Na Greyson Mwase,
Dodoma
Mwenyekiti wa Tume ya
Madini, Profesa Idris Kikula leo tarehe 13 Septemba, 2018 amekutana na Balozi
wa India Nchini, Sandeep Arya jijini Dodoma. Lengo la ziara ya Balozi Arya kwenye
Ofisi ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini lilikuwa ni kujitambulisha pamoja na
kufahamu majukumu ya Tume.
Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Kikula alieleza
kuwa Tume ya Madini imejipanga kusimamia Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 na kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya
madini nchini.
Alisema Sheria ya Madini ina matakwa yake kama vile local
content, utoaji wa huduma kwa jamii kwenye shughuli za uchimbaji madini (corporate social responsibility) na
kiapo cha uadilifu kwenye shughuli za uchimbaji madini (integrity pledge).
Alisema kuwa Tume imejipanga pia kutoa leseni haraka
iwezekanavyo na kuwasaidia wachimbaji wadogo.
Akizungumzia namna Tume ya Madini ilivyojipanga katika
kutatua changamoto ya migogoro kwenye Sekta ya Madini Nchini, Profesa Kikula
alisema kuwa Tume inaandaa mpango wa
kutatua migogoro kuanzia katika ngazi ya kijiji, kata, wilaya na taifa kwa
ujumla.
Alisema kuwa migogoro mingi inatatulika katika mamlaka
za Vijiji, Kata na Wilaya.
Aidha, Profesa Kikula alimwomba Balozi wa India
kuendelea kutoa ufadhili kwa wataalam wa Tume ya Madini hususan katika maeneo ya Uchimbaji wa Madini kwa
kutumia teknolojia ya kisasa, Usimamizi wa Rasilimali Watu na maeneo mengine ili
kukuza Sekta ya Madini Nchini.
“ Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini
inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, na kama Tume kwa kushirikiana na Wizara ya Madini tumejipanga kuhakikisha
tunakuwa na wataalam wenye weledi kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini. Hivyo basi mafunzo kwa wataalam
tunayapa kipaumbele sana,” alisisitiza Profesa Kikula.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula alimwomba Balozi
wa India kuendelea kutangaza Sekta ya Madini Nchini na kusisitiza kuwa Tanzania
ina maeneo mengi yenye madini yaliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).
Alisisitiza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya
aina mbalimbali.
Wakati huo huo Balozi wa India Nchini, Sandeep
Arya alisema kuwa nchi ya India ipo
tayari kushirikiana na Tume ya
Madini hususan katika Sekta ya Madini na
kusisitiza kuwa wapo tayari kutoa ufadhili kwa watumishi wa Tume.
Aliendelea kusema kuwa nchi ya India imekuwa ikitoa
mafunzo ya muda mrefu hususan katika
ngazi za Shahada za Uzamili na za Uzamivu katika vyuo bora na kusisitiza kuwa
itaendelea na mpango wake wa kutoa mafunzo hususan kwenye masuala ya madini.
Katika hatua nyingine,
Balozi Arya alimpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris
Kikula kwa kuteuliwa kuongoza Tume hiyo pamoja na kazi nzuri inayofanywa na
Tume ya Madini kwenye uboreshaji wa Sekta ya Madini Nchini.
Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (kushoto)
akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) mara
baada ya kuwasili kwenye Ofisi za Mwenyekiti wa Tume zilizopo jijini Dodoma
Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya akisaini kitabu
cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye
Ofisi za Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula zilizopo jijini Dodoma
Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (kushoto)
akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula
(kulia)
|
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula
akielezea majukumu ya Tume ya Madini kwa
Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya (hayupo pichani)
|
Balozi wa India Nchini, Sandeep Arya akifafanua jambo
kwenye kikao hicho
|
No comments:
Post a Comment