Na
Asteria Muhozya, Simanjiro
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki amesema kuanzia sasa Serikali itaanza kutoa Leseni za madini biashara
ya madini kwa masharti magumu huku ikimtaka kila mwombaji kutoa taarifa za mauzo ya uzalishaji,
usafirishaji pamoja na mnyororo mzima wa biashara ya madini ikiwemo fedha
zinazoingia nchini kutokana na biashara hiyo.
Pia, ameiagiza Tume
ya Madini kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha kila jambo katika mnyororo huo
linasimamiwa kikamilifu na kuongeza kuwa, yeye kama waziri mwenye dhamana
atahakikisha anafuatilia kila hatua itakayochukuliwa na tume hiyo.
“Tume ichukue hatua.
Nitakuwa na ninyi. Msiache hata mmoja atakayekwenda kinyume na haya. Nilifanya
hivyo katika Sekta ya Utumishi wa Umma hata huku kwenye sekta ya madini,
sitashindwa kufanya hivyo,” alisisitiza Waziri Kairuki.
Waziri kairuki
aliyasema hayo jana tarehe 3 Agosti, Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara wakati
akipokea taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa kuchunguza mnyororo wa madini ya
vito nchini.
Kamati hiyo ilifanya
kazi yake kwa muda wa siku 30 kuanzia tarehe
26 Aprili, 2018 kwa jukumu la
kuchunguza mnyororo wa madini ya
vito kuanzia kuzalisha hadi usafirishaji
nje ya nchi pamoja na kubaini sababu za utoroshaji wa madini na kupendekeza
hatua za kuchukuliwa ili kuzuia utoroshaji.
Pia, aliiagiza tume
ya madini kuanzia tarehe 4 Agosti, kuhakikisha inapata taarifa za uzalishaji za
migodi yote inayozalisha huku akitaka migodi husika ieleze mahali inakouzia
madini yao, anayeuziwa madini hayo na kuongeza kuwa, zoezi husika linawajumuisha
pia dealers.
Waziri Kairuki
alisema, wizara yake imeamua kusimamia suala husika ikiwa ni jitihada za kuunga
mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Magufuli za kuhakikisha kuwa rasilimali madini zinawanufaisha watanzania wote.
“ Lazima watanzania
tutambue kuwa madini haya yanamilikiwa na watanzania wote. Tunatakiwa kuyalinda
kwa ajii ya maendeleo yetu na kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Kairuki.
Akizungumzia biashara
ya madini ya tanzanite katika ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite mirerani,
alisema hakuna serikali inayotaka watu wake wasifanye biashara, hivyo, lengo la
ukuta huo ni kuhakikisha kwamba inadhibiti utoroshaji wa madini na kuweka mfumo
mzuri ambao utawezesha madini hayo kuzinufaisha pande zote.
Alisema tayari wizara
imeandaa Kanuni za Mirerani (Mirerani Contolled Area) ambazo hivi sasa
zinafanyiwa maboresho baada ya kuwepo
changamoto kadhaa katika utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine,
Waziri Kairuki alisema serikali imebaini
baadhi ya wenye leseni za ‘broker’ kukaribisha wageni kutoka nje kufanya
biashara hiyo kinyume na taratibu na
hatimaye kusafirisha madini hayo, hivyo, aliwataka wote wanaofanya hivyo
kuacha mara moja na kuwataka watanzania wote wenye taarifa kuhusu suala hilo
kutoa taarifa katika mamlaka
zinazohusika.
“Kamati hii imefanya
uzalendo na imefanya kazi kubwa sana. Nimeipokea taarifa ya kamati lakini
natamani wangenitajia majina ya watoroshaji. Nilitamani sana kuona majina
lakini naamini itaniuma sikio,” alisisitiza Waziri Kairuki.
Pia, aliongeza kuwa
serikali itazifuta leseni za uchimbaji
madini kwa wale wote ambao wameshindwa kuyaendeleza maeneo yao na kupewa
wengine wenye nia ya dhati ya kuendeleza shughuli za uchimbaji madini nchini.
Akizungumzia mkakati
wa serikali katika kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani nchini, alisema
kuwa serikali inaendelea kukiimarisha kituo cha TGC kilichopo jijini Arusha,
kwa kuongeza wataalam katika masuala ya ukataji na unga’rishaji wa madini ya
vito.
“Tayari tumepata
walimu 7 kutoka nchini India, lakini
bado tunafuatilia wengine kutoka nchini Thailand,”alisema Kairuki.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati kwa niaba ya Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Mratibu wa Kituo cha Jimolojia
Tanzania (TGC), Eric Mpesa alisema Kamati husika ilipata fursa ya kutembelea
mgodi wa Mundarara mpaka wa Namanga, Uwanja wa ndege wa KIA, Machimbo ya
Tanzanite Mirerani, TGC, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Morogoro na Machimbo ya
Epanko, Morogoro.
Akiwasilisha
mapendekezo ya kamati husika Mpesa alisema kuwa, kamati inapendekeza Serikali
kutengeneza mpango wa makazi katika eneo lililozungushiwa ukuta wa Mirerani
ikizingatia uwepo wa eneo la uchimbaji, biashara, uanzishwaji wa kituo cha One Stop Centre, huduma za kijamii,
maegesho ya vyombo vya usafiri, maeneo ya starehe na maeneo ya utalii.
Pia, alisema serikali
ihakikishe kuweka mfumo wa ulinzi katika eneo lililozungushiwa ukuta na pia
ilishauri serikali kuongeza wataalam wa Wizara katika maeneo ya migodi ili
kurahisisha ufanyaji biashara na kuwezesha kuzuia utoroshaji wa madini ya vito.
Pendekezo lingine ni
serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata teknolojia za kisasa pamoja na
tafiti za kijiolojia kufanywa na watalaam
kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa
malipo ya gharama nafuu yatakayolipwa
baada ya uzalishaji kupatikana.
Pia, Kamati
ilipendekeza seriakali kuishawishi mifuko ya jamii isaidie wadau kuanzisha benki ya Madini itakayowapa
wachimbaji na wafanyabiashara mikopo yenye masharti nafuu.
Akizungumzia mcchango
wa sekta ya madini, alisema sekta hiyo inachangia fedha za kigeni cha kiasi cha
wastani wa dola za Marekani milioni 27.8 kwa mwaka isipokuwa almasi na kati ya
hizo, asilimia 27.8 ni madini yaliyosanifiwa na kunga’rishwa na asilimia 71.3
ni madini ghafi.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa
ikichazewa kwa wadau katika migodi kutokulipa kodi stahiki za serikali.
Aliishauri wizara
kufuta leseni za wale wote walioohodhi maeneo yao bila kuyafanyia kazi ili
kuwezesha leseni husika kutumiwa na wengine wenye nia ya kuendeleza sekta ya
madini.
Kuhusu suala la mikataba ya ajira katika migodi hiyo aliishauri
serikali na wadau kukaa pamoja na kujadili suala husika na kulitafutia
ufumbuzi.
Kamati iliyoandaa
taarifa husika ilikuwa na wajumbe 13 ikiongozwa na Mwenyekiti Sammy Mollel,
Makamu Mwenyekiti Hamis Kim, Katibu Adam Rashid pamoja na wajumbe 10 na
Sekretarieti.
Wajumbe wa Kamati
hiyo walitoka TAMIDA, MAREMA, AREMA, RUVREMA, TAWOMA, BROKER pamoja na wajumbe
kutoka Wizara ya Madini na TGC.
![]() |
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti (kushoto) akiteta jambo na Mbunge wa
Simanjiro James Ole Milya (katikati) na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhandisi
Tumain Magesa (kulia).
![]() |
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na Wabunge wa Kamati ya
Nishati na Madini na wabunge wengine wa Mkoa wa Manyara, Kilimanjaro na Arusha.
![]() |
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki akifurahia jambo na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi
Mkoa wa Manyara. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na kusshoto
ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
![]() |
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa Vyama
vya Wachimbaji madini.
|
No comments:
Post a Comment