Na Asteria Muhozya,
Simanjiro
Serikali imesema
inajiandaa kuja na mbinu za kisasa zaidi za ukaguzi na ulinzi katika ukuta
unaozunguka migodi ya Tanzanite, Mirerani ili kudhibiti utoroshaji wa madini hayo yanayopatikana
Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Madini Angellah
Kairuki tarehe 2 Agosti, 2018 wakati wa
mkutano wa hadhara ulishirikisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wauzaji na
wote wanaofanya shughuli zao za ndani ya ukuta huo.
Alisema, mabadiliko
ya ujenzi wa ukuta huo ni chanya ambayo yamelenga kukuza uchumi wa nchi kupitia
sekta ya madini ili kuongeza mchango wa sekta husika katika pato la taifa.
Waziri Kairuki
alieleza ili shughuli za uuzaji na
ununuzi ziweze kufanyika ndani ya eneo hilo, tayari Serikali imejenga sehemu
maalum kwa ajili ya shughuli hizo na
kuongeza, “ baada ya kukamilika jengo hilo kutakuwa na sehemu kwa ajili ya Broker kufanyia shughuli zao hapo hapo
ndani ya ukuta.”
Aliongeza, tayari Mkataba
wa ujenzi wa Kituo cha kufanyia shughuli zote zinazohusu biashara ya madini ya
tanzanite kwa ujumla (One Stop Center) umekwishakabidhiwa na ndani ya muda
mfupi ujao, ujenzi wa jengo husika utaanza.
Akitoa ufafanuzi kuhusu
taratibu za kuingia na kufanya shughuli za uchimbaji ndani ya ukuta, Waziri
Kairuki alisema taratibu za ukaguzi zinalenga katika kudhibiti utoroshaji
madini na hivyo kuwataka wadau wote kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la
ukaguzi katika ukuta huo na kuongeza kuwa, aina ya ukaguzi unaofanywa kwa sasa
ni wa muda mpaka hapo taratibu maalum za ukaguzi zitakapokuwa tayari.
Akitoa ufafanuzi kuhusu
wazawa wenye leseni za uuzaji kulipa ada kwa
kutumia Dola za Marekani, Waziri Kairuki alieleza kuwa, kwa kuwa Kanuni
za eneo la Mirerani zimeandaliwa na Waziri mwenye dhamana na sekta, suala hilo
litafanyiwa kazi ili kipengele husika kiweze kufanyiwa marekebisho na hivyo
kuwawezesha kulipia kwa fedha za Tanzania. Pia, aliongeza kuwa, katika kipindi
hiki ambacho mabadiliko hayo hayajafanyika, wahusika watalazimika kuendelea na
utaratibu uliopo.
Ili kuongeza kasi ya
shughuli ya uthamini wa madini hayo, waziri Kairuki alisema wizara yake
itaongeza idadi ya wataalam kutoka mmoja hadi wanne ili kuongeza kasi ya
kufanya shughuli husika.
Pia, Waziri Kairuki
aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya wafanyakazi
katika migodi yao na kuongeza kuwa, suala la maslahi ya watumishi ni jambo
ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na wadau wote katika sekta husika.
“Maslahi ya
wafanyakazi yanatakiwa kuwa namba moja. Mimi ni Mbunge niliyechaguliwa kupitia
umoja wa vyama vya wafanyakazi hivyo suala la maslahi ya wafanyakazi lazima
nilisimamie kikamilifu,” alisisitiza Kairuki.
Akizungumzia suala la
usafiri ndani ya ukuta, alisema zoezi husika litaendelea kama ilivyo sasa na
kutumia fursa hiyo kukaribisha wawekezaji zaidi katika huduma ya kutoa huduma ya usafiri ndani ya ukuta huo.
Pia, alitumia fursa
hiyo kuwataka wadau wote katika eneo hilo kuwa waaminifu na kushirikiana na
serikali na hususan ofisi ya Madini katika kutoa taarifa za utoroshaji madini
hayo.
Mwisho aliwataka
Maafisa Madini kuendelea kutoa elimu ya
Sheria ya Madini pamoja na taratibu zake pia, Mbunge wa eneo husika aendelee
kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ukuta huo ili kuwawezesha
wadau wote kuwa na uelewa wa pamoja.
Kwa upande wake,
Mbunge wa Simanjiro James Ole Milya, alisema alimweleza Waziri Kairuki kuwa
kero kubwa katika eneo husika ni baina ya wamiliki wa migodi na wafanyakazi na
hivyo kumtaka Waziri kuona namna ya kushughulikia suala hilo.
Pia, alipendekeza
kuundwa kwa kamati mbili moja ikiwa ya wamiliki na wafanyakazi kwa lengo la
kuondoa mvutano uliopo sasa kati ya pande mbili.
No comments:
Post a Comment