·
Abaini raia wa
kigeni 10 wasio na vibali vya kazi waliokuwa wamejificha ndani ya mgodi
·
Atoa wiki moja
mikataba ya ajira kwa wafanyakazi
Na Greyson Mwase, Musoma
Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko leo tarehe 29 Agosti, 2018 amefanya ziara ya
kushtukiza katika Mgodi wa Dhahabu wa MMG unaomilikiwa na kampuni ya Waarmenia uliopo
katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara.
Mara
baada ya kuwasili katika mgodi huo na kupata maelezo ya namna ya uendeshaji wa
mgodi huo kutoka kwa Meneja Uendeshaji,
Sezgey Sazgyyan aliendelea na
ukaguzi wa mgodi na kubaini ukiukwaji wa
kanuni za usalama migodini ikiwa ni pamoja na watumishi kufanya kazi katika mazingira hatarishi pasipokuwa
na vifaa vya usalama mgodini.
Mara
baada ya kutoa maelekezo, Naibu Waziri Biteko alifanya kikao na uongozi wa
mgodi pamoja na wafanyakazi wa mgodi huo lengo likiwa ni kusikiliza kero
mbalimbali pamoja na kuzitatua.
Akitoa
maelezo kuhusu idadi ya wataalam wa kigeni na wa kitanzania katika mgodi huo
wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya
utekelezaji wa shughuli za mgodi huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 Afisa
Utumishi wa mgodi huo, Rose Masanja
alisema mgodi mpaka sasa una wafanyakazi 126 wa kitanzania ambao ni pamoja na
vibarua kutoka katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa mgodi na wataalam watatu
kutoka nje ya nchi.
Mara
baada ya kupokea taarifa hiyo, Naibu Waziri Biteko alimbana Masanja na kumtaka
kutoa taarifa sahihi kuhusu idadi ya
wataalam wa kigeni wanaofanya kazi kwa kuwa taarifa zote anazo kiganjani mwake
kabla ya kufanya ziara katika mgodi huo.
Mara
baada ya kauli ya Naibu Waziri Biteko, Masanja alieleza kuwa kuna wafanyakazi
wa kigeni takribani 10 wasio na vibali vya kazi na wamejificha ndani ya vyumba
na kuelekeza kwenye vyumba walivyojificha.
Naibu
Waziri Biteko akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Vicent Anney, Meneja
Uendeshaji wa Mgodi huo, Sezgey Sazgyyan
alielekea kwenye vyumba walivyojificha na kufanya msako na kubaini
watumishi wa kigeni wasio kuwa na vibali wamejificha kwenye vitanda.
Aidha,
Biteko alibaini baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo waliokuwa wamefungiwa chooni
kwa takribani masaa matatu na uongozi ili kuficha aibu ya kutokuwa na vifaa
usalama migodini.
Biteko
alimwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Vicent Anney kuwachukulia hatua za
kisheria wafanyakazi hao ambapo bila kusita Mkuu wa Wilaya huyo alielekeza
Ofisi ya Wilaya ya Uhamiaji kufika muda huohuo kuwakamata na kuwafikisha kwenye
ofisi hizo kwa ajili ya kutoa maelezo.
Katika
hatua nyingine, Biteko alisikiliza kero mbalimbali za watumishi wa mgodi huo
ambapo alielezwa kuwa watumishi wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira ya
shida ikiwa ni pamoja na kukosa huduma zote muhimu kama maji salama na
matibabu.
Akizungumza
kwa niaba ya watumishi wenzake, Afisa
Usalama wa Mgodi huo, Stephen Wambura
alisema watumishi wa kitanzania wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira yasiyo
salama bila kuwa na mikataba ya ajira na pale alipokuwa akiushauri uongozi wa
mgodi kutatua changamoto hizo alikuwa akiambulia matusi.
“Mheshimiwa
Naibu Waziri, tunashukuru sana kwa kufanya ziara katika mgodi huu kwani
tumekuwa tukifanya kazi kama watumwa huku tukikosa huduma muhimu hali
inayohatarisha usalama wa afya zetu,” alisema Wambura.
Naye
Zuwena Swedi ambaye ni muuguzi wa kituo cha huduma ya kwanza cha mgodi huo
aliongeza kuwa amekuwa akifanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na
kutopewa muda wa kutosha kupumzika hasa ikizingatiwa kuwa ni mama wa mtoto
mchanga.
Wakati
huo huo akihitimisha kikao hicho, Naibu Waziri Biteko alitoa wiki moja kwa
uongozi wa Mgodi kuhakikisha umesaini mikataba na watumishi.
Alisema
kuwa Serikali inawakaribisha wawekezaji kufanya shughuli za utafutaji na
uchimbaji wa madini nchini, hivyo wawekezaji wanaowekeza nchini wanatakiwa kufuata
sheria na kanuni za utafiti na uchimbaji wa madini.
“Ni lazima wawekezaji wakahakikisha kuwa wanafuata kanuni na sheria za madini
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watumishi wa kitanzania wanafanya shughuli za
utafutaji na uchimbaji madini katika mazingira yaliyo salama kwa afya na kupata
stahiki zao kwa wakati,” alisisitiza Biteko.
Alisema
kuwa, katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaongeza mchango wake kwenye
pato la taifa, serikali imeboresha sheria na kanuni za madini ambazo zitakuwa
na manufaa kwa watanzania na wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Mara, Vicent Anney akizungumza katika kikao hicho aliwataka
watumishi wa mgodi kutoa taarifa zozote za ukiukwaji wa sheria na kanuni za
nchi na madini na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kwa ajili
ya kuwatetea.
Pamoja
na ziara katika mgodi huo, Naibu Waziri Biteko alifanya ziara katika machimbo
ya wachimbaji wadogo yaliyopo katika eneo la Ikungwi, Musoma Vijijini na kuwataka wachimbaji hao kutotumia zebaki
katika uchenjuaji wa madini.
Meneja
Uendeshaji wa Mgodi wa Dhahabu wa MMG, Sezgey Sazgyyan (kulia) akitoa ufafanuzi
kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye mgodi huo kwa ajili
ya ziara yake tarehe 29 Agosti, 2018.
Sehemu
ya watumishi wa Mgodi wa Dhahabu wa MMG wakisikiliza maelekezo yaliyokuwa
yanatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) katika kikao
chake na uongozi na watumishi hao.
Afisa
Usalama wa Mgodi wa Dhahabu wa MMG, Stephen Wambura akiwasilisha kero yake
mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani).
Sehemu
ya raia wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi katika Mgodi wa Dhahabu wa MMG
pasipokuwa na vibali vya kazi nchini.
Sehemu
ya Mgodi wa Dhahabu wa MMG uliopo wilayani Musoma mkoani Mara.
|
Wachimbaji wadogo wanakumbana na changamoto ya chemicals kupanda bei kiholela mfano sodium cyanide ilikua ina uzwa 390000 kwa mwezi wa 7lakini kwa sasa ni 470000, wizara fanyeni kuwasaidia wachimbaji wadogo maana wanaumia na pili wanachangia kodi
ReplyDelete