya Kamati zote yamefanyiwa kazi na baadhi ya mapendekezo mengine yanaendelea kutekelezwa.

Hata hivyo, Wizara yangu imeweka vipaumbele vifuatavyo ili kuhakikisha sekta hii ya madini inaimarika na inanufaisha Watanzania wote:

(i)  Kuwa na uwazi na uwajibikaji zaidi katika Sekta ya Madini na uziduaji kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini. Tuna uhakika wa kufanikisha lengo hili kwa kuwa tuna mikakati madhubuti ya  kuimarisha ukaguzi wa migodi mikubwa, ya kati na ya uchimbaji mdogo ili kupata taarifa sahihi za uwekezaji, uzalishaji, mauzo na kodi mbalimbali; kudhibiti utoroshwaji wa madini katika maeneo ya uzalishaji na ya kutokea nchini (Exit Points); kuimarisha ukaguzi wa madini ya ujenzi na viwandani; kufuatilia taarifa za ununuzi na uuzaji (returns) kwa wafanyabiashara wa madini (Dealers & Brokers); kufuatilia wadaiwa wa tozo mbalimbali za madini kwa mujibu wa Sheria kwa wakati; kudhibiti uchimbaji na uchenjuaji haramu wa madini; na kuboresha na kuimarisha mfumo wa utoaji wa leseni za madini na kutunza taarifa zake.

(ii)  Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo na wa Kati wa Madini. Katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wanaendelea kutoka hatua waliopo sasa na kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye wachimbaji wakubwa, Wizara imetenga jumla ya maeneo 4 nchini kwa ajili ya wachimbaji wadogo na tutaendelea kutenga maeneo hayo kabla ya kugaiwa kwa wachimbaji wadogo yatabainishwa uwepo wa mashapo ya madini na Taasisi yetu ya GST ya utafiti wa madini ili kuepusha kufanya uchambuzi kwa kubahatisha. Vilevile, Wizara ya Madini kupitia STAMICO, itawaelimisha wachimbaji wadogo namna ya kutumia teknolojia ya kisasa na rahisi katika kuongeza uzalishaji na tija wakati wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Aidha, Wizara ipo katika hatua nzuri ya kukamilisha ujenzi wa Vituo 7 vya Mfano (Centres of Excellency) kwa ajili ya mafunzo ya uongezaji thamani madini, uchimbaji salama pamoja na kuongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza mapato kwa wachimbaji wadogo na Serikali. Vile vile, katika vituo hivi tutatoa Huduma za uchenjuaji kwa wachimbaji wadogo kwa gharama nafuu. Lwamgasa ambao ni mgodi wa mfano, mwisho wa mwaka huu utakamilika.

(iii)  Kuimarisha shughuli za uongezaji thamani madini. Katika eneo hili, Wizara imejiwekea mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini na kuendelea kutoa leseni za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya metali. Hadi sasa, Wizara kupitia Tume ya Madini imeshatoa leseni kadhaa za uchenjuaji, na katika hili nawasihi wananchi wenye vigezo kulingana na Sheria waombe leseni hizo. Aidha, Wizara inafanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa inapata wawekezaji mahiri na wenye sifa stahiki katika Vinu vya uchenjuaji na usafishaji wa madini. Ili kufanikisha suala hili la uongezaji thamani madini, Wizara yangu imekwishaanza taratibu za kuandaa Muswada wa Sheria ya Uongezaji Thamani Madini kwa lengo la kukuza na kusimamia vyema shughuli za uongezaji thamani madini nchini.

(iv)   Kuimarisha Ukaguzi wa Usalama, Afya, Mazingira na Uzalishaji wa Madini Migodini. Kama inavyoeleweka, shughuli za uchimbaji wa madini huweza kuambatana na athari za kiafya, usalama na uharibifu mkubwa wa mazingira. Ili kuondokana na athari hizo, Wizara imeimarisha kaguzi migodini na maeneo ya uchenjuaji wa madini, kuongeza huduma za ugani hususan kwa wachimbaji wadogo, kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali zinazohusika na usimamizi wa masuala ya Afya, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ikiwemo utekelezaji wa Mkataba wa Minamata wa kupunguza na hatimaye kuzuia matumizi ya Zebaki katika uchenjuaji. Kwa kuwa usalama migodini ni muhimu sana; natoa rai kwa wachimbaji wa madini na wale wanaofanya shughuli za uchenjuaji hususan madini ya dhahabu kuhakikisha wanaimarisha miundombinu ya mabwawa ya kuhifadhi mabaki yenye kemikali (Tailings Storage Facility – TSF) kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mwaka 2017.

(v)   Kuelimisha Umma na kuboresha Mawasiliano baina ya Wizara na Wadau wa Sekta ya Madini. Wizara yangu imeweka mikakati ya kuhakikisha inafanya mikutano ya ana kwa ana na wawekezaji na kutoa elimu kwa Umma kuhusu rasilimali madini. Lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya kina kuhusu masuala ya rasilimali madini. Kuhusu hili, ninyi wote ni shahidi wa kazi kubwa inayofanywa na mimi mwenyewe, Manaibu wangu na Tume ya Madini ya kukutana na kutembelea wananchi wanaofanya shughuli za madini na kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria za Nchi. Aidha, Wizara yangu inaahidi kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu rasilimali madini, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini kupitia vipindi mbalimbali vya redio na televisheni na njia nyingi za uelimishaji Umma.

Ndugu Washiriki, Natoa wito kwa wadau wote watumie majukwaa mbalimbali kama hili kama njia mojawapo ya kuboresha mazungumzo na mijadala ya namna gani tunaweza kunufaika na utajiri wa rasilimali iliyopo katika sekta ya uziduaji ili kuinua uchumi, kupunguza umaskini na kukabiliana na laana inayoweza kujitokeza kwenye rasilimali hizi.

Ndugu Washiriki, Kwenye Kongamano hili, nimefurahishwa na uwepo wa watu kutoka nyanja mbalimbali na mashirika yaliyowakilishwa hapa yakiwemo makampuni, mitandao ya asasi za kijamii, makundi ya madhehebu ya Imani, watafiti, wasomi, jamii, washirika wa maendeleo na viongozi wa mashirika na taasisi za kiserikali. Tunathamini michango yenu katika sekta hii na kujitoa kwenu katika mijadala ndani ya kongamano hili kutatusaidia sana kuimarisha sekta hii. Jadilianeni na badilishaneni mawazo mliyo nayo na hatimaye ibukeni na mawazo mapya ya kuboresha na kuimarisha sekta ya uziduaji nchini. Nitapenda pia kupata maazimio na mapendekezo mtakayoyafikia.

Ndugu Washiriki, Napenda nitumie fursa hii kuzihakikishia Asasi zote za Kiraia kwamba Serikali inathamini mchango wenu katika Sekta ya Madini na Sekta ya Uziduaji kwa ujumla na kuahidi ushirikiano katika utekelezaji wa Sheria na Kanuni mpya za Madini. Nitumie fursa hii pia kukaribisha wananchi wote ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini katika sekta ya madini. Nimefarijika sana kuona Asasi za Kiraia zinatoa ushirikiano kwa Serikali katika usimamizi wa rasilimali zetu kwa kuhakikisha rasilimali hizi zinawanufaisha wananchi bila ubaguzi wowote. Hii inathibitisha kwamba ushirikiano baina ya wadau mbalimbali, Serikali, Wawekezaji na CSOs katika Sekta ya Uziduaji ni jambo la msingi na lenye manufaa kwa Serikali na Wananchi wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo nchini. Nipende tu kuzihakikishia Asasi za Kiraia kuwa milango yetu Wizarani iko wazi kwa kupokea ushauri na maoni yenye lengo la kuboresha na kuimarisha Sekta hii muhimu. 

Ndugu Washiriki, Kwa mara nyingine tena nawashukuru kwa kunialika katika ufunguzi wa mkutano huu muhimu na nawakaribisha katika Jiji la Dodoma hususan Wizara ya Madini kwa ajili kuwekeza katika Sekta hii. Baada ya kusema maneno haya machache natangaza kwamba Jukwaa la Sekta ya Uziduaji Tanzania limefunguliwa rasmi.

Asanteni kwa kunisikiliza

No comments:

Post a Comment