Na Greyson Mwase,
Dodoma
Mtendaji Mkuu
wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA) na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Haroun Kinega amesema kuwa,
shirikisho hilo kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Madini limeweka
mikakati katika kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakuwa na mchango mkubwa kwenye
ukuaji wa Sekta ya Madini kupitia kodi na tozo mbalimbali.
Kinega ameyasema hayo leo tarehe 29 Oktoba, 2018 katika mkutano mkuu wa uchaguzi
wa viongozi wa FEMATA Nchini uliofanyika jijini Dodoma wenye lengo la kuchagua
viongozi wapya pamoja na kujadili changemoto mbalimbali wanazokabiliana nazo
kwenye shughuli za uchimbaji wa madini nchini.
Akielezea mikakati ya ongezeko la mapato kutokana na kodi zinazolipwa na
wachimbaji wadogo wa madini, Kinega alisema kuwa FEMATA kwa kushirikiana na
Tume ya Madini imeweka mikakati ya kuhakikisha maeneo zaidi yanatengwa na
kutolewa leseni kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini na kuwataka wachimbaji
wadogo wa madini kuunda vikundi, kusajili ili kuomba leseni na uchimbaji wao
kuwa rasmi.
“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa asilimia kubwa ya wachimbaji wadogo wa
madini nchini wanakuwa rasmi kwa kupatiwa leseni za madini ili kurahisisha ukusanyaji
wa mapato ya serikali, ninaamini tunaweza kufikia lengo kupitia mikakati
tuliyojiwekea.
Wakati huo huo akielezea mikakati ya Serikali katika kuwasaidia
wachimbaji wadogo wa madini, Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas
Mwano alisema kuwa mbali na Serikali kupitia Wizara ya Madini kutenga maeneo
kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini, elimu imekuwa ikitolewa kwa
wachimbaji wadogo kuhusu sheria na kanuni za uchimbaji wa madini pamoja na
usalama migodini.
Alisema kuwa elimu ambayo imekuwa ikitolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini imepunguza kwa
kiasi kikubwa migogoro iliyokuwa ikijitokeza kwenye maeneo yao ya uchimbaji wa
madini.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA), John Bina mbali na
kupongeza juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya
Madini aliiomba Serikali kuhamasisha
wawekezaji kutoka nje kwa ajili ya kujenga mitambo ya kuchenjulia madini nchini
na kukuza pato la taifa.
Katika uchaguzi huo wa viongozi wa FEMATA nafasi zinazogombewa ni pamoja
na Rais, Makamu wa Rais, Katibu Mkuu,
Naibu Katibu Mkuu, Mweka Hazina, Mweka Hazina Msaidizi, Mwakilishi wa Wanawake na Mwenyekiti wa Kamati ya Madini
ya Dhahabu.
Nafasi nyingine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Nishati,
Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Viwanda, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya
Chumvi, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Tanzanite, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini
ya Almas, Mwenyekiti wa Kamati ya Madini Mengine ya Vito na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Usuluhishi
na Kanuni.
Aidha, Nafasi nyingine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi,
Mjumbe wa Afya, Mazingira na Usalama Migodini, Mwakilishi wa Wafanyabiashara,
Mwakilishi wa Wachimbaji Wasio Rasmi, Mjumbe wa Mpango wa Kuongeza Uwazi na
Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Gesi na Mafuta (TEITI) na Bodi ya
Wadhamini nafasi tano.
Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA) na Kamishna kutoka
Tume ya Madini, Haroun Kinega (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari mara
baada ya ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Vyama vya
Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA) uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2017
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini
(FEMATA), John Bina akielezea mafanikio ya shirikisho hilo mbele ya wawakilishi
wa vyama vya wachimbaji wadogo wa madini mikoani (hawapo pichani)
Sehemu ya wawakilishi wa vyama vya wachimbaji wadogo wa madini mikoani
wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya
Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA), John Bina (hayupo pichani)
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Jonas Mwano (kulia) akielezea
mikakati ya Serikali kwenye uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa madini kwa
waandishi wa habari.
Sehemu ya wajumbe wa meza kuu wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa
na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA) na Kamishna kutoka
Tume ya Madini, Haroun Kinega (hayupo pichani)
No comments:
Post a Comment