Na
Greyson Mwase, Dodoma
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ametoa mwezi mmoja kwa Mwenyekiti wa
Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto
na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya kuhakikisha
mgogoro katika machimbo ya madini aina ya rubi yaliyopo katika kijiji cha Winza
kilichopo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma unamalizika ili wachimbaji hao
waendelee na shughuli zao za uchimbaji madini na kujipatika kipato.
Profesa
Kikula ametoa agizo hilo mara baada ya kupokea kero za wachimbaji wadogo wa
madini katika eneo hilo katika ziara yake katika wilaya ya Mpwapwa yenye lengo
la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero
mbalimbali za wachimbaji wadogo wa madini.
Katika
ziara hiyo Profesa Kikula aliambatana na Makamishna wa Tume, Profesa Abdulkarim
Mruma na Haroun Kinega, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini
mkoani Dodoma (DOREMA), Kulwa Mkalimoto,
Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Nicas Sangaya pamoja na waandishi
wa habari.
Alimtaka
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma
(DOREMA), Kulwa Mkalimoto na Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma,
Nicas Sangaya kushirikiana kwanza kwa kuchukua alama za eneo (coordinates) ili
kubaini maeneo yasiyo na leseni na kuwapatia wachimbaji hao ili wafanye
uchimbaji bora wenye kufuata sheria na kanuni za madini.
Aliendelea
kufafanua kuwa, kwa maeneo yenye leseni wachimbaji wadogo wa madini wanaweza
kuangalia namna ya kushirikiana na wamiliki wa leseni kwa kuingia ubia na
kujipatia kipato pasipo migogoro isiyo ya lazima.
Profesa
Kikula alisisitiza kuwa lengo la Serikali kupitia Tume ya Madini ni kuona
wachimbaji wadogo wa madini wanafanya shughuli zao katika mazingira mazuri kwa
kufuata kanuni na sheria za madini.
Katika
hatua nyingine, Profesa Kikula aliwataka wachimbaji hao kuunda vikundi vidogo
na kuomba leseni na kusisitiza kuwa Tume ya Madini ipo tayari kuwasaidia kwa njia zote kupitia wataalam wake
ikiwa ni pamoja na namna ya kuomba leseni za madini, elimu kuhusu kanuni na
sheria za madini.
Wakiwasilisha
kero zao kwa Mwenyekiti Kikula kwa nyakati tofauti, wachimbaji hao walisema
kuwa wamekuwa wakifanya shughuli zao kwa muda mrefu pasipokuwa na leseni huku
kukiwepo na watu wanaojitokeza na kudai kuwa ni wamiliki halali wa leseni za
madini.
Awali
akielezea historia ya ugunduzi wa madini aina ya rubi katika eneo hilo,
mgunduzi ambaye ni mwenyeji wa kijiji hicho,
Shabani Kigelulye alisema kuwa, kati ya mwaka 2005 na 2006 akiwa
shambani kwake katika eneo hilo aligundua mawe aliyohisi kuwa ni madini ya
rubi.
Alieleza
kuwa, katika harakati za utafiti wa
madini hayo mwaka 2007 alipeleka sampuli za mawe hayo aliyohisi kuwa ni
madini ya rubi kwa ndugu wake walioko Dodoma Mjini na Arusha na kuelezwa kuwa
yalikuwa ni madini ya rubi.
Aliendelea
kueleza kuwa kwa kushirikiana na ndugu zake alipeleka sampuli hizo za mawe
kwenye Ofisi za Madini na kushauriwa kuomba leseni na kupata.
Aliongeza
kuwa mwaka 2008 aliingia ubia na wenzake Roja Sezinga, Johnson Kamara na
Perfect Shayo na kuanza uchimbaji wa madini, na kusisitiza kuwa mwaka 2009
wakazi wengi wa kijiji hicho waliingia na kuanza kuchimba kiholela pasipokuwa
na leseni hali iliyopelekea mgogoro.
Katika
hatua nyingine Profesa Kikula alitembelea eneo lililopangwa kujengwa mtambo wa
kuyeyushia shaba na kukuta jengo lililotelekezwa tangu mwaka 2004
Mwenyekiti
wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini mkoani Dodoma (DOREMA), Kulwa
Mkalimoto alimweleza Profesa Kikula na timu yake kuwa, kampuni ya Igozomo
kutoka China ilipanga kujenga mtambo wa kuyeyushia shaba lakini baadaye
walisitisha uwekaji wa mtambo huo baada ya kutoelewana na wazawa.
Profesa
Kikula alishauri wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza kwenye shughuli za
madini nchini kukutana na wenyeviti wa vyama vya wachimbaji madini ambao
wanaweza kuwapa taratibu sahihi za uwekezaji nchini hivyo kuepuka kuingia
kwenye mikono ya matapeli.
Wakati
huohuo akiwa katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba,
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alisema kuwa suala ushiriki
wa huduma za jamii (corporate social responsibility) kwa makampuni ya madini
nchini si la hiari bali ni moja ya sheria.
Aliendelea
kufafanua kuwa ni vyema kukawepo mikataba kati ya wakuu wa wilaya na kampuni za
madini kuhusu maeneo yanayohitaji katika uboreshaji wa huduma za jamii na
kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na huduma zilizoainishwa kwenye mikataba
na kupunguza migogoro.
“
Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka
mikakati ya kuhakikisha wananchi wote wananufaika na rasilimali za
madini kupitia ushirikishwaji wananchi kwenye utoaji wa huduma kwenye kampuni
za madini (local content) na kupata huduma bora za jamii kutokana na uwekezaji
unaofanywa na kampuni za madini,” alisisitiza Profesa Kikula.
Akielezea
mikakati ya kumaliza migogoro kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini
nchini, Profesa Kikula alisema kuwa Tume ya Madini inaandaa rasimu ya mfumo wa
utatuzi wa migogoro kuanzia kwenye ngazi
ya kijiji, kata na wilaya kabla ya kufikia ngazi ya tume.
Naye
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba alimpongeza na kumshukuru
Profesa Kikula pamoja na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutatua
changamoto kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wa madini na kutoa elimu kuhusu
sheria na kanuni za madini
Aidha
Komba aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kutoa taarifa za wavamizi wasiokuwa
na leseni za madini ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Kwa
upande wake Kamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma akizungumza
katika mahojiano maalum na vyombo vya habari aliwataka wananchi wanaogundua
madini kwenye maeneo yao kutoa taarifa kwenye ofisi za vijiji na vyama vyama vya
wachimbaji madini na kufika kwenye Ofisi za Madini kwa ajili ya utambuzi wa madini na kuelekezwa namna ya kuomba leseni.
Alisema
kutokana na wagunduzi wengi kuchimba bila kushirikisha uongozi wa kijiji,
wilaya na vyama vya wachimbaji madini wamejikuta wakitoa mwanya kwa wajanja
kuomba leseni hivyo kuzalisha migogoro isiyokwisha.
Alisema
kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini
imeweka utaratibu mzuri sana wa kumlinda mgunduzi wa madini tangu anapogundua
madini hayo hadi kupata leseni.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kushoto) akisalimiana na Katibu Tawala
wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba (kulia) mara baada ya kuwasili kweye Ofisi ya
Katibu Tawala huyo.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akielezea mikakati ya Tume ya Madini
kwenye uwezeshaji wa wachimbaji wadogo wa madini nchini kwenye ofisi ya Katibu
Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba.
Kamishna
wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma akisaini kitabu cha wageni mara
baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya kijiji cha Winza kilichopo wilayani Mpwapwa
mkoani Dodoma.
Jengo
lililojengwa kwa ajili ya kusimikwa mtambo wa kuyeyushia shaba na kampuni ya Igozomo
ya China lililopo katika kijiji cha Winza wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) akizungumza na wachimbaji
wadogo wa madini katika machimbo ya Winza yaliyopo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Kamishna
wa Tume ya Madini, Haroun Kinega (kushoto) akifafanua jambo alipokuwa
akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika machimbo ya Winza yaliyopo
wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment