Monday, October 29, 2018

Hotuba ya Waziri wa Madini Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb.), akizindua Kamati ya uhamasishaji uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia nchini


Mheshimiwa Stanslaus Nyongo (Mb.), Naibu Waziri, Wizara ya Madini;

Prof. Simon Msanjila, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini;

Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati;

Ndugu Ludovick Utouh, Mwenyekiti Kamati ya TEITI;

Wajumbe wa Kamati ya TEITI;

Sekretarieti ya TEITI;

Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote ninapenda kuanza kwa kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema kwa kutujaalia kukutana siku ya leo katika uzinduzi wa Kamati ya TEITI. Kamati ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi asilia nchini Tanzania kwa kipindi cha Oktoba 2016 – Oktoba 2019. Ninakushuru ndugu Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI kwa kunialika kujumuika nanyi katika tukio hili muhimu ambalo ni kielelezo na nyenzo ya kufanikisha kuboresha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uziduaji hapa nchini. Kama mnavyofahamu, mwaka 2009 Nchi yetu ilijiunga katika mpango wa kimataifa wa kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya Uchimbaji wa Rasilimali (Extractive Industries Transparency Initiative) lengo kuu ikiwa ni kuhakikisha kwamba mapato yanayotakiwa kulipwa Serikalini kutoka Sekta ya uziduaji yanapatikana na kuwekwa wazi kwa wananchi. Msingi wa falsafa hii ya uwazi na uwajibikaji kwenye Sekta ya uziduaji umejikita kwenye Ibara ya 8 (1) (c) na Ibara 27 (1) & (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Ibara hizi zinazungumzia Serikali kuwajibika kwa wananchi wake na kwamba rasilimali zote za nchi zitatunzwa na wananchi wote kwa manufaa ya wote. Aidha, Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania ya mwaka 2015 nayo imeweka msingi imara wa kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji kwenye Sekta ya uziduaji Nchini. Hivyo, Kamati hii ninayoizindua leo hii ina umuhimu mkubwa kwa mustakabali ya maendeleo ya Taifa letu iwapo mtatekeleza majukumu yenu kwa weledi, uzalendo na kwa kuipenda nchi yenu. Ni matarajio yangu na matarajio ya kila mwenye kuitakia mema Nchi yetu, mnakwenda kutekeleza wajibu wenu ipasavyo kwa maslahi mapana ya Nchi yenu kwani Taifa limewaamini hivyo msiliangushe.

Ndugu Mwenyekiti na ndugu Wajumbe wa Kamati, Itakumbukwa kuwa, tangu TEITI ianzishwe Mwaka 2009 hii ni Kamati ya tatu. Kamati mbili za awali ziliongozwa na Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mark Bomani. Ninayo faraja kubwa ya kuishuhudia siku hii na kushiriki tukio la leo nikiwa Waziri wa Madini. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua mimi kwenye wadhifa huu na kwa kukuteua wewe Bw. Ludovick Utouh Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Mstaafu) kuiongoza Kamati ya tatu ya TEITI. Maamuzi ya Mheshimiwa Rais kumteua Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI ni maamuzi ya kimapinduzi katika kuboresha usimamizi wa rasilimali nchini ilizo nazo katika Sekta ya uziduaji na kuhakikisha kuwa manufaa yanayopatikana kutokana na rasilimali hizi yananufaisha Watanzania wote na kuleta maendeleo kwa nchi. Uteuzi wa Mwenyekiti umezingatia uwezo wake wa uongozi na kubeba dhamana hii kwa kushirikiana na wajumbe kumi na tano kutoka Serikalini, Kampuni za madini, mafuta na gesi asilia na Taasisi za Kiraia. Ni matumaini yangu utaendeleza kazi nzuri ulizokwishafanya huko nyuma katika kuiongoza Kamati hii. Aidha, kwa upande wenu wajumbe wa Kamati hii mlioteuliwa, tunaamini mnao uwezo na weledi wa kuifanya kazi hii. Vile vile tunaamini mna nafasi kubwa ya kuisaidia Serikali katika agenda yake ya kuboresha Sekta hii muhimu kwa kuainisha njia za kuboresha usimamizi wa Sekta ya uzuduaji, kuvutia wawekezaji, kuongeza pato la Taifa na kujenga imani kwa wadau wa sekta hii. Katekelezeni majukumu yenu kwa maslahi ya Nchi yenu.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, Nataka mtambue kuwa ninyi ndiyo wasimamizi wa kuhakikisha kuwa Serikali inaboresha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa Sekta ya uziduaji hususan kwenye utoaji wa leseni na mikataba; usimamizi na uendeshaji wa kampuni; ukusanyaji wa mapato; na mgawanyo wa mapato na matumizi. Vile vile, mtambue kuwa mmepewa mamlaka makubwa na mmeaminiwa kulinda maslahi ya Nchi yenu kwa kusimamia Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania ya mwaka 2015 na vigezo vya Kimataifa vya Uwazi (Extractive Industries Transparency Initiative (EITI) Requirements).

Ndugu Mwenyekiti na ndugu Wajumbe wa Kamati, Sote ni mashahidi wa jinsi Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilivyo na dhamira ya dhati kuona kwamba Sekta ya uziduaji inawanufaisha watanzania wote kwa kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato yake stahiki na wananchi wanashiriki kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za Nchi yao. Napenda kuwakumbusha kuwa Serikali na wananchi wake wana matarajio makubwa kwenu kuwa mtahakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za nchi ili kuzuia na kupunguza udanganyifu na ukwepaji wa ulipaji wa kodi kulingana na sheria za nchi yetu ili hatimaye vizazi vijavyo vinufaike na utajiri huu wa rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia za madini, mafuta na gesi asilia. Ni imani yangu na pia ni imani ya Mheshimiwa Rais kuwa kupitia uongozi wa Bw. Ludovick Utouh katika Kamati hii mtaibadilisha TEITI ile ya toka 2009 ambayo haijulikani kwa wananchi walio wengi na kuwa TEITI ambayo inajulikana na kila Mtanzania. Taasisi hii ina umuhimu wa kipekee katika kuliwezesha Taifa kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati kwa kupitia viwanda ifikapo Mwaka 2025. Ili Serikali iweze kufikia lengo hili, ni lazima jitihada ziongezwe katika kukusanya mapato ya Serikali na kuyatumia mapato hayo kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kulingana na bajeti zilizoidhinishwa.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu Wajumbe, Kamati hii ipo kisheria kulingana na Kifungu cha 10 cha Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilimia ya Mwaka 2015. Kamati itakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mapato ya Sekta ya uziduaji yanayopaswa kuwasilishwa Serikalini, yanahakikiwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi wote.
Majukumu mengine ya Kamati yatakuwa ni pamoja na:-
(i)        kuandaa mfumo wa uwekaji uwazi na uwepo wa uwajibikaji wa malipo yaliyofanywa na kampuni za uziduaji Serikalini;

(ii)      kuzitaka kampuni zote za uziduaji na taasisi za Serikali zinazoshughulika na uziduaji kutoa taarifa sahihi juu ya malipo na mapato yaliyokusanywa na taasisi hizo katika mwaka husika wa fedha;

(iii)    kuzitaka kampuni za uziduaji kuwasilisha kwenye Kamati gharama za uwekezaji, takwimu za uzalishaji na mauzo ya nje katika mwaka husika wa fedha;
(iv)     kuhamasisha ufahamu juu ya mchango wa Sekta ya uziduaji na maendeleo yake kiuchumi na kijamii pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika katika Sekta ya uziduaji; na

(v)       kusababisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya uchunguzi wa tofauti ya hesabu za malipo na mapato yanayotokana na Sekta ya uziduaji kulingana na vifungu vya sheria hii.

Ndugu wajumbe, Baada ya uteuzi wa Bw. Utouh nilishakuwa na mazungumzo naye kuhusu changamato na matatizo yanayoikumba Sekretarieti ya TEITI. Nilifurahishwa sana Mwenyekiti aliponipa taarifa ya mabadiliko ya msimamo wa EITI Makao Makuu yaliyo Oslo nchini Norway, kuwa mahusiano ya kikazi yamerejeshwa kati ya Ofisi hiyo na Ofisi yetu. Sisi Wizarani tunawaahidi kuwapa kila aina ya ushirikiano mtakaouhitaji. Tutafanya hivyo maana sote tunajenga nyumba moja. Milango yangu iko wazi wakati wote. Karibuni sana.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu wajumbe, Kwa hakika mna kazi kubwa mbele yenu. Ninafahamu kwamba ili muweze kutekeleza majukumu yenu kama yalivyoelezwa kwenye kifungu cha 10(1)(2) cha Sheria ya TEITI ya Mwaka 2015, mnahitaji rasilimali watu na vitendea kazi. Ninafahamu kuwa kazi za kila siku za Kamati yako zinatekelezwa na Sekretarieti ya TEITI. Naomba kuwafahamisha kuwa tumeanza kushughulika changamoto mbalimbali zinazofanya msitekeleze majukumu yenu ipasavyo. Kwa mfano mchakato wa uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Sekretarieti umefikia hatua nzuri. Hivyo, ninaomba muwe na subira wakati tukishughulikia changamoto hizo. Kwa sasa, endeleeni kuwatumia watumishi wa tuliowaweka kwenye Sekretarieti kutekeleza majukumu yenu. Mambo yatakuwa sawa siku siyo nyingi. Katibu Mkuu wa Madini yupo hapa, ninamuelekeza afuatilie Muundo wa TEITI ukamilike haraka iwezekanavyo kuwezesha uwepo wa kuajiri watumishi wa Sektretarieti kuendana na mahitaji. Pia, ili Kamati iweze kutekeleza vyema majukumu yake, ninamkabidhi Mwenyekiti kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati vitendea kazi kwa ajili ya rejea ambavyo ni Taarifa ya nane ya TEITI, Taarifa ya uwekaji wazi wa majina ya watu wanaomiliki hisa katika kampuni za madini, mafuta na gesi asilia hapa nchini, Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia, Sheria ya Madini, Sheria ya Mafuta, Sheria ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi na EITI Standards 2016. Katika kupitia taarifa ya nane ya TEITI, mtaona mapungufu mengi yaliyoibuliwa na Mtaalam Elekezi aliyetayarisha ripoti hiyo ambapo ni jukumu lenu kutafuta majibu na suluhisho ya matatizo hayo.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu wajumbe, Kulingana na matakwa ya Kifungu cha 10 (1) na (2) cha Sheria ya TEITI ya Mwaka 2015, majukumu yenu ni mengi na mazito. Hata hivyo, bado Kifungu 10 (3) cha Sheria hiyo, kinaitaka Kamati iandae na kuwasilisha kwangu, ripoti ya utekelezaji wa shughuli zote zilizotajwa katika kifungu kidogo cha (2) kwa ajili ya hatua stahiki katika kuboresha usimamizi wa Sekta ya uziduaji hapa nchini. Hivyo Mwenyekiti, nitakuwa nategemea kuipata mapema ripoti tajwa kwa ajili ya kuifanyia kazi.

Ndugu Mwenyekiti na Ndugu wajumbe, Mwisho, Wizara inawatakia utekelezaji mwema wa majukumu yenu na kwa mara nyingine tena mimi na wenzangu Wizarani tunawaahidi kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yenu.

Baada ya kusema hayo, napenda sasa kutamka kuwa Kamati ya tatu ya TEITI nimeizindua Rasmi leo tarehe 25 Oktoba, 2018.

Asanteni kwa kunisikiliza.


No comments:

Post a Comment