Tuesday, August 7, 2018

Viongozi wasiokwenda na kasi ya Tume ya Madini kutenguliwa


Greyson Mwase na Asteria Muhozya, Morogoro

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema kuwa viongozi pamoja na maafisa waandamizi walioteuliwa kufanya kazi katika Tume ya Madini teuzi zao zinaweza kutenguliwa iwapo watafanya kazi kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 06 Agosti, 2018 wakati wa ufunguzi wa mafunzo  ya kazi kwa viongozi  na maafisa waandamizi wa Tume ya Madini  iliyofanyika mjini Morogoro na kuhudhuriwa na watendaji na watumishi kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. delardus Kilangi.

Alisema kuwa, Serikali imewateua kufanya kufanya kazi na Tume ya Madini  huku ikiwa na matarajio makubwa ikiwa ni pamoja na kuondoa kabisa urasimu kwenye utoaji wa leseni kwa kuhakikisha kuwa wanatoa leseni kwa wakati, kutatua mogogoro ya wachimbaji wadogo na kuwa wabunifu kwenye ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini.

Aidha, Waziri Kairuki aliongeza kuwa watendaji wapya wanatakiwa kuwa makini kwenye zoezi zima la utoaji wa leseni kwa kuhakikisha kuwa wanahakiki historia za waombaji wa leseni kwenye uchimbaji madini kabla ya kutoa leseni mpya.

“Ni vyema mkahakikisha kuwa mnafahamu kwa kina historia za waombaji wa leseni za madini hususan kwenye mapato na matumizi kwa mwaka, ulipiaji wa leseni, ushiriki katika utoaji wa huduma za jamii, uzingatiaji wa kanuni za uhifadhi na mazingira na kuwapatia leseni waombaji  wale tu watakaokidhi vigezo,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine,Waziri Kairuki alitoa onyo kwa watumishi watakaothubutu kuhujumu mfumo wa huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao ujulikanao kama online mining cadastre transactional portal na kuongeza kuwa Wizara haitasita kuwachukulia hatua za kisheria watakaohujumu mfumo.

Waziri Kairuki aliwataka maafisa madini wa mikoa kuhakikisha wanaainisha maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini na kumpatia taarifa mapema na kuhakikisha wanafanya mikutano ya mara kwa mara na wachimbaji wadogo ili kubaini changamoto zao.

Awali akielezea mafunzo hayo, Waziri Kairuki alisema mafunzo hayo ya siku sita yatalenga kutoa elimu kuhusu historia ya mabadiliko ya sheria ya madini, sheria ya madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, muundo wa tume ya madini na mawasiliano ya ndani na nje ya tume.

Aliendelea kueleza maeneo mengine kuwa ni pamoja na muundo na mfumo wa mawasiliano wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), taratibu za ofisi na makusanyo na maduhuli ya Serikali kwa njia ya kieletroniki (GEPG), usimamizi na utunzaji wa mali za umma, taratibu za utoaji wa leseni za shughuli za madini na ushirikishwaji wa wananchi/wazawa katika shughuli za madini.

Maeneo mengine ni pamoja na ukaguzi wa madini na biashara, utatuzi wa migogoro katika sekta ya madini, taratibu za uwasilishaji wa taarifa makao makuu ya Tume na kwenye mamlaka nyingine zinazohusika, utunzaji wa siri katika utumishi wa umma, masuala ya utawala na rasilimaliwatu, sheria, kanuni na taratibu za fedha, usimamizi wa mifumo ya udhibiti wa ndani, maadili katika utumishi wa umma na mfumo wa uwazi wa upimaji utendaji kazi (OPRAS)

Alisema kuwa  kwa kuwa tume imepata watumishi wa kutosha inatakiwa kuunda kamati mbalimbali za kisheria na kitendaji kama vile kamati ya maadili, kamati ya ukaguzi, kamati ya ajira za kigeni na baraza la wafanyakazi ili kuifanya tume iweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza katika mafunzo hayo alimshukuru Waziri Kairuki kwa uteuzi wa watendaji wapya wa Tume ya Madini na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuyafanyia kazi yote watakayojifunza.

Wakati huohuo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi alisema kuwa mabadiliko ya sheria ya madini yaliyofanyika Tanzania ni hatua ya ushujaa na kuongeza kuwa mataifa mengine yameanza kujifunza.

Alisema kutokana na muhimu wa Sekta ya Madini kwenye mchango wa ukuaji wa uchumi wa nchi ameamua kufika mwenyewe kuja kutoa mafunzo kwa viongozi na maafisa waandamizi wa Tume ya Madini ili waweze kusimamia ipasavyo sekta hiyo kwa kutumia sheria na kanuni za madini.


Sehemu ya washiriki wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani) kwenye ufunguzi huo.

Kutoka kushoto, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya, Kamishna wa Tume ya Madini, Dk. Athanas Macheyeki wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani) kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kulia) akibadilishana mawazo na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) kwenye mafunzo hayo.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele) Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu waliokaa mbele) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ( kushoto waliokaa mbele), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, (wa pili kushoto waliokaa mbele) na  , Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga (wa pili kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Madini.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele) Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu waliokaa mbele) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ( kushoto waliokaa mbele), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, (wa pili kushoto waliokaa mbele) na  , Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga (wa pili kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji kutoka Tume ya Madini.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele) Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu waliokaa mbele) Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ( kushoto waliokaa mbele), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, (wa pili kushoto waliokaa mbele) na  , Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga (wa pili kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya (kushoto) akibadilishana mawazo na sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo.

Kaimu Mhasibu Mkuu wa Tume ya Madini, Avodia Lukonge (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkaguzi wa Ndani kutoka Tume ya  Madini, Happiness Shirima kabla ya kuanza kwa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Monday, August 6, 2018

Leseni za Madini sasa kutolewa kwa Masharti Magumu-Kairuki


Na Asteria Muhozya, Simanjiro

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema kuanzia sasa Serikali itaanza kutoa Leseni za madini biashara ya madini kwa masharti magumu huku ikimtaka kila mwombaji  kutoa taarifa za mauzo ya uzalishaji, usafirishaji pamoja na mnyororo mzima wa biashara ya madini ikiwemo fedha zinazoingia nchini kutokana na biashara hiyo.

Pia, ameiagiza Tume ya Madini kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha kila jambo katika mnyororo huo linasimamiwa kikamilifu na kuongeza kuwa, yeye kama waziri mwenye dhamana atahakikisha anafuatilia kila hatua itakayochukuliwa  na tume hiyo.

“Tume ichukue hatua. Nitakuwa na ninyi. Msiache hata mmoja atakayekwenda kinyume na haya. Nilifanya hivyo katika Sekta ya Utumishi wa Umma hata huku kwenye sekta ya madini, sitashindwa kufanya hivyo,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Waziri kairuki aliyasema hayo jana tarehe 3 Agosti, Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara wakati akipokea taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa kuchunguza mnyororo wa madini ya vito nchini.

Kamati hiyo ilifanya kazi yake kwa muda wa siku 30  kuanzia tarehe 26 Aprili, 2018 kwa  jukumu la kuchunguza  mnyororo wa madini ya vito  kuanzia kuzalisha hadi usafirishaji nje ya nchi pamoja na kubaini sababu za utoroshaji wa madini na kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuzuia utoroshaji.

Pia, aliiagiza tume ya madini kuanzia tarehe 4 Agosti, kuhakikisha inapata taarifa za uzalishaji za migodi yote inayozalisha huku akitaka migodi husika ieleze mahali inakouzia madini yao, anayeuziwa madini hayo na kuongeza kuwa, zoezi husika linawajumuisha pia dealers.

Waziri Kairuki alisema, wizara yake imeamua kusimamia suala husika ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli za kuhakikisha kuwa rasilimali madini zinawanufaisha watanzania wote.

“ Lazima watanzania tutambue kuwa madini haya yanamilikiwa na watanzania wote. Tunatakiwa kuyalinda kwa ajii ya maendeleo yetu na kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Kairuki.

Akizungumzia biashara ya madini ya tanzanite katika ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite mirerani, alisema hakuna serikali inayotaka watu wake wasifanye biashara, hivyo, lengo la ukuta huo ni kuhakikisha kwamba inadhibiti utoroshaji wa madini na kuweka mfumo mzuri ambao utawezesha madini hayo kuzinufaisha  pande zote.

Alisema tayari wizara imeandaa Kanuni za Mirerani (Mirerani Contolled Area) ambazo hivi sasa zinafanyiwa maboresho  baada ya kuwepo changamoto kadhaa katika utekelezaji wake.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema serikali imebaini  baadhi ya wenye leseni za ‘broker’ kukaribisha wageni kutoka nje kufanya biashara hiyo kinyume na taratibu na  hatimaye kusafirisha madini hayo, hivyo, aliwataka wote wanaofanya hivyo kuacha mara moja na kuwataka watanzania wote wenye taarifa kuhusu suala hilo kutoa taarifa  katika mamlaka zinazohusika.

“Kamati hii imefanya uzalendo na imefanya kazi kubwa sana. Nimeipokea taarifa ya kamati lakini natamani wangenitajia majina ya watoroshaji. Nilitamani sana kuona majina lakini naamini itaniuma sikio,” alisisitiza Waziri Kairuki.

Pia, aliongeza kuwa serikali itazifuta leseni za  uchimbaji madini kwa wale wote ambao wameshindwa kuyaendeleza maeneo yao na kupewa wengine wenye nia ya dhati ya kuendeleza shughuli za uchimbaji madini nchini.

Akizungumzia mkakati wa serikali katika kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani nchini, alisema kuwa serikali inaendelea kukiimarisha kituo cha TGC kilichopo jijini Arusha, kwa kuongeza wataalam katika masuala ya ukataji na unga’rishaji wa madini ya vito.
“Tayari tumepata walimu  7 kutoka nchini India, lakini bado tunafuatilia wengine kutoka nchini Thailand,”alisema Kairuki.

Akiwasilisha  taarifa ya Kamati kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo,  Mratibu wa Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC), Eric Mpesa alisema Kamati husika ilipata fursa ya kutembelea mgodi wa Mundarara mpaka wa Namanga, Uwanja wa ndege wa KIA, Machimbo ya Tanzanite Mirerani, TGC, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Morogoro na Machimbo ya Epanko, Morogoro.

Akiwasilisha mapendekezo ya kamati husika Mpesa alisema kuwa, kamati inapendekeza Serikali kutengeneza mpango wa makazi katika eneo lililozungushiwa ukuta wa Mirerani ikizingatia uwepo wa eneo la uchimbaji, biashara, uanzishwaji wa kituo cha One Stop Centre, huduma za kijamii, maegesho ya vyombo vya usafiri, maeneo ya starehe na maeneo ya utalii.

Pia, alisema serikali ihakikishe kuweka mfumo wa ulinzi katika eneo lililozungushiwa ukuta na pia ilishauri serikali kuongeza wataalam wa Wizara katika maeneo ya migodi ili kurahisisha ufanyaji biashara na kuwezesha kuzuia utoroshaji wa madini ya vito.

Pendekezo lingine ni serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata teknolojia za kisasa pamoja na tafiti za kijiolojia kufanywa na watalaam  kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa malipo ya gharama nafuu yatakayolipwa  baada ya uzalishaji kupatikana.

Pia, Kamati ilipendekeza seriakali kuishawishi mifuko ya jamii isaidie wadau  kuanzisha benki ya Madini itakayowapa wachimbaji na wafanyabiashara mikopo yenye masharti nafuu.

Akizungumzia mcchango wa sekta ya madini, alisema sekta hiyo inachangia fedha za kigeni cha kiasi cha wastani wa dola za Marekani milioni 27.8 kwa mwaka isipokuwa almasi na kati ya hizo, asilimia 27.8 ni madini yaliyosanifiwa na kunga’rishwa na asilimia 71.3 ni madini ghafi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara  Alexander  Mnyeti alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikichazewa kwa wadau katika migodi kutokulipa kodi stahiki za serikali.

Aliishauri wizara kufuta leseni za wale wote walioohodhi maeneo yao bila kuyafanyia kazi ili kuwezesha leseni husika kutumiwa na wengine wenye nia ya kuendeleza sekta ya madini.

Kuhusu suala la mikataba  ya ajira katika migodi hiyo aliishauri serikali na wadau kukaa pamoja na kujadili suala husika na kulitafutia ufumbuzi.

Kamati iliyoandaa taarifa husika ilikuwa na wajumbe 13 ikiongozwa na Mwenyekiti Sammy Mollel, Makamu Mwenyekiti Hamis Kim, Katibu Adam Rashid pamoja na wajumbe 10 na Sekretarieti.

Wajumbe wa Kamati hiyo walitoka TAMIDA, MAREMA, AREMA, RUVREMA, TAWOMA, BROKER pamoja na wajumbe kutoka Wizara ya Madini na TGC.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (kushoto) akiteta jambo na Mbunge wa Simanjiro James Ole Milya (katikati) na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhandisi Tumain Magesa (kulia). 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na Wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini na wabunge wengine wa Mkoa wa Manyara, Kilimanjaro na Arusha. 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akifurahia jambo na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Manyara. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na kusshoto ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo. 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na Kamati iliyochunguza mnyororo wa madini ya vito  kuanzia kuzalisha hadi usafirishaji nje ya nchi pamoja na kubaini sababu za utoroshaji wa madini na kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuzuia utoroshaji. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Vyama vya Wachimbaji madini.

Friday, August 3, 2018

Serikali kuweka mbinu za kisasa ulinzi Mirerani


Na Asteria Muhozya, Simanjiro

Serikali imesema inajiandaa kuja na mbinu za kisasa zaidi za ukaguzi na ulinzi katika ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite, Mirerani  ili kudhibiti utoroshaji wa madini hayo yanayopatikana Wilayani Simanjiro Mkoa wa   Manyara.

Hayo  yalisemwa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki  tarehe 2 Agosti, 2018 wakati wa mkutano wa hadhara ulishirikisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wauzaji na wote wanaofanya shughuli zao za ndani ya ukuta huo.

Alisema, mabadiliko ya ujenzi wa ukuta huo ni chanya ambayo yamelenga kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini ili kuongeza mchango wa sekta husika katika pato la taifa.

Waziri Kairuki alieleza  ili shughuli za uuzaji na ununuzi ziweze kufanyika ndani ya eneo hilo, tayari Serikali imejenga sehemu maalum kwa ajili ya shughuli  hizo na kuongeza, “ baada ya kukamilika jengo hilo kutakuwa na sehemu kwa ajili ya Broker kufanyia shughuli zao hapo hapo ndani ya ukuta.”

Aliongeza, tayari Mkataba wa ujenzi wa Kituo cha kufanyia shughuli zote zinazohusu biashara ya madini ya tanzanite kwa ujumla (One Stop Center) umekwishakabidhiwa na ndani ya muda mfupi ujao, ujenzi wa jengo husika utaanza.

Akitoa ufafanuzi kuhusu taratibu za kuingia na kufanya shughuli za uchimbaji ndani ya ukuta, Waziri Kairuki alisema taratibu za ukaguzi zinalenga katika kudhibiti utoroshaji madini na hivyo kuwataka wadau wote kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la ukaguzi katika ukuta huo na kuongeza kuwa, aina ya ukaguzi unaofanywa kwa sasa ni wa muda mpaka hapo taratibu maalum za ukaguzi zitakapokuwa tayari.

Akitoa ufafanuzi kuhusu wazawa wenye leseni za uuzaji kulipa ada kwa  kutumia Dola za Marekani, Waziri Kairuki alieleza kuwa, kwa kuwa Kanuni za eneo la Mirerani zimeandaliwa na Waziri mwenye dhamana na sekta, suala hilo litafanyiwa kazi ili kipengele husika kiweze kufanyiwa marekebisho na hivyo kuwawezesha kulipia kwa fedha za Tanzania. Pia, aliongeza kuwa, katika kipindi hiki ambacho mabadiliko hayo hayajafanyika, wahusika watalazimika kuendelea na utaratibu uliopo.

Ili kuongeza kasi ya shughuli ya uthamini wa madini hayo, waziri Kairuki alisema wizara yake itaongeza idadi ya wataalam kutoka mmoja hadi wanne ili kuongeza kasi ya kufanya shughuli husika.

Pia, Waziri Kairuki aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya wafanyakazi katika migodi yao na kuongeza kuwa, suala la maslahi ya watumishi ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na wadau wote katika sekta husika.

“Maslahi ya wafanyakazi yanatakiwa kuwa namba moja. Mimi ni Mbunge niliyechaguliwa kupitia umoja wa vyama vya wafanyakazi hivyo suala la maslahi ya wafanyakazi lazima nilisimamie kikamilifu,” alisisitiza Kairuki.

Akizungumzia suala la usafiri ndani ya ukuta, alisema zoezi husika litaendelea kama ilivyo sasa na kutumia fursa hiyo kukaribisha wawekezaji zaidi katika huduma ya kutoa  huduma ya usafiri ndani ya ukuta huo.

Pia, alitumia fursa hiyo kuwataka wadau wote katika eneo hilo kuwa waaminifu na kushirikiana na serikali na hususan ofisi ya Madini katika kutoa taarifa za utoroshaji madini hayo.

Mwisho aliwataka Maafisa Madini  kuendelea kutoa elimu ya Sheria ya Madini pamoja na taratibu zake pia, Mbunge wa eneo husika aendelee kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ukuta huo ili kuwawezesha wadau wote kuwa na uelewa wa pamoja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro James Ole Milya, alisema alimweleza Waziri Kairuki kuwa kero kubwa katika eneo husika ni baina ya wamiliki wa migodi na wafanyakazi na hivyo kumtaka Waziri kuona namna ya kushughulikia suala hilo.

Pia, alipendekeza kuundwa kwa kamati mbili moja ikiwa ya wamiliki na wafanyakazi kwa lengo la kuondoa mvutano uliopo sasa kati ya pande mbili.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akisisitiza jambo wakati akizungumza na  katika mkutano wa hadhara na wananchi wanaofanya shughuli zao ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, mirerani.  Wanaofuatilia mbele ni Mbunge wa Simanjiro James Ole Milya (kulia) na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Tumain Magesa.
Sehemu ya wananchi waliofika katika mkutano wa hadhara ambao ulijumuisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wauzaji, wanunuzi na wanaofanya shughuli mmbalimbali ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, Mireran wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki, hayupo pichani.

Sehemu ya wananchi waliofika katika mkutano wa hadhara ambao ulijumuisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wauzaji, wanunuzi na wanaofanya shughuli mmbalimbali ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, Mireran wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki, hayupo pichani.

Sehemu ya wananchi waliofika katika mkutano wa hadhara ambao ulijumuisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wauzaji, wanunuzi na wanaofanya shughuli mmbalimbali ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, Mireran wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki, hayupo pichani.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumain Magesa akieleza jambo wakati wa mkutano wa hadhara kati ya Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani) na wadau wa madini ya tanzanite wanaofanya shughuli zao ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, mirerani. Wanaofuatilia ni wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wadau wanaofanya shughuli zao ndani ya ukuta wakitaka kusilisha malalamiko yao kwa Waziri  Kairuki.

Naona fahari uwekezaji wa Mwanga Gems-Kairuki


Na Asteria Muhozya, Simanjiro

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema anaona fahari kutokana na uwekezaji wa Kiwanda cha Kuchakata madini ya Kinywe (Graphite) uliofanywa na Kampuni ya wazawa ya GOD Mwanga Gems Ltd iliyopo Kata ya Endiamtu, Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 2 Agosti, alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kujionea shughuli zinazofanywa na kiwandani hapo.

Amesema Serikali imekuwa ikihamasisha waombaji wa leseni za madini kuwekeza katika maeneo mbalimbali hivyo, jambo lililofanywa na kiwanda hicho ikiwemo malengo ya kiwanda husika kufungua  viwanda vingine katika mikoa ya Tanga na Manyara ni jambo la kujivunia na fahari kwa Tanzania.

“Nimefurahishwa sana namna kampuni hii inavyofanya kazi. Serikali kupitia wizara yangu imekuwa ikihamasisha uwekezaji. Tuko tayari kuwasimamia na kuwasaidia katika hili. Tunataka kutengeneza ajira zaidi, kukuza uchumi kupitia madini lakini pia serikali kupata kodi,” amesisitiza Kairuki.

Akijibu ombi la kampuni hiyo kupata kibali cha kuuza madini hayo nje, Waziri Kairuki ameahidi kampuni hiyo kuwa mara baada ya taratibu za utoaji vibali kukamilika Wizara kupitia Tume ya Madini itatoa kibali kwa kampuni husika iendelee na taratibu zake za  kuuzwa nje ya nchi madini hayo.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Kairuki amewataka wenye leseni za madini kutozitumia leseni hizo kuziweka rehani kwa kuwa Sheria ya Madini inakataza jambo hilo badalayake zinatakiwa kutumiwa katika malengo yaliyokusudiwa.

“Wapo baadhi ya wawekezaji wamepewa leseni lakini hawajafanya chochote wengine wanaweka rehani leseni hizi. Nafurahi kuona mzawa mwenzetu amefanya jambo kubwa kama hili, leo nimejionea uhalisia  katika jambo hili,” amesema Waziri Kairuki.

Pia, Waziri Kairuki ameishauri kampuni husika kuendelea kuitumia Maabara ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST) kwa ajili ya shughuli za utafiti na pia kuwatumia wahitimu wa Chuo Cha Madini Dodoma (MRI) katika suala la ajira.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amesema Wizara imewachukulia hatua watumishi 40 kutokana na kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma katika suala zima la usimamizi katika sekta husika.

“Wapo tuliowahamisha vituo vya kazi, wengine tumewasimamisha. Tunachotaka ni kuendana na kasi na huku wakizingatia maadili ya utumishi,” amesema Waziri Kairuki.

Aidha, amesisitiza suala la wawekezaji kuendelea kutoa taarifa za uzalishaji ili  serikali iweze  kupata kodi zake  huku akisisitiza suala la ulipaji kodi  kwa serikali na wenye leseni zao kuzitumia na kuzalisha kwa viwango vinavyohitajika.

Kwa upande, Meneja wa Kiwanda hicho Henry Mbando ameiomba serikali kukisaidia kiwanda hicho kupata kibali kwa ajili ya kuuza madini hayo nje ya nchi ambayo yana masoko katika nchi za Marekani, Kanada, China na ulaya.

Ameongeza kuwa, madini hayo yanatumika kutengeneza bidhaa mbalimbali  za viwandani vikiwemo vipuri vya magari, betri za magari na mitambo mengine.

Ameongeza kuwa, soko la madini hayo ni katika nchi za
Akizungumzia idadi ya wafanyakazi waliopo kiwandani hapo amesema kiwanda kina jumla ya watumishi 80 huku waanawake wakiwa 2 na wanaume 78.

Naye, Mmiliki wa kampuni hiyo, Godlisten Mwanga ameishukuru Serikali kwa msamaha wa kodi katika baadhi ya mitambo aliyoinunu kwa ajili ya kiwanda hicho na pia kumshukuru waziri Kairuki kwa kuona umuhimu wa kutembelea kiwanda husika.

Amesema kiwanda hicho kimezalisha tani zaidi ya 2,000 na zilizotayari kwa ajili ya kuuzwa ni tani 200.

Akizungumzia suala la kibali kwa kampuni husika Kamishna wa Madini Mhandisi David Mlabwa amesema kuwa, awali kampuni hiyo ilikuwa haijakidhi vigezo vya kupata kibali lakini baada ya kukidhi viwango hivyo itapatiwa kibali.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki (katikati) akitembelea maeneo mbalimbali katika kiwanda cha Kuchakata Madini ya Graphite cha GodMwanga Gems Ltd. Wa kwanza kulia ni Mmiliki wa kiwanda hicho Godlisten Mwanga na wa kwanza kuli kwa waziri ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Tumaini Magesa.

Mmiliki wa kampuni ya God Mwanga Gems Ltd.Godlisten (kulia) Mwanga akimwonesha Waziri wa Madini Angellah Kairuki madini ya Grahite ambayo tayari yamechakatwa.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki (katikati) akipita katika maeneo mbalimbali ya kiwanda cha God Mwanga Gems Ltd kuona namna shughuli mbalimbali za uchakataji wa madini ya Kinywe zinavyofanyika.

Kamati ya ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini yaanza kupitia mipango ya kampuni zilizoomba leseni za madini


Na Greyson Mwase

Leo tarehe 02 Agosti, 2018 Kamati ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) imekutana jijini Dodoma kwa ajili ya kupitia mipango ya ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini iliyowasilishwa na kampuni za uchimbaji wa madini nchini zilizoomba leseni za madini.


Kikao kwa ajili ya upitiaji wa mipango ya ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini iliyowasilishwa na kampuni za uchimbaji wa madini nchini zilizoomba leseni za madini kikiendelea.
Kutoka kushoto Mkurugenzi wa Idara ya Leseni na TEHAMA kutoka Tume ya Madini, Terence Ngole, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria kutoka Wizara ya Madini, Edwin Igenge na Kamishna wa Kazi kutoka  Ofisi ya  Waziri Mkuu ( Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu), Hilda Kabissa wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Kamishna- Tume ya Madini, Dk. Athanas Macheyeki (hayupo pichani).

Katibu Mtendaji – Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kulia) akieleza jambo kwenye kikao hicho. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Athanas Macheyeki.

Kutoka kushoto Afisa Biashara kutoka Tume ya Madini, Issa Lunda, Meneja wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Tume ya Madini, Miriam Mbaga wakifuatilia majadiliano yaliyokuwa yanaendelea katika kikao hicho.

Thursday, August 2, 2018

Watoroshaji Tanzanite kiama kinakuja-Waziri Kairuki


Na Asteria Muhozya, Simanjiro

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema Serikali itaaendelea kusimamia  ulinzi  na kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite na watakaokwenda  kinyume na matakwa ya Sheria, kiama chao  kinakuja.

Waziri Kairuki aliyasema hayo tarehe 1 Agosti wakati wa ziara yake mkoani Manyara wakati alipotembelea migodi mbalimbali ya madini  ya tanzanite ndani ya ukuta wa Mirerani.

Alisema ziara hiyo ililenga kuangalia suala zima la ulinzi katika ukuta unaozunguka migodi  ya tanzanite, shughuli za uchimbaji madini  mengine zinavyofanyika na kuangalia namna uzalishaji wa madini ya tanzanite  unavyoendelea katika migodi husika.

Kairuki aliongeza kuwa, ziara hiyo ililenga  kuangalia namna Sheria ya Madini inavyotekelezwa, masuala ya Mikataba ya watumishi katika migodi  na namna migodi husika inavyolipa  kodi  mbalimbali za Serikali  yakiwemo masuala ya usalama sehemu za kazi na  wafanyakazi kwa ujumla.

“Utoroshaji madini hausaidii, fedha ni za haraka lakini zinawaadhibu watanzania walio wengi kwa kuwa, fedha hizo hizo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo. Hivyo, kila mtanzania awe mlizi wa mwenzake,” alisema Kairuki.

Awali, akizungumza  katika eneo Lemshuku kunakofanyika shughuli za uchimbaji wa madini ya Green Garnet, waziri Kairuki alisema kuwa, serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo katika kuchangia pato la taifa kupitia shughuli za uchimbaji, hivyo akawaasa wachimbaji nchini kufuata Sheria, kanuni na taratibu ili kufanya shughuli halali ikiwemo kulipa kodi stahiki.

Akizungmzia suala la ruzuku kwa wachimbaji wadogo, waziri Kairuki alisema hivi sasa serikali imesitisha kwa muda utoaji rukuzu kwa kuwa inaandaa utaratibu wa wazi na endelevu ambao utawezesha wachimbaji  na serikali kunufaika kupitia rasilimali madini.

Aliongeza kuwa, serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa shughuli za uchimbaji mdogo wa madini ikiwemo kuhakikisha kuwa inawawezesha wachimbaji kutoka uchimbaji mdogo kwenda katika uchimbaji wa kati na kuongeza, “tayari tumetenga maeneo zaidi ya 44 kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Akitolea ufafanuzi suala la vibarua katika migodi ya madini, aliwataka wale wote wanaofanya vibarua katika maeneo hayo kuhakikisha kuwa, wanapata mikataba yao kabla ya kuanza kazi.

Kuhusu masuala ya utoaji leseni za uchimbaji madini, Waziri Kairuki  alisema   ndani ya kipindi cha wiki 2 Tume ya Madini itaanza kutoa leseni kwa waombaji waliokidhi vigezo na kuongeza kuwa, kwa wanaomiliki leseni bila kuziendeleza watanyang’nywa na hivyo akawaasa wamiliki wasiokuwa na uwezo wa kuendeleza maeneo yao kutoa tarifa ili waweze kuunganishwa na wenye uwezo wa kuwekeza waweze kushirikiana.

Pia, waziri Kairuki alihamasisha kuhusu uwekezaji katika mashine za kukata na kunga’risha madini ili kuwezesha shughuli hizo kufanyika nchini na kuongeza kuwa, kupitia Sheria Mpya ya Madini  hairuhusu yoyote kusafirisha madini ghafi nje ya nchi.

Kwa upande wake,  Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mlabwa, alisema  ni lazima Sheria, Kanuni na taratibu zizingatiwe wakati wa utekelezaji shughuli za uchimbaji madini na kuongeza kuwa, serikali inatambua mchango wa kila aina ya madini yanayopatikana nchini.

Naye, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Tumaini Magesa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto alisema kuwa, shughuli za uchimbaji katika eneo la Mirerani zinaendelea na hivyo serikali itaendelea kuboresha ulinzi na kuhakikisha kwamba unaimalika.


Waziri wa Madini Angellaha Kairuki akipima ubora wa madini ya Tanzanite katika kifaa maalum baada ya kuzalishwa kutoka katika mgodi wa moja ya wachimbaji madini ya tanzanite. 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia madini ya Green Garnet alipotembelea moja ya migodi inayochimba madini hayo katika eneo la Lemshuku Wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara wakati wa zira yake. 

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akieleza jambo wakati akipata ufafanuzi kutoka kwa mchimbaji (aliye ndani ya shimo) wakati alipotembelea moja ya migodi ya madini ya Green Garnet katika eneo la Lemshuku wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara.
Sehemu ya wachimbaji katika eneo la Lemshuku Wilayani Simanjiro kunakofanyika shughuli za uchimbaji madini ya Green Garnet wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki hayupo pichani wakati wa ziara yake katika eneo hilo.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiteta jambo na Kamishna wa Madini Mhandisi David Mlabwa (kulia) mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Kilimanjaro tayari kwa kuanza ziara ya kikazi mkoani Manyara. Wanaofuatilia ni baadhi viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Manyara na Wataalam kutoka  Wizara ya Madini.

Waziri wa Madini akiteta jambo wakati alipotembelea mgodi wa Franone Mining & Gems Co. Ltd uliopo ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, Mirerani.