Monday, September 10, 2018

Prof. Kikula aagiza kikundi cha wachimbaji madini kupewa leseni ndani ya mwezi mmoja


Na Greyson Mwase, Dodoma

Septemba 06, 2018

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amemwagiza Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA),  Kulwa Mkalimoto na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya kuhakikisha wanakipatia kikundi cha wachimbaji wadogo wa madini kijulikanacho  kwa jina la “Hapa Kazi Tu” kinachoendesha shughuli za uchimbaji wa madini aina ya sunstone katika kijiji cha Suguta wilayani Kongwa mkoani Dodoma leseni ya uchimbaji madini ndani ya mwezi mmoja kwa kufuata kanuni na sheria za madini.

Profesa Kikula alitoa agizo hilo tarehe 05 Septemba, 2018 katika  machimbo ya madini hayo yaliyopo katika kijiji hicho kwenye ziara yake ya siku mbili katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo, kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.

Katika ziara hiyo, Profesa Kikula aliambatana na Makamishna wa Tume, Profesa Abdulkarim Mruma na Haroun Kinega, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA),  Kulwa Mkalimoto, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya pamoja na waandishi wa habari.

Mara baada ya kusikiliza kero za wachimbaji wadogo hao Profesa Kikula mbali na kutoa  agizo hilo alimwelekeza Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA),  Kulwa Mkalimoto, kuhakikisha anasaidia kikundi cha wachimbaji wadogo hao katika taratibu zote za usajili wa kikundi  kabla ya kuanza kushirikiana na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma katika upatikanaji wa leseni ndani ya mwezi mmoja.

Aidha, Profesa Kikula alimtaka Mwenyekiti huyo kuwasaidia wachimbaji hao katika usajili kwenye vyama vya  wachimbaji madini Tanzania pamoja na utafutaji wa masoko na bei elekezi kwenye masoko ya kimataifa.

“Kutokana na kuwa na mtandao mkubwa na uelewa kwenye masoko na bei elekezi za madini kwenye masoko ya kimataifa, nakuelekeza kama Mwenyekiti wa wachimbaji kuhakikisha unawasaidia wachimbaji hawa hususan kwenye maeneo ya masoko na bei elekezi ili uchimbaji wao uwanufaishe wao na Serikali kupata mapato stahiki,” alisema Profesa Kikula.

Profesa Kikula alisema Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia uboreshaji wa sheria na kanuni za madini pamoja na utoaji wa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu sheria na kanuni hizo.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula aliwataka wachimbaji wadogo nchini kuhakikisha kupitia viongozi wao kwenye vyama vya  wachimbaji madini wanashirikiana kwa karibu na viongozi wa vijiji, wilaya na ofisi za madini ili uchimbaji wao ulete tija zaidi kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Awali, wakiwasilisha kero mbalimbali wachimbaji hao walisema kuwa wamekuwa wakikutana na vikwazo mbalimbali kwenye usajili wa kikundi chao hali iliyopelekea ucheleweshwaji wa maombi ya leseni.

Akizungumza kwa niaba ya kikundi hicho, Job Pandila alisema awali waliwasilisha maombi yao kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ajili ya taratibu za usajili lakini kumekuwa na ugumu katika usajili wa kikundi chao kutokana na kutokuwa na uelewa wa namna bora ya kuwasilisha viambatisho kwenye maombi ya usajili wa kikundi.

Pandila aliendelea kusema kuwa uchelewaji wa usajili wa kikundi umepelekea kushindwa kuomba leseni ya madini na kuomba msaada katika usajili wa kikundi pamoja na maombi ya leseni ili waendelee na uchimbaji wa madini na kujipatika kipato.

Awali kabla ya kufika katika kijiji cha Suguta, Profesa Kikula alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembie na kuelezwa changamoto mbalimbali kwenye shughuli za uchimbaji madini zilizopo katika wilaya ya Kongwa.

Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembie alisema kumekuwepo na mgogoro kwenye eneo la Suguta lililopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma kutokana na wachimbaji wengi kutokuwa na leseni za uchimbaji madini pamoja na uelewa mdogo wa sheria na kanuni za uchimbaji madini.

Aidha,  Ndejembie alimpongeza Profesa Kikula na timu yake kwa kutembelea wilaya ya Kongwa na kusisitiza kuwa ziara hiyo mbali na kutoa elimu kwa wachimbaji madini, itapunguza migororo isiyo na lazima iliyokuwa ikijitokeza.

Wakati huo huo katika kikao chake na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Profesa Kikula aliwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini kuandaa utaratibu wa utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji madini kuhusu sheria na kanuni za uchimbaji madini.

Katika ziara hiyo Profesa Kikula pamoja na ujumbe wake, walitembelea pia machimbo ya Rays Metal Corporation na Tambi Minerals Resources yaliyopo katika kijiji cha Tambi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembie. Kushoto ni Kamishna wa Tume ya Madini, Haroun Kinega. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Deogratius Ndejembie (kulia) mara baada ya kumalizika kwa kikao kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo. 

Kutoka kushoto, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya, Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Deogratius Ndejembie na Kamishna wa Tume ya Madini, Haroun Kinega wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kikao hicho. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) na Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma (kulia) wakiangalia moja ya mawe ili kubaini madini yaliyomo kwenye machimbo ya Suguta yaliyopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma. 

Sehemu ya wachimbaji wadogo wa madini wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (hayupo pichani) kwenye machimbo ya Suguta yaliyopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma. 

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara kwenye kwenye machimbo ya Suguta yaliyopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma. 

Mmoja wa watendaji wa migodi ya shaba ya Rays Metal Corporation na Tambi Minerals Resources iliyopo katika kijiji cha Tambi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma akitoa ufafanuzi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (katikati). Kulia ni Kamishna wa Tume ya Madini, Haroun Kinega. 

Sehemu ya mgodi wa shaba wa Rays Metal Corporation uliopo katika kijiji cha Tambi wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

No comments:

Post a Comment