Na
Asteria Muhozya, Simanjiro
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki amesema anaona fahari kutokana na uwekezaji wa Kiwanda cha Kuchakata
madini ya Kinywe (Graphite) uliofanywa na Kampuni ya wazawa ya GOD Mwanga Gems
Ltd iliyopo Kata ya Endiamtu, Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Waziri Kairuki
ameyasema hayo leo tarehe 2 Agosti, alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la
kujionea shughuli zinazofanywa na kiwandani hapo.
Amesema Serikali
imekuwa ikihamasisha waombaji wa leseni za madini kuwekeza katika maeneo
mbalimbali hivyo, jambo lililofanywa na kiwanda hicho ikiwemo malengo ya
kiwanda husika kufungua viwanda vingine katika
mikoa ya Tanga na Manyara ni jambo la kujivunia na fahari kwa Tanzania.
“Nimefurahishwa sana
namna kampuni hii inavyofanya kazi. Serikali kupitia wizara yangu imekuwa ikihamasisha
uwekezaji. Tuko tayari kuwasimamia na kuwasaidia katika hili. Tunataka
kutengeneza ajira zaidi, kukuza uchumi kupitia madini lakini pia serikali
kupata kodi,” amesisitiza Kairuki.
Akijibu ombi la
kampuni hiyo kupata kibali cha kuuza madini hayo nje, Waziri Kairuki ameahidi
kampuni hiyo kuwa mara baada ya taratibu za utoaji vibali kukamilika Wizara
kupitia Tume ya Madini itatoa kibali kwa kampuni husika iendelee na taratibu
zake za kuuzwa nje ya nchi madini hayo.
Kufuatia hali hiyo,
Waziri Kairuki amewataka wenye leseni za madini kutozitumia leseni hizo
kuziweka rehani kwa kuwa Sheria ya Madini inakataza jambo hilo badalayake
zinatakiwa kutumiwa katika malengo yaliyokusudiwa.
“Wapo baadhi ya wawekezaji
wamepewa leseni lakini hawajafanya chochote wengine wanaweka rehani leseni
hizi. Nafurahi kuona mzawa mwenzetu amefanya jambo kubwa kama hili, leo
nimejionea uhalisia katika jambo hili,”
amesema Waziri Kairuki.
Pia, Waziri Kairuki
ameishauri kampuni husika kuendelea kuitumia Maabara ya Taasisi ya Jiolojia na
Utafiti Tanzania (GST) kwa ajili ya shughuli za utafiti na pia kuwatumia
wahitimu wa Chuo Cha Madini Dodoma (MRI) katika suala la ajira.
Katika hatua
nyingine, Waziri Kairuki amesema Wizara imewachukulia hatua watumishi 40
kutokana na kwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma katika suala zima la
usimamizi katika sekta husika.
“Wapo tuliowahamisha
vituo vya kazi, wengine tumewasimamisha. Tunachotaka ni kuendana na kasi na
huku wakizingatia maadili ya utumishi,” amesema Waziri Kairuki.
Aidha, amesisitiza
suala la wawekezaji kuendelea kutoa taarifa za uzalishaji ili serikali iweze kupata kodi zake huku akisisitiza suala la ulipaji kodi kwa serikali na wenye leseni zao kuzitumia na
kuzalisha kwa viwango vinavyohitajika.
Kwa upande, Meneja wa
Kiwanda hicho Henry Mbando ameiomba serikali kukisaidia kiwanda hicho kupata
kibali kwa ajili ya kuuza madini hayo nje ya nchi ambayo yana masoko katika
nchi za Marekani, Kanada, China na ulaya.
Ameongeza kuwa, madini
hayo yanatumika kutengeneza bidhaa mbalimbali za viwandani vikiwemo vipuri vya magari, betri
za magari na mitambo mengine.
Ameongeza kuwa, soko
la madini hayo ni katika nchi za
Akizungumzia idadi ya
wafanyakazi waliopo kiwandani hapo amesema kiwanda kina jumla ya watumishi 80
huku waanawake wakiwa 2 na wanaume 78.
Naye, Mmiliki wa
kampuni hiyo, Godlisten Mwanga ameishukuru Serikali kwa msamaha wa kodi katika
baadhi ya mitambo aliyoinunu kwa ajili ya kiwanda hicho na pia kumshukuru
waziri Kairuki kwa kuona umuhimu wa kutembelea kiwanda husika.
Amesema kiwanda hicho
kimezalisha tani zaidi ya 2,000 na zilizotayari kwa ajili ya kuuzwa ni tani
200.
Akizungumzia suala la
kibali kwa kampuni husika Kamishna wa Madini Mhandisi David Mlabwa amesema
kuwa, awali kampuni hiyo ilikuwa haijakidhi vigezo vya kupata kibali lakini
baada ya kukidhi viwango hivyo itapatiwa kibali.
Mmiliki wa
kampuni ya God Mwanga Gems Ltd.Godlisten (kulia) Mwanga akimwonesha Waziri wa
Madini Angellah Kairuki madini ya Grahite ambayo tayari yamechakatwa.
|
Waziri wa
Madini Angellah Kairuki (katikati) akipita katika maeneo mbalimbali ya kiwanda
cha God Mwanga Gems Ltd kuona namna
shughuli mbalimbali za uchakataji wa madini ya Kinywe zinavyofanyika.
|
No comments:
Post a Comment